Anataka kuacha masomo kwa kutoiamini nia yake

Swali: Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mwenye kujifunza elimu katika yale yanayokusudiwa uso wa Allaah na hakuna anachotaka isipokuwa jambo la kidunia, basi hatoipata harufu ya Pepo.”

au maneno mfano wa hayo. Mimi ni mwanafunzi katika chuo kikuu na tunasoma elimu za Kishari´ah. Mara nyingi najiambia mwenyewe kwamba nitaacha masomo kwa sababu ya Hadiyth hii kwa sababu sio mwenye kumtakasia Allaah nia katika kusoma kwangu. Bali naona kuwa nasoma kwa ajili ya kupata shahada na pesa. Mimi ni mwenye wasiwasi. Nakuomba nasaha na Allaah akujaze kheri.

Jibu: Allaah amjaze kheri kwa swali hili ambalo wakati mwingine huenda likawatatiza wanafunzi wengi. Ni jambo linalotambulika kwamba wale wanaoingia katika chuo kikuu wanachotaka ni kufikia cheo ambacho wataweza kuwanufaisha watu. Hakuna njia ya kufikia jambo hilo isipokuwa kwa shahada. Akisoma katika chuo kikuu ili aweze kufikia shahada ili baada ya hapo awe msomeshaji, mwalimu, hakimu, mwalimu, mwelekezaji na mtoa mawaidha, basi hiyo ni kheri. Hii ni nia njema na haina kasoro. Kwa sababu ni jambo linalotambulika hii leo lau atakuja mtu ambaye ni msomi lakini hana shahada na akafanya maombi ili awe profesa chuo kikuu atakubaliwa? Hatokubaliwa kwa sababu hana shahada.

Kwa ajili hiyo tunawaambia ndugu zetu kwamba nia zao ni njema ikiwa mnataka kwa shahada hizo kufikia cheo muweze kuwanufaisha waja wa Allaah. Ni nia njema na haina neno. Ni watu wangapi waliosoma katika chuo kikuu ambapo Allaah akanufaisha kupitia wao! Wamekuwa ni mahakimu, walinganizi, waelekezaji na waalimu ambapo Allaah akanufaisha kupitia wao.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Liqaa´ ash-Shahriy (72) http://binothaimeen.net/content/1659
  • Imechapishwa: 09/04/2020