Anachotakiwa kufanya muislamu anapoingia msikitini siku ya ijumaa


Swali: Ni lipi bora wakati ninapoingia msikitini siku ya ijumaa kuswali swalah za sunnah nyingi au kusoma Qur-aan?

Jibu: Yote mawili ni kheri. Kuswali swalah za sunnah nyingi ni jambo lililowekwa katika Shari´ah. Kwa sababu imekuja katika Hadiyth:

“Yule atakayeoga na akajitwaharisha kadri na atavyoweza kisha akajipaka mafuta au manukato halafu akaenda na asitenganishe kati ya watu wawili na akaswali yale aliyoandikiwa….”

Endapo ataswali kiasi anachoweza kisha akakaa na kuanza kusoma Qur-aan mpaka pale imamu atapokuja ndio jambo lililowekwa katika Shari´ah. Kuswali na kusoma yote ni mambo yamewekwa katika Shari´ah.

Ni jambo lenye kujulikana kwamba aina ya swalah ni bora zaidi. Kwa sababu ndani ya swalah tayari kuna kisomo. Iwapo ataswali na akakithirisha kuswali sunnah ndio bora zaidi. Mtu kukithirisha kuswali ni jambo limewekwa katika Shari´ah. Halafu baada ya hapo asome kile kitachomsahilikia katika Qur-aan. Kwa ajili hii imekuja katika Hadiyth iliyotangulia ya kwamba muislamu anatakiwa kuswali hadi pale imamu atapokuja. Hili ndio bora zaidi. Vilevile ikiwa ataswali na akaketi na kuanza kusoma Qur-aan pia ni kheri.

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaa Mutanawwi´ah (01) http://audio.islamweb.net/audio/index.php?page=FullContent&audioid=190884#219018
  • Imechapishwa: 29/12/2017