Baadhi ya sifa za wanawake wa Peponi

Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

وَبَشِّرِ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ أَنَّ لَهُمْ جَنَّاتٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ ۖ كُلَّمَا رُزِقُوا مِنْهَا مِن ثَمَرَةٍ رِّزْقًا ۙ قَالُوا هَـٰذَا الَّذِي رُزِقْنَا مِن قَبْلُ ۖ وَأُتُوا بِهِ مُتَشَابِهًا ۖ وَلَهُمْ فِيهَا أَزْوَاجٌ مُّطَهَّرَةٌ ۖ وَهُمْ فِيهَا خَالِدُونَ

“Wape bishara njema wale walioamini na wakatenda mema kwamba watapata mabustani yapitayo chini yake mito, kila watakaporuzukiwa humo katika matunda kuwa ni riziki husema “Haya ndiyo yale tuliyoruzukiwa kabla” na wataletewa hali ya kuwa yanafanana; na watapata humo wake waliotwahirika nao humo ni wenye kudumu milele.”[1]

Kila watakaporuzukiwa humo katika matunda kuwa ni riziki husema “Haya ndiyo yale tuliyoruzukiwa kabla” bi maana katika aina na sifa yake. Yote ni yenye kufanana katika uzuri na utamu. Hakuna tunda ambalo ni maalum na hakuna wakati fulani ambapo wanaacha kuburudika na ladha. Wakati wote ni wenye kuburudika kwa kuyala. Maneno Yake:

وَأُتُوا بِهِ مُتَشَابِهًا

“… na wataletewa hali ya kuwa yanafanana… ”

Ni yenye kufanana majina lakini yenye ladha tofauti. Kuna maoni mengine yanasema kuwa ni yenye kufanana katika rangi na ni yenye kutofautiana katika jina. Kuna maoni mengine yanasema kwamba yenyewe kwa yenyewe ni yenye kufanana katika uzuri, utamu na uburudikaji. Pengine haya ya mwisho ndio maoni sahihi.

Kisha baada ya kutaja makazi yao, nguvu zao katika kula, kunywa na matunda yao ndipo akataja wake zao. Akawasifu kwa sifa kamilifu, fupi na ya wazi zaidi kwa kusema:

وَلَهُمْ فِيهَا أَزْوَاجٌ مُطَهَّرَةٌ

“… na watapata humo wake waliotwahirika… “

Hakusema kuwa wametwahirika kutokamana na dosari fulani ili wasifu huo ukusanye aina zote za utwahirifu. Wametwahirika kitabia, kimaumbile, kiulimi na macho. Tabia zao ni kwamba wao ni wenye mahaba wanaopendwa na waume zao kwa sababu ya tabia zao nzuri, wenye kutekeleza haki za mume na pia adabu za kimaneno na za kimatendo.

Pia wanawake hao wametwahirishwa maumbile yao kutokamana na hedhi, nifasi, manii, mkojo, kinyesi, makamasi, mate, harufu mbaya na wamesafishwa kimaumbile pia kwa ukamilifu wa urembo. Hawana kasoro yoyote. Bali ni wabora na warembo. Wamesafishwa ndimi zao na viungo vyao. Watakuwa ni wanawake wenye staha wanaoinamisha macho na wenye macho mapana mazuri ya kuvutia kwa waume zao na pia wenye staha kwenye ndimi zao kutokamana na maneno yote mabaya.

[1] 02:25

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdur-Rahmaan bin Naaswir as-Sa´diy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Taysiyr-ul-Kariym, uk. 36
  • Imechapishwa: 29/05/2020