Dalili za Qur-aan na Sunnah kuthibitisha adhabu ya kaburini

Dalili za Ahl-us-Sunnah, Salaf wa Ummah huu na maimamu juu ya kwamba neema na adhabu zinakuwa kwenye roho na mwili kutoka katika Qur-aan na Sunnah. Dalili za Qur-aan ni hizi zifuatazo:

1- Allaah (Ta´ala) amesema:

وَحَاقَ بِآلِ فِرْعَوْنَ سُوءُ الْعَذَابِ النَّارُ يُعْرَضُونَ عَلَيْهَا غُدُوًّا وَعَشِيًّا ۖ وَيَوْمَ تَقُومُ السَّاعَةُ أَدْخِلُوا آلَ فِرْعَوْنَ أَشَدَّ الْعَذَابِ

“Na watu wa Fir’awn ikawazunguka adhabu mbaya. Wanadhihirishiwa Moto asubuhi na jioni na Siku kitaposimama Qiyaamah [kutasemwa]: “Waingizeni watu wa Fir’awn katika adhabu kali kabisa.”” (40:45-46)

Kinacholengwa katika Aayah ni kuwa Allaah ameeleza kuwa wanaonyeshwa adhabu asubuhi na jioni na halafu akamalizia kwa kusema:

وَيَوْمَ تَقُومُ السَّاعَةُ أَدْخِلُوا آلَ فِرْعَوْنَ أَشَدَّ الْعَذَابِ

“… na Siku kitaposimama Qiyaamah [kutasemwa]: “Waingizeni watu wa Fir’awn katika adhabu kali kabisa.””

Hii ni dalili yenye kuonesha kuwa adhabu ya kwanza ni ndani ya kaburi kabla ya siku ya Qiyaamah. Hii ni dalili yenye kuthibitisha adhabu ya kaburi.

2- Allaah (Ta´ala) amesema:

فَذَرْهُمْ حَتَّىٰ يُلَاقُوا يَوْمَهُمُ الَّذِي فِيهِ يُصْعَقُونَ يَوْمَ لَا يُغْنِي عَنْهُمْ كَيْدُهُمْ شَيْئًا وَلَا هُمْ يُنصَرُونَ وَإِنَّ لِلَّذِينَ ظَلَمُوا عَذَابًا دُونَ ذَٰلِكَ وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَهُمْ لَا يَعْلَمُونَ

“Basi waachilie mbali mpaka wakutane na Siku yao ambayo humo watakumbana na mngurumo angamizi. Siku ambayo njama zao hazitowafaa kitu chochote na wala wao hawatonusuriwa. Na hakika wale waliodhulmu watapata adhabu nyingine isiyokuwa hiyo, lakini wengi wao hawajui.” (52: 45-47)

Kinacholengwa ni Kauli Yake:

عَذَابًا دُونَ ذَٰلِكَ

“… adhabu nyingine isiyokuwa hiyo.”

Inawezekana ikawa ni adhabu chini ya hapo kwa mauaji na mengineyo duniani na inawezekana vilevile ikawa ni adhabu ndani ya kaburini na hili ndio dhahiri. Kwa sababu wengi katika wao wamekufa na hawakuadhibiwa duniani. Au inawezekana vilevile makusudio yake ikawa imeenea zaidi kuliko hivo na ikawa inahusu yote mawili; wakaadhibiwa duniani na ndani ya kaburi. Kwa hali yoyote kuna uthibitisho wa adhabu ya kaburi.

Kuhusiana na Sunnah kumepokelewa mapokezi mengi kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) juu ya uthibitisho wa adhabu na neema za kaburi kwa yule mwenye kustahiki hayo. Mapokezi haya yamepokelewa kwa njia nyingi kimaana na si kimatamshi kwa kitu ambacho kinafidisha yakini. Hivyo basi ni wajibu kuitakidi kuthibiti kwa hilo na kuliamini na mtu asizungumzie namna yake kwa sababu akili haiwezi hilo. Miongoni mwa dalili hizi ni:

1- Hadiyth ya Baraa´ bin ´Aazib (Radhiya Allaahu ´anh) ambapo ndani yake mna:

“Ninajilinda kwa Allaah kutokana na adhabu ya kaburi.” Abu Daawuud (4753).

Ndani yake vilevile mna kisa cha mja muumini ambapo atasema:

“Ee nafsi nzuri! Toka kwenye msamaha na radhi za Allaah.” Kisha akasema: “Itatoka kama linavyotoka tone kwenye chombo cha maji.” Ndani yake mna: “Atanadi mwenye kunadi kutoka mbinguni: “Amesema kweli mja Wangu, mwikalisheni Peponi na mumfungulie mlango wa Peponi” kisha akaendelea kusema: “Ajiwe na harufu na manukato ya Peponi.” Ama kuhusu kafiri ataambiwa: “Ee mwenye nafsi chafu! Toka kwenye khasira na ghadhabu za Allaah” kisha akaendelea kusema: “Roho itatoka kwenye mwili wake, wataivuta kama chuma cha moto kitokavyo kwenye pamba zilizolowa.” Ndani yake mna: “Atanadi mwenye kunadi kutoka mbinguni: “Amesema uongo, mwikalisheni na mumfungulie mlango wa Motoni” na ajiwe na joto lake.”

Ahl-us-Sunnah wal-Hadiyth wamesimama upande wa yenye kuwajibisha Hadiyth hii na ina yenye kuyatilia nguvu katika “as-Swahiyh” ikiwa ni pamoja na yale aliyotaja al-Bukhaariy (Radhiya Allaahu ´anh) kutoka kwa Sa´iyd bin Qataadah kutoka kwa Anas (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mja anapowekwa kwenye kaburi lake na watu wake wakamuacha husikia mlio wa viatu vyao.”

Mpaka alipofikia kusema:

“Ama kuhusu muumini husema “Ninashuhudia kuwa yeye ni mja na Mtume wa Allaah.” Kisha ataambiwa: “Tazama makazi yako Motoni ambapo Allaah amekubadilishia kwa kukupa makazi Peponi” na atayaona yote mawili.”

Qadaatah anaendelea kusema:

“Tumesimuliwa pia kuwa: “Atakunjuliwa kaburi lake.” al-Bukhaariy (1374) na Muslim (2870).

Hii ni Hadiyth ya pili.

3- Yaliyokuja katika “as-Swahiyh” ya al-Bukhaariy na “as-Swahiyh” ya Muslim kupitia kwa Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ambaye ameeleza “Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipita kwenye makaburi mawili na akasema “Hawa wanaadhibiwa na hawaadhibiwi kwa kubwa; kuhusu mmoja wao alikuwa hajisitiri kutokana na mkojo na mwingine alikuwa anaeneza uvumi… “

4- Katika “as-Swahiyh” ya Ibn Haatim kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mmoja wenu anapotiwa kwenye kaburi lake hujiwa na Malaika wawili wa rangi nyeupe bluu ambapo mmoja wao anaitwa Munkar na mwingine Nakiyr… “

5- Katika “as-Swahiyh” ya Muslim kupitia kwa Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ambaye ameeleza kuwa:

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akitufunza du´aa hii kama anavyotufunza Suurah katika Qur-aan akisema “Ee Allaah! Ninakuomba unikinge na adhabu ya Jahannam, unikinge na adhabu ya kaburi, unikinge na fitina ya al-Masiyh ad-Dajjaal na unikinge na fitina ya waliohai na waliokufa.”

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajhiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Hidaayah ar-Rabbaaniyyah fiy Sharh al-´Aqiydah at-Twahaawiyyah (02/617-618)
  • Imechapishwa: 19/05/2020