Allaah pekee ndiye awezaye kuuokoa ulimwengu kutokamana na janga la corona


Himdi zote njema anastahiki Allaah, Mola wa walimwengu. Swalah na salamu zimwendee Mtume wetu Muhammad, kizazi chake na Maswahabah zake wote.

Kutokana yale yanayowapitikia watu waislamu hii leo na walimwengu wote kwa ujumla janga la maradhi ya corona ambayo wamekufa kwa sababu yake watu wengi na bado yanaendelea kuwa ni tishio kwa watu wengine, hivyo ni lazima kwa walimwengu wote na kwaswa waislamu kurejea kwa Allaah ili ayaondoshe maradhi haya. Kwani ni Yeye Allaah (Jalla wa ´Alaa) ndiye ameyateremsha na ni Yeye ndiye muweza wa kuyaondosha na kuwalinda waislamu kutokamana nayo. Allaah (Jalla wa ´Alaa) amesema:

وَإِذَا مَسَّكُمُ الضُّرُّ فِي الْبَحْرِ ضَلَّ مَن تَدْعُونَ إِلَّا إِيَّاهُ ۖ فَلَمَّا نَجَّاكُمْ إِلَى الْبَرِّ أَعْرَضْتُمْ ۚ وَكَانَ الْإِنسَانُ كَفُورًا

“Inapokuguseni dhara baharini hupotea wale mnaowaomba isipokuwa Yeye pekee. Pindi anapokuokoeni katika nchi kavu, mnakengeuka; mtu amekuwa ni mwingi wa kukufuru.”[1]

قُلْ مَن يُنَجِّيكُم مِّن ظُلُمَاتِ الْبَرِّ وَالْبَحْرِ تَدْعُونَهُ تَضَرُّعًا وَخُفْيَةً لَّئِنْ أَنجَانَا مِنْ هَـٰذِهِ لَنَكُونَنَّ مِنَ الشَّاكِرِينَ قُلِ اللَّـهُ يُنَجِّيكُم مِّنْهَا وَمِن كُلِّ كَرْبٍ ثُمَّ أَنتُمْ تُشْرِكُونَ

“Sema: “Nani anakuokoeni kutokamana na viza vya nchikavu na bahari mnapomuomba kwa kunyenyekea na kwa siri [huku mkisema]: “Akituokoa kutokamana na [janga] hili, bila shaka tutakuwa miongoni mwa wenye kushukuru.” Sema: ”Allaah anakuokoeni katika hayo na katika kila janga, halafu nyinyi mnamshirikisha!”[2]

Hakuna kimbilio kutokamana na khatari hii na nyenginezo isipokuwa kwa kurejea kwa Allaah, kunyenyekea mbele Yake na kumuomba du´aa kwa wingi ili ayaondoshe na shari zake na awasalimishe waislamu na walimwengu wote kutokamana nayo. Kwani hakika Allaah ndiye kayateremsha na Yeye ndiye muweza wa kuyaondosha, jambo ambalo ni lepesi kwa Allaah. Ni lazim kwetu kukumbuka udhaifu wetu na kumuhitajia kwetu Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala), kukithirisha kumwomba, kutoa swadaqah na kufanya matendo mema. Huenda Allaah akaondosha kile alichokiteremsha. Kwani hakika Yeye ndiye muweza wa hayo. Ni jambo litalofikiwa kwa kuomba kwa wingi, kuwatendea wema mafukara na masikini na matendo mema. Allaah yukaribu na mwenye kuitikia. Allaah (Jalla wa ´Alaa) amesema:

وَإِذَا سَأَلَكَ عِبَادِي عَنِّي فَإِنِّي قَرِيبٌ ۖ أُجِيبُ دَعْوَةَ الدَّاعِ إِذَا دَعَانِ

“Watakapokuuliza waja Wangu kuhusu Mimi, basi Mimi ni niko karibu; naitikia du’aa ya muombaji anaponiomba.”[3]

Ee Allaah! Ee Mola wetu, ee Mlinzi wetu! Hakika sisi ni waja Wako ambao ni wenye kukuhitajia Wewe. Tunakuomba utuondoshee janga hili na khatari hii kutoka kwa walimwengu wote na khaswa waisalmu na aweke badali yake wepesi na kheri. Hakuna mwengine anayesamehe madhambi isipokuwa Wewe na wala hakuna mwengine awezaye kuyaondosha mabalaa isipokuwa Wewe. Wewe ndiye Mola wetu na Mlinzi  wetu. Wewe unatutosheleza na ndiye mbora wa kuwakilishiwa mambo. Ee Allaah ondosa kile ulichoteremsha. Ee Allaah ondosa kile ulichoteremsha. Ee Allaah ondosha ugonjwa huu uliyoteremsha na weka badali yake faraja, wepesi, kheri na afya kwa walimwengu wote na khaswa waislamu. Wewe ndiye muweza wa jambo hilo:

قُلْ مَن يُنَجِّيكُم مِّن ظُلُمَاتِ الْبَرِّ وَالْبَحْرِ تَدْعُونَهُ تَضَرُّعًا وَخُفْيَةً لَّئِنْ أَنجَانَا مِنْ هَـٰذِهِ لَنَكُونَنَّ مِنَ الشَّاكِرِينَ قُلِ اللَّـهُ يُنَجِّيكُم مِّنْهَا وَمِن كُلِّ كَرْبٍ ثُمَّ أَنتُمْ تُشْرِكُونَ قُلْ هُوَ الْقَادِرُ عَلَىٰ أَن يَبْعَثَ عَلَيْكُمْ عَذَابًا مِّن فَوْقِكُمْ أَوْ مِن تَحْتِ أَرْجُلِكُمْ أَوْ يَلْبِسَكُمْ شِيَعًا وَيُذِيقَ بَعْضَكُم بَأْسَ بَعْضٍ ۗ انظُرْ كَيْفَ نُصَرِّفُ الْآيَاتِ لَعَلَّهُمْ يَفْقَهُونَ

“Sema: “Nani anakuokoeni kutokamana na viza vya nchikavu na bahari mnapomuomba kwa kunyenyekea na kwa siri [huku mkisema]: “Akituokoa kutokamana na [janga] hili, bila shaka tutakuwa miongoni mwa wenye kushukuru.” Sema: ”Allaah anakuokoeni katika hayo na katika kila janga, halafu nyinyi mnamshirikisha!” Sema: “Yeye ni muweza wa kukuleteeni adhabu kutoka juu yenu au kutoka chini ya miguu yenu au akutatanisheni mfarikiane kuwa makundimakundi na akuonjesheni baadhi yenu [mashambulizi kutoka] kwa wengineo.” Tazama jinsi Tunavyozipambanua Aayah wapate kufahamu.”[4]

Allaah (Jalla wa ´Alaa) ndiye muweza wa kila kitu. Yeye ndiye anawapa mtihani waja Wake. Lau isingelikuwa huruma, msamaha na wema Wake basi kusingelibaki juu ya ardhi kiumbe chochote. Lakini Yeye (Subhaanahu wa Ta´ala) ni msamehevu na Mwingi wa kurehemu, muweza wa kila jambo, Yeye yukaribu na mwenye kuitikia, Yeye ndiye mlinzi na mwenye kustahiki kuhimidiwa. Wewe ndiye Mlinzi wetu – mbora wa kulinda na mbora wa kunusuru. Ee Allaah ondosa kile ulichoteremsha. Ee Allaah ondosa kile ulichoteremsha. Ee Allaah ondosa kile ulichoteremsha.  Ee Allaah ondosha ugonjwa huu uliyoteremsha kutoka kwa walimwengu wote na khaswa waislamu. Ee Allaah! Tusalimishe kutokamana na shari za wenye shari, vitimbi vya watenda madhambi na majanga ya usiku na mchana. Wewe ndiye muweza wa kila jambo na wala hakuna pa kukimbilia wala uokozi kutokamana Nawe isipokuwa Kwako. Umetakasika kutokamana na mapungufu na kasoro zote, hakika sisi tumedhulumu. Umetakasika kutokamana na mapungufu na kasoro zote, hakika sisi tumedhulumu. Umetakasika kutokamana na mapungufu na kasoro zote, hakika sisi tumedhulumu. Ee Allaah! Tuondoshee majanga, magonjwa, shari na fitina zote. Kwani hakika Wewe juu ya kila jambo ni muweza. Hakika Wewe ndiye Mlinzi wetu – mbora wa kulinda na mbora wa kunusuru. Allaah anatutosheleza na ndiye mbora wa kuwakilishiwa mambo. Swalah na salamu zimwendee Mtume wetu Muhammad, kizazi chake na Maswahabah zake wote.

[1] 17:67

[2] 06:63-64

[3] 02:186

[4] 06:63-65

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://www.youtube.com/watch?v=fzQGaORfHwk&feature=youtu.be
  • Imechapishwa: 10/04/2020