Mtu ambaye Allaah amemkunjulia kifua chake juu ya hukumu ya kilimwengu, basi utamuona ni mwenye kuridhia mipango na makadirio ya Allaah na mwenye utulivu. Utamsikia akisema:

“Mimi ni mja, Allaah ndiye Mola wangu anafanya akitakacho.”

Mtu anayekuwa katika hali kama hii anakuwa siku zote ni mwenye furaha. Si mwenye kuhisi dhiki wala wasiwasi. Anapata maumivu, lakini haimfikishi kupata msongo wa mawazo au dhiki. Kwa ajili hiyo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Ajabu iliyoje juu ya jambo la muumini. Hakika jambo lake siku zote ni kheri. Hilo haliwi isipokuwa kwa yule ambaye ni muumini. Anapofikwa na kheri, basi husubiri na ikawa ni kheri kwake. Na anapofikwa na dhara, husubiri na ikawa ni kheri kwake.”[1]

Kifua kilichokunjuliwa kinazipokea hukumu za Allaah za kidini na pia hukumu Zake za kilimwengu. Hahisi dhiki kabisa kwa hukumu za Allaah. Mtume wetu Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni mfano mzuri kabisa juu ya hayo. Kwa ajili hiyo utamuona kuwa yeye ndiye mtu mwenye kumcha Allaah zaidi, mwenye kumtii Allaah zaidi na mwenye kusubiri zaidi makadirio ya Allaah. Watu walimfanya nini wakati alipoanza kulingania? Ni maradhi gani yaliyompata? Homa yake ni sawa na homa ya wanamme wawili. Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Niliingia kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ilihali ana homa ya juu. Nikasema: “Ee Mtume wa Allaah! Homa yako ni ya juu kali.” Akasema: “Ndio, mimi hushikwa na homa kama wanavyoshikwa homa wanamme wenu wawili.” Nikasema: “Ni kwa sababu unalipwa mara mbili.” Akajibu: “Ndio. Ni kwa sababu hiyo. Muislamu hapatwi na kutaabika, uzito, maradhi, huzuni, maudhi, dhiki mpaka ule mwiba unaomchoma isipokuwa Allaah humfutia dhambi zake kwayo kama ambavo majani yanavopukuchika kwenye mti.”[2]

Hali ilifikia kiasi cha kwamba alipatwa na maumivu makali kabla ya kufa. Anatengana na dunia akiwa ni mwenye subira ya hali ya juu. Subira ni ngazi ya juu ambayo haifikiwi isipokuwa kwa kuwepo kitu ambacho mtu anakitarajia.

[1] Muslim (2999).

[2] al-Bukhaariy (5648) na Muslim (2571).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tafsiyr al-Qur-aan al-Kariym, Juz’ ´Amma, uk. 247-248
  • Imechapishwa: 22/04/2020