ar-Raajhiy kuhusu taarifu ya Mtume na Nabii

Ni ipi tofauti kati ya Nabii na Mtume? Kuna wanachuoni waliosema kuwa tofauti ya Nabii na Mtume ni kuwa wote wawili wanateremshiwa Wahy, lakini Mtume anateremshiwa Wahy na anaamrishwa kuufikisha. Ama Nabii anateremshiwa Wahy na haamrishwi kuufikisha. Akiteremshiwa Wahy na akaamrishwa kuufikisha, huyo ni Mtume. Akiteremshiwa Wahy na asiamrishwe kuufikisha, huyo ni Nabii. Lakini hata hivyo kauli hii haina nguvu.

Kauli sahihi ni kwamba Mtume ni yule ambaye anatumwa kwa umati wa kikafiri ambapo baadhi wakamuamini na baadhi wengine wakamkanusha. Kwa mfano Nuuh (´alayhis-Salaam) alitumwa kwa makafiri baadhi wakamuamini na wengine wakamkanusha. Kadhalika Huud, Swaalih, Shu´ayb, Ibraahiym, Muusa, ´Iysaa na Mtume wetu Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Kuhusiana na Nabii ni yule anayetumwa kwa watu ambao ni waumini na wanawalazimisha kutendea kazi Shari´ah iliokutwa hapo kabla. Kwa mfano Aadam (´alayhis-Salaam) ni Nabii ambaye alitumwa kwa watoto wake na zama zake hakukutokea shirki. Hali kadhalika Shiyt.

Nuuh (´alayhis-Salaam) ndiye alikuwa Mtume wa kwanza aliyetumwa katika ardhi baada ya kutokea shirki na akawa ametumwa kwa watoto wake na wengine.

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajhiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Hidaayah ar-Rabbaaniyyah fiy Sharh al-´Aqiydah at-Twahaawiyyah (01/128)
  • Imechapishwa: 31/05/2020