Swali: Hapo nyuma ilitokea mimi kulala katika moja ya hospitali na wakaingia pamoja nami watu wawili katika kile chumba ambacho nalala na nikabaki hapo kwa muda wa siku tatu. Katika kipindi hicho mimi nilikuwa naswali na wao hawaswali ingawa ni waislamu kutoka katika nchi yangu na sikuwaambia kitu. Je, nina dhambi kwa vile sikuwaamrisha kitu? Mambo yakiwa hivo ni nini kafara ya hilo?

Jibu: Ilikuwa ni wajibu kwako kuwanasihi na kuwakataza yale maovu makubwa waliyoyaendea ambayo ni kuacha swalah. Kufanya kwako hivo ni kutendea kazi maneno ya Allaah (Subhaanah):

وَلْتَكُن مِّنكُمْ أُمَّةٌ يَدْعُونَ إِلَى الْخَيْرِ وَيَأْمُرُونَ بِالْمَعْرُوفِ وَيَنْهَوْنَ عَنِ الْمُنكَرِ ۚوَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ

“Wawepo kutoka kwenu watu wanaolingania kheri na kuamrisha mema na unaokataza maovu. Hao ndio waliofaulu.”[1]

Na Aayah nyenginezo zenye maana kama hiyo. Vilevile kwa ajili ya kutendea kazi maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Yeyeote yule katika nyinyi atakayeona maovu, basi ayazuie kwa mkono wake. Asipoweza, afanye hivo kwa mdomo wake. Asipoweza, afanye hivo kwa moyo  wake – na hiyo ni imani dhaifu kabisa.”

Ameipokea Imaam Muslim katika “as-Swahiyh” yake.

Midhali hukufanya hivo basi ni lazima kwako kufanya tawbah ya kweli juu ya dhambi hiyo. Ukweli wa tawbah ni kujutia yale uliyofanya, kujinasua nayo na kuazimia kutorudi katika mfano wa kitu kama hicho hali ya kuwa ni mwenye kumtakasia nia Allaah, kumtukuza, kutarajia thawabu Zake na kuogopa adhabu Yake. Yule mwenye kutubia basi Allaah humsamehe. Amesema (Ta´ala):

وَإِنِّي لَغَفَّارٌ لِّمَن تَابَ وَآمَنَ وَعَمِلَ صَالِحًا ثُمَّ اهْتَدَىٰ

”Hakika Mimi ni Mwingi mno wa kusamehe kwa anayetubia na akaamini na akatenda mema kisha akaendelea kuongoka.”[2]

[1] 03:104

[2] 20:82

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (10/259)
  • Imechapishwa: 12/09/2021