az-Zubayr bin al-A´waam bin Khuwaylid bin Asad bin ´Abdil-´Uzzaa bin Qusayy bin Kilaab bin Murrah bin Ka´b bin Lu’ayy bin Ghaalib.

Alikuwa ni mfuasi wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na ami yake upande wa shangazi yake Swafiyyah bin ´Abdil-Muttwalib. Ni mmoja katika wale watu maarufu walioahidiwa Pepo. Ni mmoja katika wale sita wa mashauriano. Yeye ndiye  wa mwanzo kuchukua upanga wake katika njia ya Allaah. Abu ´Abdillaah – Allaah amridhie. Aliingia ndani ya Uislamu akiwa bado ni chipukizi wa miaka kumi na sita.

´Urwah amesema:

“Wakati az-Zubayr alipoingia katika Uislamu alikuwa na miaka nane. Shaytwaan akaeneza uvumi kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amefungwa kaskazini mwa Makkah. Kipindi hicho az-Zubayr alikuwa na miaka kumi na mbili. Wakati aliposikia hivo, akachukua upanga wake na kutoka. Watu waliokuwa wanamuona wanashangaa na kusema: “Mtoto yuko na upanga?” Tahamaki akakutana na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Akasema: “Una nini, ee az-Zubayr?” Akamweleza aliyosikia na kusema: “Nimekuja kumpiga upanga ambaye amekufunga.”

Imepokelewa kwamba az-Zubayr alikuwa mrefu. Anapopanda kipando cha mnyama, basi miguu yake inafika ardhini. Ndevu zake zilikuwa khafifu na hakuwa na mabega makubwa.

Amepokea Hadiyth chache.

Baadhi ya waliohadithia kutoka kwake ni wanawe ´Abdullaah, Musw´ab, ´Urwah na Ja´far, Maalik bin Aws bin al-Hadathaan, al-Ahnaf bin Qays, ´Abdullaah bin ´Aamir bin Kurayz, Muslim bin Jundub, Abu Haakim ambaye alikuwa huri wake, na wengineo.

´Abdullaah bin az-Zubayr amesema:

“Nilisema kumwambia baba yangu: “Ni kwa nini husimulii kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kama anavofanya fulani na fulani?” Akasema: “Sikutengana naye tangu nilipokuwa muislamu, lakini nimemsikia akisema:

“Yule mwenye kunisemea uongo kwa makusudi, basi ajiandalie makazi yake Motoni.”

Muusa bin Twalhah amesema:

“´Aliy, az-Zubayr, Twalhah na Sa´d walizaliwa mwaka mmoja.”

al-Madaa-iniy amesema:

“Twalhah, az-Zubayr na ´Aliy walikuwa rika moja.”

Ibn Ishaaq amesema:

“Kutokana na yale niliyosikia ni kwamba az-Zubayr, ´Uthmaan, Twalhah, ´Abdur-Rahmaan na Sa´d waliingia katika Uislamu kupitia mikononi mwa Abu Bakr.”

Musw´ab bin az-Zubayr amesema:

“az-Zubayr alipigana vita bega kwa bega akiwa pamoja na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akiwa na miaka kumi na saba.”

Muusa bin ´Uqbah na Ishaaq wamenukuu kwamba alihajiri kwenda Uhabeshi. Lakini hakukaa huko kwa muda mrefu.

´Aaishah amesema:

“Ee mpwa wangu! Babu zako wawili – yaani Abu Bakr na az-Zubayr – ni miongoni mwa wale ambao Allaah amesema juu yake:

الَّذِينَ اسْتَجَابُوا لِلَّـهِ وَالرَّسُولِ مِن بَعْدِ مَا أَصَابَهُمُ الْقَرْحُ

“Wale waliomuitikia Allaah na Mtume baada ya kuwapata majeraha.”[1]

Jaabir amesema:

“ Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisema siku ya Khandaq: “Ni nani ambaye atatuletea khabari za Banuu Quraydhwah?” az-Zubayr akasema: “Mimi.” Akaketi juu ya farasi na kitambo kidogo akaja na khabari zao. Kisha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema mara ya pili vivyo hivyo na az-Zubayr akasema tena: “Mimi.” Halafu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema mara ya tatu vivyo hivyo na az-Zubayr akasema tena: “Mimi.” Ndipo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Kila Mtume ana wafuasi na mfuasi wangu mimi ni az-Zubayr.”

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“az-Zubayr ni binamu yangu na mfuasi wa Ummah wangu.”

ath-Thawriy amesema:

“Hawa watatu ndio wanusura wa Maswahabah; Hamzah, ´Aliy na az-Zubayr.”

Katika “as-Swahiyh” ya Muslim Abu Hurayrah amesimulia kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa katika Hiraa´ pamoja na Abu Bakr, ´Umar, ´Uthmaan, ´Aliy, Twalhah na az-Zubayr. Tahamaki mlima ukaanza kutikisika. Ndipo Mtume wa Allaah  (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema:

“Tulizana! Hakuna aliye juu yako isipokuwa Nabii, mkweli au shahidi.”[2]

Ibn Abiy Laylaa amesema:

“Siku ya ngamia az-Zubayr aliondoka akamwacha ´Aliy. Akakutana na mwanae ´Abdullaah ambaye akamwambia: “Mwoga! Mwoga!” az-Zubayr akasema: “Watu wamejua kuwa mimi si mwoga. Lakini ´Aliy amenieleza kitu alichokisikia kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hivyo nikaapa kwamba sintopigana naye vita.”

Qataadah amesema:

“Nilikuwa pamoja na az-Zubayr siku ya ngamia wakati Ibn Jurmuuz alipomuua. Akazikwa kwenye bonde la wanyama wakali. ´Aliy yeye na Maswahabah zake wakamshukia na kulia kwa ajili yake.”[3]

Abu Nadhwrah amesema:

“Kichwa cha az-Zubayr kilitumwa kwa ´Aliy. Ndipo ´Aliy akasema: “Jiandalie makazi yako Motoni! Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amenihadithia kwamba mwenye kumuua az-Zubayr atakuwa Motoni.”[4]

ash-Sha´biy amesema:

“Nilikutana na Maswahabah zaidi ya mia tano. Wote walikuwa wakisema: “´Aliy, ´Uthmaan, Twalhah na az-Zubayr wako Peponi.”

Kwa sababu ni miongoni mwa wale kumi walioshuhudiwa Pepo, walishiriki vita vya Badr, walikuweko chini ya mti na kula kiapo cha usikivu, ni miongoni mwa wale waislamu wa mwanzo kabisa, ambao Allaah amesema kuwa Amewaridhia nao wamemridhia, waliuliwa na wakaruzukiwa kufa shahidi. Tunawapenda na tunawachukia wale nne waliowaua.”

al-Bukhaariy amesema:

“Aliuliwa Rajab mwaka wa 36.”

al-Qahdhwamiy amesema:

“Alikuwa amemuoa Asmaa’ bint Abiy Bakr, ´Aatikah (Dadake na Sa´iyd bin Zayd), Umm Khaalid bint Khaalid bin Sa´iyd na Umm Musw´ab al-Kalbiyyah.”

Ibn-uz-Zubayr amesema:

“Wakati aliposimama az-Zubayr siku ya ngamia, aliniita. Nikasimama pambizoni mwake. Akanambia: “Ee mwanangu kipenzi! Hakika hii leo hatouliwa isipokuwa dhalimu au mdhulumiwa. Mimi sijioni vyengine isipokuwa kwamba nitauliwa hali ya kuwa ni mwenye kudhulumiwa. Wasiwasi wangu mkubwa ni deni langu. Unaona deni letu lituachie kitu chochote katika mali yetu? Ee mwangu kipenzi! Uza mali yetu na ulipe deni langu.”

Ibn-uz-Zubayr amesema:

“Baba yangu aliniamrisha kulipa deni lake. Akasema: “Ee mwanangu kipenzi! Ukishindwa kulipa lote, basi mtake msaada mlinzi wangu.” Naapa kwa Allaah kwamba sikujua anachomaanisha mpaka niliposema: “Ee babangu kipenzi! Ni nani mlinzi wako?” Akasema: “Allaah (´Azza wa Jall).” Naapa kwa Allaah hakuna wakati wowote nilipata uzito wa kulipa deni lake isipokuwa nilisema: “Ee mlinzi wa az-Zubayr, mlipie deni lake.” Hivyo linalipwa.”

[1] 3:172

[2] Muslim (2417) na at-Tirmidhiy (3698).

[3] at-Twabaqaat (3/111) ya Ibn Sa´d kwa cheni ya wapokezi ambayo wanamme wake ni waaminifu.

[4] at-Twayaalisiy (2/145) na Ibn Sa´d (3/1/73). Swahiyh kwa mujibu wa al-Haakim na adh-Dhahabiy akaafikiana naye.

  • Mhusika: Imaam Shams-ud-Diyn Muhammad bin Ahmad adh-Dhahabiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Siyar A´laam-in-Nubalaa’ (1/41-67)
  • Imechapishwa: 09/03/2021