Anaitwa Asmaa’ bint Abiy Bakr ´Abdillaah bin Abiy Quhaafah ´Uthmaan. Umm ´Abdillaah al-Qurashiyyah at-Tamiymiyyah al-Makkiyyah kisha al-Madaniyyah.

Yeye ndiye mama wa khaliyfah ´Abdullaah bin az-Zubayr na dada yake na mama wa waumini ´Aaishah na mwanamke wa mwisho katika Muhajiruun aliyefariki.

Alipokea Hadiyth nyingi na akaishi muda mrefu. Alikuwa akijulikana kama “Mwanamke mwenye kanda mbili”.

Mama yake alikuwa akiitwa Qutaylah bint ´Abdil-´Uzzaa al-´Aamiriyyah.

Miongoni mwa waliopokea kutoka kwake ni wanawe wawili ´Abdullaah na ´Urwah, mjukuu wake ´Abdullaah bin ´Urwah, Ibn ´Abbaas na Abu Waaqid al-Laythiy.

Alikuwa ni mkubwa kwa ´Aaishah kwa miaka kumi na kitu.

Alihajiri akiwa na ujauzito wa ´Abdullaah.

Imesemekana kwamba hakutokwa na jino hata moja.

Alishuhudia vita vya Yarmuuk pamoja na mume wake az-Zubayr.

Yeye, baba yake, babu yake na mwanae az-Zubayr wote walikuwa Maswahabah.

Asmaa´ bint Abiy Bakr ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Nitasimama karibu na Hodhi nikitazama ni nani anayenijia katika nyinyi.”[1]

Muslim al-Qurriy amesema:

“Tuliingia nyumbani kwa mama yake na Ibn-uz-Zubayr. Alikuwa ni mnene na mwanamke kipofu. Tukamuuliza kuhusu hajj ya Tamattu´. Akasema: ”Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameiruhusu.”[2]

´Abdur-Rahmaan bin Abiyz-Zinaad amesema:

“Asmaa´ alikuwa mkubwa kwa ´Aaishah kwa miaka kumi.”

Asmaa´ amesema:

“Wakati Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipotaka kuhajiri, nilimwandalia mkoba wa chakula nyumbani kwa baba yangu. Hata hivyo sikupata kwa ajili ya mkoba wake wa chakula wala chombo chake cha maji kitu cha kufungia nacho. Nikamwambia baba yangu: “Sipati kitu isipokuwa mkanda wangu.”Ndipo akasema:”Ugawanye mara mbili na ufunge kwao.”

Ndio maana akaitwa “Mwanamke wa kanda mbili”.

Ibn Abiy Mulaykah amesema:

”Asmaa´ akishikwa na maumivu ya kichwa. Akiweka mkono wake juu ya kichwa chake na kusema: ”Ni kutokana na dhambi zangu. Lakini anayosamehe Allaah ndio mengi zaidi.”[3]

´Urwah amepokea kutoka kwa Asmaa´ ambaye amesema:

”az-Zubayr alinioa na hakuwa akimiliki kitu isipokuwa farasi. Nilikuwa nikimpa chakula na maji na nikishona ndoo yake kubwa na kutengeneza unga. Sikuwa mzuri wa kutengeneza wa kutengeneza mkate, hivyo nilikuwa na wasichana wa ki-Answaar wanaonifanyia na walikuwa wazuri na wanawake waaminifu. Nilikuwa nikibeba juu ya kichwa changu kokwa za tende kutoka katika ardhi ya az-Zubayr ambayo alipewa na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) iliokuwa theluthi mbili za Farsakh kutokea nyumbani kwangu. Siku moja nilikuwa na kokwa za tende kichwani mwangu ambapo ghafla nikakutana na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akiwa pamoja na baadhi ya Maswahabah zake. Akaniita na kusema ”Ikh, Ikh”[4] ili anibebe nyuma yake. Nikaona haya na nikakumbuka wivu wako. Ndipo akasema: ”Naapa kwa Allaah kwamba kubeba kokwa za tende kulikuwa ni kukubwa zaidi kwangu kuliko kupanda pamoja naye.”Baada ya hapo Abu Bakr akanitumia mfanya kazi wa kike kuja kumshughulikia huyo farasi na ilikuwa ni kana kwamba ameniacha huru.”[5]

Ibn-uz-Zubayr amesema:

“Aayah hii imeteremka juu ya Asmaa´. Mama yake alikuwa anaitwa Qutaylah ambaye siku moja alikuja na zawadi. Amsaa´ hakuzikubali mpaka alipomuuliza kwanza Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Ndipo kukateremshwa:

لَّا يَنْهَاكُمُ اللَّـهُ عَنِ الَّذِينَ لَمْ يُقَاتِلُوكُمْ فِي الدِّينِ وَلَمْ يُخْرِجُوكُم مِّن دِيَارِكُمْ أَن تَبَرُّوهُمْ وَتُقْسِطُوا إِلَيْهِمْ ۚ إِنَّ اللَّـهَ يُحِبُّ الْمُقْسِطِينَ

”Allaah hakukatazeni kuwatendea wema wale wasiokupigeni vita katika dini na wala hawakukutoeni kutoka majumbani mwenu. Hakika Allaah anapenda watendao uadilifu.”[6]

Muhammad bin al-Munkadir amesema:

“Asmaa´ alikuwa mkarimu.”

Ibn-uz-Zubayr amesema:

“Sijawahi kumuona mtu ambaye alikuwa mwenye kutoa sana kama ´Aaishah na Asmaa´. Utoaji wao ulikuwa unatofautiana. ´Aaishah alikuwa akikusanya kitu baada ya kingine mpaka mwishoni anakitoa. Asmaa´ alikuwa hakusanyi kitu kwa ajili ya siku ya kesho asubuhi.”

Faatwimah bint al-Mundhir amesema:

“Asmaa´ alikuwa anashikwa na maradhi fulani na anawaacha huru watumwa wote.”[7]

Hishaam bin ´Urwah amesema:

“Katika wakati wa Sa´iyd bin al-´Aasw wezi walikuwa wengi al-Madiynah. Ndipo Asmaa´ akachukua kisu na akawa anakiweka chini ya kcihwa chake.”[8]

Aliishi kwa muda wa miaka 100.

Mama yake na Abul-Muhayyah amesema:

“Baada ya al-Hajjaaj kumuua Ibn-uz-Zubayr, aliingia kwa Asmaa´ na akamwambia: “Ee mama yangu kipenzi! Hakika kiongozi wa waumini ameniamrisha nikuage. Unahitajia chochote?” Asmaa´ akasema: “Mimi si mama yako. Mimi ni mama wa yule aliyesulubiwa. Hakuna ninachohitaji. Lakini napenda kukueleza kwamba nimemsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema: “Kutajitokeza katika Thaqiyf mwongo na mkandamizi. Kuhusu mwongo tumekwishauona – bi maana al-Mukhtaar. Na kuhusu mkadamizi ndiye wewe.” Ndipo akamwambia Asmaa´: “Mkandamizi wa wanafiki.”

Ya´laa at-Taymiy amesema:

“Niliingia Makkah siku tatu baada ya kuuliwa Ibn-uz-Zubayr na alikuwa amesulubiwa. Akaja mama yake ambaye alikuwa kikongwe, mrefu na mwanamke kipofu akamwambia al-Hajjaaj: “Je, hivi sumefika wakati wa waliopanda washuke?” Akasema: “Mnafiki?” Asmaa´ akasema: “Naapa kwa Allaah kwamba hakuwa mnafiki. Alikuwa ni mwenye kuswali na kufunga kwa wingi. Alikuwa ni mtenda wema.” Akasema: “Ondoka zako, kikongwe! Umekwishachanganyikiwa!” Asmaa´ akasema: “Naapa kwa Allaah sijachanganyikiwa tangu nimsikie Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema: ““Kutajitokeza katika Thaqiyf mwongo na mkandamizi… “

Kulisemwa kuambiwa Ibn ´Umar baada ya kusulubiwa kwa Ibn-uz-Zubayr:

“Asmaa´ yuko msikitini.” Akamwendea na kumwambia: “Miili hii si chochote. Hakika si vyenginevyo roho ziko kwa Allaah. Kwa hivyo basi, mche Allaah na uwe na subira.”Asmaa´ akasema: “Kipi kinachonizuia? Kichwa cha Yahyaa bin Zakariyyaa alipewa zawadi malaya mmoja miongoni mwa wamalaya wa wana wa israaiyl.”

Ibn Abiy Mulaykah amesema:

“Baada ya kuuliwa kwa Ibn-uz-Zubayr, nilimtembelea Asmaa´. Akasema: “Nimepata khabari kwamba bwana huyo amemsulubu ´Abdullaah. Ee Allaah! Usinifishe mpaka nimwandae na kumvika sanda.” Mwili wake ukaletwa kwake ambapo akamwandaa na kumvika sanda kwa mikono yake baada ya kuondokwa na macho yake.”

Ibn Abiy Mulaykah amesema:

“Alimswalia swalah ya jeneza na hakukupita wiki isipokuwa akafariki.”

Ibn Sa´d amesema:

“Alifariki baada ya mwanae kwa nyusiku kadhaa.”

Yeye ndiye alikuwa wa mwisho katika wale wahajiri wa kutoka Makkah.

Amepokea Hadiyth khamsini na nane. al-Bukhaariy na Muslim wote kwa pamoja wamepokea kumi na tatu. al-Bukhaariy mwenyewe amepokea tano na Muslim nne.

[1] Muslim (2293).

[2] Ahmad (6/348).

[3] Ibn Sa´d (8/251).

[4] Ibn Hajar amesema:

”Ni maneno anayoambiwa ngamia ili apige magoti.” (Fath-ul-Baariy (9/389))

[5] al-Bukhaariy (5224).

[6] 60:8

[7] Ibn Sa´d (8/251).

[8] Ibn Sa´d (8/251).

  • Mhusika: Imaam Shams-ud-Diyn Muhammad bin Ahmad adh-Dhahabiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Siyar A´laam-in-Nubalaa’ (2/287-296)
  • Imechapishwa: 06/01/2021