Anashindwa kutimiza nadhiri yake ya kuswali kila siku Rawaatib


Swali: Kuna mtu aliona kuwa anapuuzia Sunan za Rawaatib. Akataka kuweka maazimio ya kuzitekeleza kikamilifu. Matokeo yake akaweka nadhiri kwa Allaah asiache Sunnah yoyote ile ya Raatibah ambapo akajilazimisha mwenyewe kwa kitu ambacho Allaah hakumlazimisha nacho. Hivi sasa anaona kuwa anafanya upungufu. Ni upi umfumbuzi wa mtu huyu ambaye amejisababishia kuikalifisha nafsi yake kitu asichokiweza?

Jibu: Hiki kitu anakiweza. Rawaatib kila mtu anaziweza. Lakini akisafiri zinaanguka kwake. Kwa sababu aliweka nadhiri ya swalah za Rawaatib. Rawaatib safarini zinaanguka isipokuwa Raatibah ya Fajr. Zingatieni maneno yangu ya Rawaatib katika Nawaafil. Nawaafil safarini hazianguki. Mwenye kusema kwamba imependekezwa safarini kwa msafiri kuacha kuswali Sunnah amekosea. Rawaatib zinazoanguka safarini ni tatu; za Dhuhr, za Maghrib na za ´Ishaa. Hizi tunakwambia kwamba zinaanguka pale unaposafiri. Lakini, je, zinaanguka kwake ikiwa kama atadhamiria kusafiri kwa ajili ya kuziangusha Rawaatib hizi tatu? Hapana. Hivi ni vitimbi visivyofaa kitu. Kwa ajili hii wanachuoni wamesema kuwa msafiri swawm haimlazimu. Lakini ikiwa atasafiri ili asiweze kufunga, katika hali hiyo safari kwake inakuwa haramu na kuacha kufunga pia kunakuwa haramu.

Tunachotaka kusema kumwambia ndugu ni kwamba hili ni jambo linalowezekana.  Kusema kwamba ni jambo haliwezi si kweli. Kila mmoja anaweza kuswali Rak´ah mbili kabla ya Dhuhr na Rak´ah mbili baada yake, Rak´ah mbili baada ya Maghrib na Rak´ah mbili baada ya ´Ishaa na Rak´ah mbili baada ya Fajr. Hakuna uzito wowote. Amtake msaada Allaah, atekeleze nadhiri yake na kutowashauri wengine juu ya jambo la kuweka nadhiri.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Liqaa' ash-Shahriy (52) http://binothaimeen.net/content/1175
  • Imechapishwa: 06/07/2019