Swali: Ni ipi hukumu ya ambaye anawaswalisha watu akiwa na jeraha?

Jibu: Ikiwa jeraha juu yake limefungwa bendeji basi afute juu yake wakati wa kutawadha na wakati wa kuoga josho la janaba. Kunamtosha kufanya hivo. Swalah yake ni sahihi. Ni mamoja ni imamu, maamuma au anayeswali peke yake. Asipokuwa na jeraha basi afanye Tayammum juu yake baada ya kuosha viungo vyake vilivyo salama. Kunamtosha kufanya hivo na swalah yake ni sahihi. Allaah (Ta´ala) amesema:

فَاتَّقُوا اللَّـهَ مَا اسْتَطَعْتُمْ

”Mcheni Allaah muwezavyo.”[1]

Isitoshe Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na waislamu wengine waliopatwa na majeraha siku ya Uhud waliswali na majeraha yao. Aidha Abu Daawuud (Rahimahu Allaah) kupitia kwa Jaabir (Radhiya Allaahu ´anh) kwamba kuna bwana mmoja alipatwa na jeraha na baadhi ya marafiki zake wakamfutu kwamba anatakiwa kuoga ambapo akafanya hivo na akafariki. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema:

“Wamemuua? Allaah nao awaue. Kwa nini wasiulize kama hawajui? Hakika si venginevyo dawa ya ujinga ni kuuliza.”

Kisha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema:

“Kulikuwa kunamtosha kufunga juu ya jeraha lake kitambaa ambapo akapangusa juu yake na akaosha mwili wake uliobaki.”

[1] 64:16

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (10/119 )
  • Imechapishwa: 18/08/2021