Ameingia katika Takbiyr ya tatu katika swalah ya jeneza

Swali: Kuna mtu amepitwa na Takbiyr tatu katika swalah ya jeneza. Afanye nini na ni vipi atalipa Takbiyr hizi zilizompita?

Jibu: Akiiingia katika Takbiyr ya nne basi amuombee maiti. Kwa sababu hii ndio sehemu ya kumuombea maiti kwa upande wa imamu na wewe ni mwenye kumfuata imamu. Imamu akitoa Tasliym na wakalibakiza jeneza ili watimize swalah zao wale waliokuja wamechelewa basi watalipa yaliyowapita kwa sifa yake. Lakini ikiwa jeneza litanyanyuliwa – kama inavyofanywa mara nyingi – basi azifuatanishe Takbiyr kwa kusema “Allaahu Akbar”, “Allaahu Akbar” halafu atoe Tasliym. Akitaka vilevile anaweza kuleta Tasliym pamoja na imamu.

Sijajaaliwa kusoma Sunnah yoyote kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) juu ya haya masuala. Lakini hata hivyo haya ndio maneno ya wanachuoni. Wanasema iwapo ataweza kuyaleta yaliyompita kabla ya jeneza lile kunyanyuliwa basi afanye hivo. Vinginevyo ima atoe Tasliym pamoja na imamu au azifuatanishe Takbiyr kisha atoe Tasliym.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Liqaa’ ash-Shahriy (30) http://binothaimeen.net/content/695
  • Imechapishwa: 25/10/2017