Katika zama hizi, watu wameendelea katika suala la Ruqyah nawameichukulia kuwa riziki na biashara. Wakafungua maduka ya kufanya Ruqyah. Kama ofisi za madaktari. Na wanaichukulia (hiyo Ruqyah) pesa kama wanavyofanya madaktari. Mambo kama haya kunakhofiwa juu yake maangamivu. Kwa kuwa lengo lao ni kuchuma pesa. Na pengine wasijali Halali na Haramu na wala wasijali Ruqyah ya Kishari´ah na Ruqyah ya ki-Shirki. Kwa kutaka kuvuta watu kwao. Maendeleo haya ya Ruqyah kwa kiasi ambacho imekuwa sasa inaogopwa kuingia ndani yake yasiyokubalika Kishari´ah na yasiyojuzu katika Dini ya Allaah (´Azza wa Jall). Hili ni jambo la kwanza.

Jambo la pili ni kuwa, hili halikuwa linajulikana wakati wa Salaf; ya kwamba wanafungua maduka, kutoza pesa na kuajiri wafanya kazi. Hili halikuwa linajulikana kwa Salaf. Salaf walikuwa wanatumia Ruqyah, lakini hawakuwa wanaitumia namna hii. Walikuwa wanaitumia wakati wa haja nayo, bila ya kufanya mambo kama haya, ya kufungua maduka. Nao (Salaf) ni wajuzi zaidi wa yanayojuzu na yasiyojuzu. Lau jambo hili lingekuwa linajuzu, basi wao walikuwa ni watu wenye pupa zaidi ya kuwanufaisha watu. Kutokufanya kwao jambo hili na hawakufungua maduka ya Ruqyah kwa aina hii, tumepata kujua kuwa jambo hili sio Mashru´ah.

Hali kadhalika, miongoni mwa watu kuko wanaotupetuka mipaka katika Ruqyah mpaka wanaitoa katika mipaka ya Kishari´ha na kuipeleka katika mipaka iliyokatazwa. Mnajua kuwa kuko ambao wanawasomea watu kikundi kikubwa na wanaiuza (hiyo Ruqyah) sokoni. Na kuko ambao wanaiuza sokoni na kuhesabu bei yake; hichi ni kisomo cha bei kadhaa na kadhaa, hichi ni kisomo cha bei nafuu na hichi ni kisomo cha bei kali. Huku ni kufanya mchezo na Ruqyah na kuitoa katika mipaka yake ya Kishari´ah kwa kutafuta tu pesa, kutafuta riziki na kutaka kula mali za watu.

Miongoni mwa watu, kuko wanaowasomea kundi la watu kubwa, wagonjwa wanakuwa mbele yake. Anawasomea kwa Microphone (kipazasauti). Je, hii ni katika Ruqyah ya Kishari´ah? Ruqyah ya Kishari´ah ambayo ni maarufu, ni msomaji anamsomea mgonjwa moja kwa moja. Ama kuwasomea idadi kubwa ya watu, makumi ya watu au sehemu ya kikundi na akasomea wote, hili halikuwa linajulikana (kwa Salaf) na ni kuitoa Ruqyah katika asli yake iliyowekwa. Na makusudio yao kwa kufanya hivi ni kutaka kula pesa za watu, anakusanya kikundi kikubwa ili apate kuchua kiwango fulani kwa kila mmoja (anayemsomea). Lau asingelisomea ila mtu mmoja tu au wawili, asingelipata pesa zote hizi. Na huku ni kuifanyia upuuzi Ruqyah na kuitoa katika mipaka yake ya Kishari´ah.

Miongoni mwa watu kuko ambao wanasomea watu kupitia simu nao wanakuwa nje ya mji. Je, hii kweli ni Ruqyah? Na mara nyingi katika hali hii, (msomaji anamwambia msomewaji) “nitumie kiwango cha pesa katika benki na nitakusomea kwenye simu.” Kauli yake: “… na mimi nitakusomea kwenye simu.” Je, kweli kitendo hichi kinaingia katika Ruqyah? Hii kabisa sio Ruqyah ya Kishari´ah.

  • Mhusika: Imaam Swalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://www.youtube.com/watch?v=rv-4tVKEdHA
  • Imechapishwa: 01/04/2018