Cha kufanya kwa anayechenguka wudhuu´ katikati ya swalah na swalah ya aliye na gesi nyingi

Swali: Mtu akipatwa na hadathi ndani ya swalah yake afanye nini akiwa ni imamu au maamuma ana akawa yuko na gesi?

Jibu: Mtu akipatwa na hadathi ndani ya swalah yake basi ni wajibu kwake kutoka ndani ya swalah yake. Haijuzu akabaki ndani yake hata kama atakuwa ni imamu au maamuma. Akiwa ni imamu basi atoke aende akatawadhe na kurudi. Akiwa ni imamu atoke pia na aseme kuwaambia walioko nyuma yake:

“Fulani! Sogea mbele na kamilisha kuwaswalisha watu.”

Katika hali hiyo swalah ya maamuma haiharibiki.

Kadhalika endapo imamu ataingia ndani ya swalah na katikati ya swalah akakumbuka kuwa hana wudhuu´ basi ni wajibu kwake kuondoka na aweke mahala pake mwengine atakayekamilisha swalah yao.

Mtu akiwa na gesi na hawezi kujizuia kwa maana ya kwamba inamtoka hovyo bila kutaka kwake, basi hukumu yake ni kama yule ambaye anatokwa na mkojo hovyohovyo. Hivyo atatakiwa kuwa anatawadha baada ya kuingia wakati wa swalah, ajihifadhi na aswali. Akitokwa na kitu katikati ya swalah yake swalah haiharibiki.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (12/453-454)
  • Imechapishwa: 05/08/2017