Bora kusoma Qu-aan kimyakimya au kwa sauti ya juu?

Swali: Namshukuru Allaah kuona kwamba nasoma Qur-aan vizuri sana karibu na kuhifadhi kichwani. Lakini tatizo langu ni kwamba ninapopaza sauti katika kusoma pasi na msahafu basi mara nyingi hukosea. Je, kuna neno au sipati thawabu nikisoma kimyakimya?

Jibu: Kusoma kimyakimya ndio bora. Hilo ni kutokana na Hadiyth iliyopokelewa na kikosi cha wanachuoni kwa cheni ya wapokezi ilio nzuri kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliyesema:

”Kuisoma Qur-aan kwa sauti ya juu ni kama kutoa swadaqah waziwazi na ambaye anasoma Qur-aan kimyakimya ni kama anayetoa swadaqah kwa kuficha.”

Hii ni dalili inayofahamisha kwamba kusoma kimyakimya ndio bora kama ambavo kutoa swadaqah kwa kujificha ndio bora. Isipokuwa manufaa yakipelekea kusoma kwa sauti ya juu. Kama mfano wa imamu anayewaswalisha watu, Khatwiyb anayewakhutubia watu na ambaye anamsikiliza. Katika hali hiyo asome kwa sauti ya juu ili watu wamsikie na wafaidike.

Ikiwa kusoma kimyakimya kuna manufaa zaidi kwako na kunakusaidia kuhifadhi Qur-aan, bali kunakusadia pia juu ya kusoma vizuri, basi kusoma kimyakimya ndio bora. Isipokuwa ikiwa ndugu zako wanakuhitajia uwasikilizishe. Basi katika hali hiyo wasikilize kutoka kwenye msahafu ili usifanye makosa au angalau uwe na msahafu ukiuhitajia utazame ndani yake au kuweko mtu ambaye amehifadhi ambaye atakufungulia.

Tunacholenga ni kwamba kukiwa kuna manufaa yanayopelekea kusoma kwa sauti ya juu basi itakuwa ndio bora. Kama hakuna haja ya kusoma kwa sauti basi kusoma kimyakimya ndio bora ili uweze kusoma kisomo kizuri.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (05/393)
  • Imechapishwa: 13/02/2021