Babu yao Ibaadhiyyah na Mu´attwilah waliozua fitina katika Ummah


Imethibiti ya kwamba mtu wa kwanza kusema kuwa Qur-aan imeumbwa ni al-Ja´d bin Dirham aliyenukuu kutoka kwa myahudi. Hapa chini nakuwekea mlolongo wa hilo.

Ibn Athiyr amesema pindi alipokuwa akimzungumzia al-Jahm bin Swafwaan:

“Maoni yake ya kukanusha sifa za Allaah aliyachukua kutoka kwa al-Ja´d bin Dirham, ambaye na yeye alichukua ukanushaji huu kutoka kwa Abaan bin Sam´aan, ambaye na yeye aliyachukua kutoka kwa Twaaluut, ambaye na yeye aliyachukua kutoka kwa mjomba wake Labiyd bin al-A´swam myahudi ambaye alimfanyia uchawi Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Labiyd alikuwa ni zindiki ambaye anasema kuwa Tawraat imeumbwa.”[1]

Huu ndio mlolongo wenye giza unaoanza kwa myahudi. Huu ndio mlolongo wa Jahmiyyah ambao wanazikanusa sifa za Allaah na vifaranga vyao wengine wanaokanusha sifa za Allaah (´Azza wa Jall). Miongoni mwa sifa hizo ni sifa ya maneno na kusema kuwa Qur-aan imeumbwa kama viumbe vyengine kukiwemo majini, mbingu, ardhi na viumbe vyenginevyo vya Allaah. Hivyo ndivyo anavyoonelea pia al-Khaliyliy. Hii ndio sababu ya kikweli ya chanzo cha kujitokeza kwa fitina ambayo walitumbukia ndani yake wanachuoni wengi wa Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah katika zama za al-Ma´muun, al-Mu´taswim na al-Waathiq mpaka mtihani juu ya Ummah ukaondoshwa kupitia kwa al-Mutawakkil ambaye alikuja kuitokomeza fitina hii ya kuumbwa kwa Qur-aan, Sunnah ikaenea na akaamrisha kueneza Hadiyth za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hayo yalikuwa kwa fadhila za kuwa imara kwa Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) – ambaye ndiye Imaam wa Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah – baada ya Allaah (´Azza wa Jall) kumfanya kuwa ngangari juu ya haki katika kuondosha dhiki kutoka kwa Ummah. Imaam Ahmad alibainisha kuwa Qur-aan ni maneno ya Allaah na kwamba maneno ni sifa miongoni mwa sifa Zake. Anaumba vitu vilivyoumbwa kupitia maneno Yake. Amesema (Ta´ala):

إِنَّمَا أَمْرُهُ إِذَا أَرَادَ شَيْئًا أَن يَقُولَ لَهُ كُن فَيَكُونُ

“Hakika amri Yake anapotaka jambo hukiambia: “Kuwa! – nacho huwa.”[2]

Imaam Ahmad aliwaomba aliokuwa akijadiliana nao mbele ya al-Mu´taswim kuleta Aayah moja kutoka katika Qur-aan au Hadiyth moja kutoka katika Sunnah za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) inayothibitisha kuwa Qur-aan imeumbwa. Lakini hata hivyo wakagonga mwamba.

Hii ndio sababu ya kujitokeza kwa fitina kati ya waislamu. Mambo si kama anavyosema al-Khaliyliy ya kwamba sababu ya kujitokeza kwa fitina ni “Je, maneno ya Allaah ni yenye kuteremshwa, yameumbwa au ni ya tangu hapo kale?” Kwa kuwa istilahi hizi zimeingizwa na Ahl-ul-Bid´ah waliochukua ´Aqiydah yao kutoka katika fikira za mayahudi. Wale wanaosema kuwa Qur-aan imeumbwa wameyapokea hayo kutoka kwa myahudi mchawi Labiyd bin al-A´swam aliyekuwa akisema kuwa Tawraat imeumbwa. Hayo yametangulia kunukuliwa kutoka kwa Ibn Athiyr na wengineo ambao wamesema kuwa mtu wa kwanza kueneza maneno haya ni al-Jahm bin Swafwaan ambaye aliyachukua kutoka kwa al-Ja´d bin Dirham. Huyu ndiye wa kwanza katika Ummah wa Kiislamu aliyesema kuwa Qur-aan imeumbwa ambapo Mu´tazilah wakazipokea fikira zake. Fitina hii ilizimwa wakati wa al-Mutawakkil. Hivi sasa al-Khaliyliy anataka kuwasha moto wake katika kitabu chake hichi pamoja na kuwa yeye mwenyewe amekubali kuwa waliochochea moto wa fitina hiyo ni mazanadiki. Miongoni mwa watu hao ni myahudi Abu Shaakir ad-Diyswaaniy aliyemtaja katika kitabu chake na kwamba alivaa vazi la Kiiislamu ili kuzua fitina. Hivi sasa nataka kumuuliza al-Khaliyliy swali lifuatalo: Je, myahudi huyu Abu Shaakir ad-Diyswaaniy alisema kuhusu Qur-aan ya kwamba ni maneno ya Allaah aliyozungumza kwayo na akayasikia Jibriyl kutoka Kwake na akateremka nayo kwa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambapo akawa amezua fitina kwa maneno haya au kinyume chake alisema kuwa Qur-aan imeumbwa kama alivyosema al-Ja´d bin Dirham ambaye mlolongo wa maneno yake unaenda mpaka kwa myahudi ambaye ni Labiyd bin al-A´swam? Maoni haya ndio yaliyochukuliwa na Mu´tazilah na kundi katika Ibaadhiyyah waliokuja nyuma ambapo wakazua fitina na wakaufarikisha Ummah. al-Khaliyliy hawezi kusema kuwa alisema sehemu ya kwanza ya sentesi kwa kuwa uhalisia wa mambo unashuhudia kinyume na hivyo.

[1] al-Kaamil (07/75).

[2] 36:82

  • Mhusika: ´Allaamah ´Aliy bin Naaswir al-Faqiyhiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ar-Radd al-Qawiym, uk. 190-191
  • Imechapishwa: 14/01/2017