Anakuwa mchangamfu wa ´íbaadah anapokuwa na marafiki peke yake

Swali: Pindi ninapokuwa kambini au safarini na ndugu zangu kwa ajili ya Allaah nahifadhi swalah na khaswa swalah ya Fajr na vivyo hivyo swalah zilizopendekezwa. Lakini ninaporudi kambini nakuwa mvivu wa swalah ya Fajr na mara nyingi napitiwa na usingizi kuiswali na vivyo hivyo swalah zilizopendekezwa. Je, kitendo hichi ni katika unafiki?

Jibu: Kitendo hichi ni kama mlivosikia ya kwamba ni katika kuzembea. Huku ni kuzembea. Huyu ni miongoni mwa sampuli ya pili ambayo ni kuzembea. Ni lazima uwe namna hiyo daima; ni mamoja ukiwa kambini na marafiki zako. Bali daima unatakiwa kuwa mchangamfu na shauku ya kutekeleza mambo ya wajibu; kuswali kwa mkusanyiko kukiwemo swalah ya Fajr na swalah za Rawaatib. Hivi ndivo anavokuwa muumini juu ya mambo ya wajibu. Imesuniwa kuwa na uchangamfu katika mambo ya wajibu na vivyo hivyo mambo yaliyopendekezwa.

Kuchukulia wepesi swalah ya Fajr ni miongoni mwa sifa za wanafiki. Kadhakika kuchukulia wepesi swalah nyinginezo za mkusanyiko ni miongoni mwa sifa za wanafiki:

إِنَّ الْمُنَافِقِينَ يُخَادِعُونَ اللَّـهَ وَهُوَ خَادِعُهُمْ وَإِذَا قَامُوا إِلَى الصَّلَاةِ قَامُوا كُسَالَىٰ

“Hakika wanafiki wanafikiri wanamhadaa Allaah na hali Yeye ndiye Mwenye kuwahadaa na wanaposimama kuswali basi husimama kwa uvivu.” (04:142)

Ni vipi unaridhia nafsi yako kujifananisha na maadui wa Allaah? Haikupasi kuridhia kujifananisha na maadui wa Allaah na wala haijuzu kwako. Bali ni lazima kuharakia kuswali Fajr pamoja na wengine kama zilivyo swalah nyinginezo. Ukiwa huna mwenye kukuamsha basi unatakiwa kuweka alamu ikusaidie na umwombe Mola Wako akusaidie na ulale mapema. Usichelewe kulala na wala usikeshe. Ukikesha hutosikia alamu na wala hutoamka baada ya kuamshwa. Lakini ukilala mapema kutakusaidia kuamka. Mche Allaah. Tunalazimika kumcha Allaah juu ya jambo hili na tusichukulii wepesi na tukakesha kwenye video, TV au mambo mengine. Inapofika Fajr mtu anakuwa kama maiti na hawezi kuamka. Haya ni maovu makubwa na ni kujifananisha na maadui wa Allaah wanafiki. Tahadhari.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/4081/ما-حكم-من-ينشط-للعبادة-مع-الرفقة-فقط
  • Imechapishwa: 07/06/2022