Amefanya makosa mengi pamoja na kuapa kwa kusema uongo wakati wa Ramadhaan

Swali: Nimefanya makosa mengi katika funga yangu. Nataraji kwa Allaah atanisamehe. Ni ipi kafara ya kusema uongo niliosema? Ni ipi kafara ya kuapa kwa jina la Allaah hali ya kusema uongo? Nimeapa kiapo kikubwa juu ya jambo maalum kisha nikakhalifu kiapo hiki na hivi sasa nataka kutubu na kukafiria kiapo hiki. Lakini hata hivyo sikumbuki vilikuwa viapo ngapi?

Jibu: Swali hili lina mambo mengi:

1- Makosa mengi wakati wa kufunga. Ni kipi mtu anachoweza kufanya? Anachoweza mtu kufanya ni kutubu kwa Allaah (´Azza wa Jall). Mtu anatakiwa kujuta, nafsi yake iathirike na atie maazimio ya kutorudi. Akitubu kwa Allaah basi atambue kuwa Allaah anasema:

قُلْ يَا عِبَادِيَ الَّذِينَ أَسْرَفُوا عَلَىٰ أَنفُسِهِمْ لَا تَقْنَطُوا مِن رَّحْمَةِ اللَّـهِ ۚ إِنَّ اللَّـهَ يَغْفِرُ الذُّنُوبَ جَمِيعًا

“Sema: Enyi waja Wangu ambao wamechupa mipaka juu ya nafsi zao: “Msikate tamaa na rehema za Allaah, hakika Allaah anasamehe dhambi zote.”[1]

Dhambi yoyote unayotubia kwayo Allaah anakusamehe.

2- Kuhusu kiapo alichoapa lakini hata hivyo hajui ni viapo ngapi, achukue ile idadi ya chini. Kwa mfano kama amekadiria kuwa ni viapo kumi au ishirini, basi ajaalie kuwa ni kumi. Kwa sababu msingi ni kutakasika kwa dhimma. Halazimiki kafara ambayo hakujua kuwa imemuwajibikia.

[1] 39:53

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Liqaa´ ash-Shahriy (61) http://binothaimeen.net/content/1382
  • Imechapishwa: 08/06/2020