Anafupisha kanzu zake lakini anaburuta mavazi mengine


Swali: Baadhi ya watu wanafupisha kanzu zao mpaka juu kidogo ya fundo mbili za mguu lakini suruwali zao zinabaki kuwa refu. Ni ipi hukumu ya hilo?

Jibu: Nguo inayovuka kongo mbili za mguu ni haramu. Ni mamoja mtu amefanya hivo katika kanzu, kikoi, suruwali au juba. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Kile chenye kuvuka chini ya macho mawili ya mguu basi kiko Motoni.”

Ameipokea al-Bukhaariy.

“Watu aina tatu Allaah hatowatakasa siku ya Qiyaamah, hatowatazama, hatowatakasa na watakuwa na adhabu chungu; yule mwenye kubuta nguo yake, mwenye kusimanga juu ya kile alichokitoa na mwenye kuuza bidhaa yake kwa kiapo cha uongo.”

Ameipokea Muslim katika “as-Swahiyh” yake.

Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuwaambia baadhi ya Maswahabah zake:

“Tahadhari na nguo yenye kuvuka kongo mbili za mguu. Kwani hakika ni katika kiburi.”

Hadiyth hizi kwa kutajwa kwa kuenea na kutajwa kwa njia isiyofungamana zinajulisha kuwa nguo yenye kuvuka kongo mbili za mguu ni dhambi kubwa ingawa mtendaji atadai kuwa hakukusudia kufanya kiburi. Kuhusu ambaye atafanya hivo kwa kiburi basi dhambi yake ni kubwa zaidi. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yule mwenye kuburuta nguo yake kwa kiburi basi Allaah hatomtazama siku ya Qiyaamah.”

Aidha kwa kufanya hivo atakuwa amekusanya kati ya kuvaa nguo yenye kuvuka macho mawili ya mguu na pia kiburi. Tunamwomba Allaah afya kutokamana na hilo.

Kuhusu maneno yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kumwambia Abu Bakr pindi alipomwambia kwamba kikoi chake kinamshuka ingawa anapambana nacho ambapo (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamwambia:

“Hakika wewe si miongoni mwa wale wanaofanya hivo kwa kiburi.”

Hadiyth hii si dalili yenye kufahamisha kuwa inafaa kwa ambaye hatokusudia kiburi. Bali inajulisha kuwa yule ambaye nguo yake itamshuka pasi na kukusudia kufanya kiburi sambamba na hilo akawa anapambana nayo na kuiweka sawa basi hapati dhambi kwa hilo. Kuhusu yale yanayofanywa na baadhi ya watu ambapo wanateremsha nguo zao chini ya kongo mbili za mguu ni kitu kisichojuzu. Sunnah ni kanzu na mavazi mengine yafike mpaka katikati ya ugoko mpaka juu kidogo ya macho mawili ya mguu kwa ajili ya kutendea kazi Hadiyth zote.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (06/484)
  • Imechapishwa: 28/02/2021