Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

وَإِن كُنتُمْ فِي رَيْبٍ مِّمَّا نَزَّلْنَا عَلَىٰ عَبْدِنَا فَأْتُوا بِسُورَةٍ مِّن مِّثْلِهِ وَادْعُوا شُهَدَاءَكُم مِّن دُونِ اللَّـهِ إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ

“Mkiwa mko katika shaka kutokana na Tuliyoyateremsha juu ya mja Wetu, basi leteni Suurah mfano wake na waiteni mashahidi wenu pasipo na Allaah mkiwa ni wakweli.”[1]

Hii ni dalili ya kiakili juu ya ukweli wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na ukweli wa yale aliyokuja nayo. Amesema:

وَإِن كُنتُمْ

“Mkiwa mko katika shaka… “

Enyi ambao mnamfanyia ukaidi Mtume, mnaopinga ujumbe wake, mnaodai ni mwongo katika kuwa na shaka kutokana na yale Tuliyoteremsha juu ya mja wetu na kujiuliza kama ni haki au si haki. Hili hapa jambo la ufumbuzi linalotatua mzozo kati yenu: huyo ni mtu kama nyinyi na si mfaswaha wala msomi kuwashinda. Aidha nyinyi mnamjua tokea alipokua kati yenu na kwamba alikuwa ni mtu asiyejua kuandika wala kusoma. Amekujieni na Kitabu ambacho amedai kuwa ni chenye kutoka kwa Allaah ambacho nyinyi mnaonelea kuwa ameibuni na kuziua, mambo yakiwa hivo mnavosema basi leteni Suurah moja mfano wake na watakeni msaada wale wasaidizi na mashahidi wenu wote mnaowaweza kuwafikia, kwani hilo ni jambo jepesi kwenu na khaswa kwa kuzingatia kwamba nyinyi ni watu wenye ufaswaha na mabingwa wa kuzungumza na wenye uadui mkubwa dhidi ya Mtume. Mkileta Suurah moja tu mfano wake basi mambo ni kama mlivodai. Msipoleta Suurah moja mfano wake na mkashindwa kabisa – na hamtoweza kufanya hivo. Lakini tathmini hii ni kwa njia ya inswafu na kushuka pamoja nao.

Hii ni alama kubwa na dalili ya wazi kabisa juu ya ukweli wake na ukweli wa ujumbe aliokuja nao.

[1] 02:23

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdur-Rahmaan bin Naaswir as-Sa´diy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Taysiyr-ul-Kariym, uk. 34
  • Imechapishwa: 11/05/2020