Anawasafirisha waalimu wakike na kuwapeleka kijijini

Swali: Kuna ndugu mmoja alikuwa anahitaji pesa na hivyo akaanza kuwasafirisha waalima wakike kutoka mji fulani kwenda kwenye kijiji kingine ambapo kilikuwa umbali wa takriban 150 km. Hakupata Mahram wao isipokuwa mke wake. Je, kitendo hichi kinajuzu au ni haramu pamoja na kuzingatia ya kwamba mtu huyu hajui hukumu?

Jibu: Maneno yake aliposema kuwa hakupata Mahram wao isipokuwa mke wake ni ibara isiyokuwa sahihi. Kwa nini tunasema hivo? Mke sio Mahram. Mke ni mwanamke ambaye yeye mwenyewe anahitajia Mahram. Lakini iwapo angelisema kuwa hawi faragha na mwanamke yeyote katika wanawake hawa, kwa msemo mwingine ni kwamba anawapeleka kwa pamoja na anawarudisha kwa pamoja na hawi faragha na yeyote kwa kuwa yuko pamoja nao mke wake, matamshi yangelikuwa ya sawa.

Mimi naona kuwa midhali yule msafirishaji ni mwaminifu katika dini yake na hakai faragha na mwanamke yeyote na wanarudi hiyohiyo siku ya kwamba hakuna neno kufanya hivo. Kwa kuwa hii haizingatiwi kuwa ni safari. Hakuna mtu awezaye kusema kuwa wamesafiri kwenda kusomesha hata kama itakuwa 100 km au zaidi ya hapo. Umbali huu hauzingatiwi kuwa ni safari kwa kuwa wanarudi hiyohiyo siku kabla mjini kwao huku usiku haujaingia.  Kilicho muhimu ni kwamba hii sio safari na hakuna makatazo. Kilichokatazwa ni kukaa faragha. Hakuna neno maadamu hakuna kukaa nao faragha. Lakini ni wajibu kwa wale wasimamizi wa wanawake kumtupia jicho kwelikweli yule msafirishaji na wamtazame kama ni mwaminifu au si mwaninifu.

  • Mhusika: http://binothaimeen.net/content/900
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Liqaa’ ash-Shahriy (40) http://binothaimeen.net/content/902
  • Imechapishwa: 22/08/2018