Uhakika wa Ahl-us-Sunna juu ya kuonekana kwa Allaah Aakhirah ni kwamba wameshikamana na Qur-aan na Sunnah na wametolea dalili kwa maandiko mengi kutoka katika Kitabu cha Allaah na Sunnah za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) juu ya kuthibitisha kuonekana kwa Allaah Aakhirah. Kadhalika wametumia dalili ya maafikiano na akili ya wazi. Dalili zao ni nyingi katika maudhui haya ikiwa ni pamoja na:

Dalili kutoka katika Qur-aan Tukufu:

Dalili ya kwanza: Allaah (Ta´ala) amesema:

لَهُم مَّا يَشَاءُونَ فِيهَا وَلَدَيْنَا مَزِيدٌ

“Watapata humo wayatakayo, na Kwetu kuna yaliyo ziada” (50:35)

Bi maana waumini.

لَهُم مَّا يَشَاءُونَ فِيهَا

“Watapata humo wayatakayo… “

Yaani Peponi.

وَلَدَيْنَا مَزِيدٌ

“… na Kwetu kuna yaliyo ziada.”

Bi maana kumuona Allaah Aakhirah. Wanachuoni wamefasiri kuwa neno “ziada” ya kwamba ni kumuona Allaah Aakhirah.

Dalili ya pili: Allaah (Ta´ala) amesema:

لِّلَّذِينَ أَحْسَنُوا الْحُسْنَىٰ وَزِيَادَةٌ

“Kwa wale waliofanya mazuri watapata Pepo na zaidi.” (10:26)

أَحْسَنُوا الْحُسْنَىٰ وَزِيَادَةٌ

“… waliofanya mazuri watapata Pepo na zaidi.”

“al-Husnaa” bi maana Pepo. Ina maana kuona Uso wa Allaah Mtukufu kama ilivokuja tafsiri ya hilo katika Hadiyth Swahiyh ambayo ameipokea Imaam Muslim ambapo amesema:

“Ziada ni kuona Uso wa Allaah Mtukufu.” Muslim (181)

Dalili ya tatu: Allaah (Ta´ala) amesema:

وُجُوهٌ يَوْمَئِذٍ نَّاضِرَةٌ إِلَىٰ رَبِّهَا نَاظِرَةٌ

“Kuna nyuso siku hiyo zitanawiri. Zikimtazama Mola wake.” (75:22-23)

makusudio “Dhwaad” hapa ambapo imefuatiwa na “Ilaa” ni kuona kwa macho ya usoni kumuona Mola (Jalla Jallaaluh).

Dalili ya nne: Allaah (Ta´ala) amesema:

كَلَّا إِنَّهُمْ عَن رَّبِّهِمْ يَوْمَئِذٍ لَّمَحْجُوبُونَ

“Hapana! Hakika wao siku hiyo watawekewa kizuizi [wasimuone] Mola wao.” (83:15)

Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) ameeleza kuwa makafiri watazuiwa kumuona Allaah. Hii ni dalili inayoonesha kuwa vipenzi Wake watamuona. Vinginevyo ingelikuwa na waumini wao pia hawatomuona Mola Wao basi kungelikuwa hakuna tofauti kati yao na makafiri katika kuzuiwa. Pale ambapo makafiri watakuwa ni wenye kuzuiwa ikawa ni dalili yenye kuonesha kuwa waumini watamuona Allaah na hawatozuiwa. Imaam ash-Shaafi´iy pia (Rahimahu Allaah) alitolea dalili kwa hili. Amesema:

“Pale ambapo watu hawa (makafiri) watakuwa ni wenye kuzuiwa katika hali ya khasira, ikawa ni dalili yenye kuonesha kuwa mawalii wake watamuona katika hali ya furaha.”

Hizi ni dalili kutoka katika Kitabu Kitukufu ambazo zinaonesha kuwa waumini watamuona Mola Wao siku ya Qiyaamah.

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajhiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Hidaayah ar-Rabbaaniyyah fiy Sharh al-´Aqiydah at-Twahaawiyyah (01/219-221)
  • Imechapishwa: 30/05/2020