Dalili za kimaumbile za Salaf kuthibitha kuwepo Allaah juu

Dalili za Salaf, maimamu na Ahl-us-Sunnah juu ya kuthibitisha kuwepo juu kwa Allaah kutokana na maumbile:

Wametoa dalili ya kimaumbile: Viumbe wote kutokana na maumbile yao na nyoyo zao zilizosalimika hunyanyua mikono yao wakati wa kuomba du´aa kuielekeza mbinguni na hukusudia kwa kufanya hivo upande wa juu wakati wa kumnyenyekea Allaah (Ta´ala). Hili ni jambo la kimaumbile ambalo Allaah amewaumba kwalo waja Wake pasina kulipokea kutoka kwa Mitume. Wanahisi mioyoni mwao maumbile ya kidharura kumuomba kutokea kwa juu. Yule mjakazi ambaye hakuwa mwarabu ambaye aliambiwa na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Allaah Yuko wapi?” Akajibu: “Mbinguni.”

Mjakazi huyu alijibu hivi kutokana na maumbile ambayo Allaah amemuumba nayo na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akawa amemkubalia kwa hilo na bali akamshuhudilia imani.

Wapinzani wanaopinga kuwepo juu kwa Allaah wamepingana na hili kwa sababu mbili:

1- Sababu ya kwanza: Kule mtu kunyanyua mikono yake wakati wa kuomba du´aa ni kwa sababu mbingu ndio Qiblah cha du´aa kama ambavyo Ka´bah ndio Qiblah cha swalah na si kwa sababu Allaah Yuko mbinguni.

Hili linaweza kujibiwa kwa majibu yafuatayo:

Jibu la kwanza: Madai yenu ya kusema kuwa mbingu ndio Qiblah cha du´aa ni jambo halikuthibiti katika Qur-aan wala Sunnah na wala halikusemwa na yeyote katika Salaf wa Ummah huu. Hili ni katika mambo yaliyowekwa katika Shari´ah na ya kidini. Hivyo haijuzu likawa ni lenye kufichikana kwa Salaf wa Ummah huu na wanachuoni wao.

Jibu la pili: Qiblah cha du´aa ndio Qiblah cha swalah. Dalili ya hilo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akielekea Qiblah wakati wa kuomba du´aa katika matukio mengi. Hivyo basi, mwenye kudai kuwa du´aa ina Qiblah mbali na Qiblah cha swalah huyo ni mwenye kuzusha katika dini na mwenye kwenda kinyume na mkusanyiko wa waislamu.

Jibu la tatu: Qiblah ndipo mja anapoelekeza uso wake kama anavyoielekea Ka´bah wakati wa kuswali, wakati wa kuomba du´aa, wakati wa Dhikr na wakati wa kuchinja. Zile sehemu ambazo ndani yake ananyanyua mikono yake haiitwi kuwa ni Qiblah. Hili si kwa hakika wala majazi.

Jibu la nne: Lau mbingu ndio ingelikuwa Qiblah cha du´aa basi ingelikuwa ni jambo lililowekwa katika Shari´ah mwombaji du´aa auelekeze uso wake huko. Hili ni jambo ambalo halikuwekwa katika Shari´ah.

Jibu la tano: Qiblah ni jambo ambalo kunakubalika kufutwa na kugeuzwa kama ambavyo Qiblah kilivyogeuzwa kutoka Jerusalemu na kuelekea Ka´bah. Kitendo cha ki-Tawhiyd ambacho ni kuelekeza uso upande wa juu ni la kimaumbile na halikubaliki kugeuzwa.

Jibu la sita: Mwenye kuelekea katika Ka´bah anajua kuwa Allaah hayuko huko. Hili ni tofauti na mwenye kuomba du´aa. Yeye anaelekea kwa Mola na Muumbaji Wake akitaraji huruma Wake umteremkie.

2- Sababu ya pili: Wenye kupinga wanasema kuwa dalili zenu zinapingana mswaliji kuweka paji lake la uso chini katika ardhi pamoja na kwamba Allaah hayuko upande wa ardhi [chini]. Kama jinsi mswaliji anaweka paji lake la uso chini katika ardhi – pamoja na kuwa Allaah hayuko upande wa chini ya ardhi – vivyo hivyo [mswaliji huyo] ananyanyua mikono yake wakati wa kuomba du´aa lakini haina maana kuwa Yuko juu.

Wanajibiwa kwa kuambiwa kuwa mswaliji kuweka paji la uso wake chini ya ardhi analenga kumnyenyekea Yule Aliyeko juu. Anafanya hivo kwa kuonesha unyonge na unyenyekevu wake Kwake. Hafanyi hivo kwa kukusudia kuwa Yuko chini. Hili halihisi yule mwenye kusujudu isipokuwa yenye kusimuliwa kutoka kwa Bishr bin al-Mariysiy ya kwamba alisikiwa akisema ilihali yuko kwenye Sujuud:

سبحان ربي الأسفل

“Ametakasika, Mola wangu, aliyeko chini.”

Allaah amfedheheshe. Allaah ametakasika na hilo utakaso ulio mkubwa kabisa.

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajhiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Hidaayah ar-Rabbaaniyyah fiy Sharh al-´Aqiydah at-Twahaawiyyah (01/414-416)
  • Imechapishwa: 19/05/2020