Amejiunga na imamu akidhani ni Fajr kumbe ni swalah ya kupatwa kwa jua

Swali: Kuna mtu alijiunga pamoja na imamu katika swalah ya kupatwa kwa jua ilihali hajui kama ni swalah ya kupatwa kwa jua. Akaswali na huku akidhani kuwa ni swalah ya Fajr. Afanye nini? Je, inamtosha swalah hii au arudi tena kuiswali?

Jibu: Ikiwa alifanya hivo kabla ya kuingia kwa alfajiri… kwa sababu kuna baadhi ya watu wanaona kupatwa kwa jua saa tatu kabla ambapo akaswali. Ikiwa aliswali kabla ya kuingia kwa alfajiri basi swalah yake si sahihi au kwa msemo mwingine haisihi kuwa faradhi. Katika hali hii anatakiwa kuendelea pamoja na imamu au aikate na ndio bora zaidi. Asitishe swalah ya Fajr aliyonuia na ajiunge pamoja na imamu kwa kunuia swalah ya kupatwa kwa jua.

Ama ikiwa hayo yametokea baada ya kuingia kwa alfajiri – kama ilivyo hali kwa wengi ambao wanaswali baada ya alfajiri kuingia – hapa akijiunga nao kwa nia ya Fajr kisha ikaja kumbainikia kuwa ni swalah ya kupatwa kwa jua, basi anatakiwa kunuia kujitenga na imamu na aikamilishe kwa kujengea ya kwamba ni swalah ya Fajr. Mfano wa hilo amejiunga naye akamkuta yuko anasoma, kisha akarukuu naye Rukuu´ ya kwanza, akainuka kutoka hapo na kuanza kusoma tena, hapa mswaliji huyu aliyekuja amechelewa atatambua kuwa hii ni swalah ya kupatwa kwa jua ambayo amenuia Fajr. Katika hali hii tunamwambia anuie kuswali peke yake na aikamilishe kujengea ya kwamba ni swalah ya Fajr kisha ajiunge na imamu katika yale yatayokuwa yamebaki katika swalah ya kupatwa kwa jua.

Tunafupisha kwa kusema ikiwa imamu ameanza swalah ya kupatwa kwa jua kabla ya kuingia alfajiri na huyu akawa amejiunga naye kwa kunuia swalah ya Fajr, basi akitambua kuwa ni swalah ya kupatwa kwa jua tunamwambia akate nia. Kwa sababu hawezi kuijenga swalah ya kupatwa kwa jua juu ya swalah ya faradhi. Anachotakiwa ni kukata nia papohapo na kujiunga upya pamoja na imamu. Ikiwa hayo ni baada ya kuingia alfajiri na akatambua kuwa ni swalah ya kupatwa kwa jua, basi anuie kuswali peke yake na wala asikate swalah. Bali anatakiwa kunuia kuswali peke yake na aikamilishe juu ya kwamba ni swalah ya Fajr kisha jiunge na imamu katika yale yatayokuwa yamebaki katika swalah ya kupatwa kwa jua.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Liqaa’ ash-Shahriy (38) http://binothaimeen.net/content/862
  • Imechapishwa: 27/06/2018