Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

 يَا أَيُّهَا النَّاسُ اعْبُدُوا رَبَّكُمُ الَّذِي خَلَقَكُمْ وَالَّذِينَ مِن قَبْلِكُمْ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ الَّذِي جَعَلَ لَكُمُ الْأَرْضَ فِرَاشًا وَالسَّمَاءَ بِنَاءً وَأَنزَلَ مِنَ السَّمَاءِ مَاءً فَأَخْرَجَ بِهِ مِنَ الثَّمَرَاتِ رِزْقًا لَّكُمْ ۖ فَلَا تَجْعَلُوا لِلَّـهِ أَندَادًا وَأَنتُمْ تَعْلَمُونَ

“Enyi watu! Mwabuduni Mola wenu ambaye amekuumbeni na wale wa kabla yenu mpate kumcha. Ambaye amewafanyieni ardhi kuwa ni tandiko na mbingu kuwa ni paa na akateremsha kutoka mbinguni maji, akawatolea kwayo matunda kuwa ni riziki zenu. Hivyo basi, msimfanyie Allaah waliolingana naye na hali ya kuwa nyinyi mnajua.”[1]

Hii ni amri inamuhusu kila mtu. Nayo ni ile ´ibaadah yenye kuenea kwa kutekeleza maamrisho ya Allaah, kuacha makatazo na kusadikisha maelezo Yake. Amewaamrisha (Ta´ala) kwa yale aliyowaumbia. Amesema (Ta´ala):

وَمَا خَلَقْتُ الْجِنَّ وَالْإِنْسَ إِلَّا لِيَعْبُدُونِ

“Sikuumba majini na watu isipokuwa waniabudu.”

Kisha akajengea hoja ya ulazima wa kumwabudu Yeye kwamba ndiye Mola wao ambaye amewalea kwa aina mbalimbali za neema, akawaumba baada ya kutokuweko kwao, akawaumba wale waliokuwa kabla yao, akawaneemesha kwa neema zilizojificha na zenye kuonekana. Amewafanyia ardhi kuwa kama tandiko ambapo wanatulizana juu yake na wakanufaika kwa kujenga, kulima, kupanda, kutoka sehemu moja kwenda nyingine na manufaa mengine mengi.

Pia ameifanya mbingu kuwa paa kwa ajili ya makazi yenu na akaziweka manufaa mbalimbali mambo ambayo ni katika ya lazima mnayoyahitajia kama mfano wa jua, mwezi na nyota.

 فَلَا تَجْعَلُوا لِلَّـهِ أَندَادًا وَأَنتُمْ تَعْلَمُونَ

“Hivyo basi, msimfanyie Allaah waliolingana naye na hali ya kuwa nyinyi mnajua.”

Washirika na wenza katika viumbe ambapo mkawaabudu kama mnavomwabudu Allaah ilihali wao ni kama nyinyi wameumbwa, wanaruzukiwa na wanaedeshwa. Hawamiliki kiasi cha punje mbinguni wala ardhini. Pia hawawanufaishi wala hawakudhuruni.

 وَأَنتُمْ تَعْلَمُونَ

“… na hali ya kuwa nyinyi mnajua.”

Mnajua kuwa Allaah hana mshirika wala mwenza si katika kuumba, kuruzuku, kuyaendesha mambo wala katika ´ibaadah. Ni vipi basi mtawaabudu waungu wengine pamoja na kwamba mnajua jambo hilo? Haya ni maajabu makubwa na upumbavu wa hali ya juu.

Aayah hii imekusanya kati ya kumwabudu Allaah pekee na kukataza kumwabudu mwengine asiyekuwa Yeye. Pia imebainisha hoja juu ya ulazima wa kumwabudu Allaah na ubatilifu wa kumwabudu mwengine asiyekuwa Yeye.

 لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ

“… mpate kumcha.”

Maana yake inaweza kuwa pale ambapo mtamwabudu Allaah pekee basi mtaogopa adhabu Yake. Kwa sababu mmefanya sababu ya kujikinga. Pia inaweza kuwa na maana kwamba pindi mtamwabudu Allaah basi mtakuwa miongoni mwa wachaji Allaah na wenye kusifika kwa uchaji. Maana zote mbili ni sahihi na ni zenye kulazimiana. Yule mwenye kutekeleza ´ibaadah kikamilifu basi atakuwa miongoni mwa wenye kumcha Allaah. Na yule ambaye atakuwa miongoni mwa wenye kumcha Allaah atasalimika kutokamana na adhabu ya Allaah.

[1] 02:21-22

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdur-Rahmaan bin Naaswir as-Sa´diy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Taysiyr-ul-Kariym, uk. 34
  • Imechapishwa: 08/05/2020