Swali: Mwanamke amejiharamishia sigara na akaapa kwa Qur-aan kwamba hatorudi kuvuta sigara na hatimaye akavuta. Baada ya hapo akatoa kafara. Mwishowe mume wake akamlazimisha kuvuta kisha hakurudi tena kuvuta. Ni ipi hukumu?

Jibu: Mara hii ya mwisho ni kama ya kwanza; amejiharamishia kuvuta sigara kwa ajili ya kujizuia lakini hata hivyo akarudi. Hivyo ni lazima kwake kutoa kafara ya kiapo. Kafara aliyotoa ikiwa ni kwa kiwango cha kuwalisha masikini kumi basi dhimma yake imetakasika. Vinginevyo ni lazima kwake kuitakasa dhimma yake kwa kuwalisha masikini kumi.

Miongoni mwa makosa aliyofanya mume wake ni yeye kumwamrisha kurudi kuvuta sigara. Huku ni kumwamrisha kufanya maasi. Asingelimtii mume wake kwa jambo hilo. Haijuzu kwa mwanamke kumtii mume wake kwa kitu kilichoharamishwa.

Watu walitofautiana juu ya hukumu ya sigara mara ya kwanza ilipojitokeza. Wako walioihalalisha, wengine wakaiharamisha, wengine wakaichukulia kuwa imechukizwa na wengine wakasema kuwa bora zaidi ni mtu kujiepusha nayo. Lakini baada ya kubaini madhara yake kwa makubaliano ya madaktari wote wa leo ikatubainikia na sisi ya kwamba ni haramu na kwamba haijuzu kwa mtu kuivuta. Kwa sababu inapelekea madhara kwenye mwili, kuharibu pesa bila faida na pia ina harufu mbaya ambayo inamuudhi yule ambaye hajazowea kuivuta.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Nuur ´alaad-Darb (19) http://binothaimeen.net/content/6837
  • Imechapishwa: 14/09/2021