Imaam an-Nawawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

19- Abul ‘Abbaas ´Abdullaah Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza:

“Siku moja nilikuwa nyuma ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akanambia: “Ee Kijana! Nitakufundisha maneno: Mhifadhi Allaah Naye Atakuhifadhi. Muhifadhi Allaah utamkuta mbele yako. Ukiomba, muombe Allaah, ukitafuta msaada tafuta kutoka kwa Allaah. Jua ya kwamba ikiwa taifa zima litaungana kukunufaisha wewe kwa kitu, basi hutonufaika isipokuwa kwa kitu alichokwishakuandikia Allaah. Kadhalika wakikusanyika kukudhuru kwa chochote, howatokudhu isipokuwa tu kwa kitu alichokwishakuandikia. Kwani kalamu zimeshanyanyuliwa na sahifa zimeshakauka.

Ameipokea at-Tirmidhiy ambaye amesema kuwa Hadiyth ni Hasan Swahiyh

Katika upokezi mwingine usiokuwa wa at-Tirmidhiy imekuja:

“Muhifadhi Allaah utakuta katangulia mbele yako. Mjue Mola Wako wakati wa raha Atakujua wakati wa shida. Jua kuwa yaliyokukosa hayakuwa yakukupata na yaliokupata hayakuwa yakukukosa. Jua kuwa ushindi uko pamoja na subira, na faraja iko pamoja na dhiki, na raha iko pamoja na shida.”

MAELEZO

Kule Allaah (Jalla wa ´Alaa) kumhifadhi mja katika dini ndio jambo kubwa linalotakikana. Kwa ajili hii ndio maana (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akimuomba Allaah mara nyingi amuhifadhi na fitina na moyo wake kutobadilika, kama katika kauli yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Ee Mwenye kuzigeuza nyoyo! Uthibitishe moyo wangu katika utiifu Wako.”

Ameipokea at-Tirmidhiy (2140)

Kitu kikubwa ambacho mja anatakikana kukipupia ni kusalimika katika dini yake. Allaah (Jalla wa ´Alaa) anaweza kumpa mja mtihani wa kuwa na kasoro katika dini yake na kupatwa na utata kwa kupuuzia mambo ambayo anawajibika kumtekelezea nayo Allaah (Jalla wa ´Alaa). Kwa hivyo, mja akipatwa na kasoro katika dini basi ametoka katika ulinzi wa Allaah (Jalla wa ´Alaa). Anaweza kuadhibiwa kwa kufanywa kuwa mwenye kughafilika, kunyimwa elimu ya dini, kujiwa na utata na asijue ni vipi atautatua au akatumbukia ndani yake, kama Alivyosema (Jalla wa ´Alaa):

فَلَمَّا زَاغُوا أَزَاغَ اللَّـهُ قُلُوبَهُمْ

“Pindi walipopotoka, basi Allaah akazipotosha nyoyo zao.” (61:05)

نَسُوا اللَّـهَ فَنَسِيَهُمْ

“Wamemsahau Allaah, basi Naye amewasahau.” (09:67)

فَأَمَّا الَّذِينَ فِي قُلُوبِهِمْ زَيْغٌ فَيَتَّبِعُونَ مَا تَشَابَهَ مِنْهُ ابْتِغَاءَ الْفِتْنَةِ وَابْتِغَاءَ تَأْوِيلِهِ

“Basi wale ambao katika nyoyo zao mna upotovu, hufuata zile zilizoshabihiana kutafuta fitnah na kutafuta tafsiri zake.” (03:07)

إِنْ هِيَ إِلَّا فِتْنَتُكَ تُضِلُّ بِهَا مَن تَشَاءُ وَتَهْدِي مَن تَشَاءُ

“Haya si chochote isipokuwa ni majaribio Yako. Unampotoa kwayo Umtakaye na Unamwongoza Umtakaye.” (07:155)

Vilevile Aayah nyinginezo zinaonyesha ya kwamba mja anaweza kupotoshwa. Kupotoshwa katika dini ndio upotevu mkubwa.

Kwa ajili hii inatakikana kwa mja kuwa na pupa ya kumhifadhi Allaah (Jalla wa ´Alaa) katika maamrisho Yake, akipitikiwa akimbilie kuomba msamaha, kujuta na kuitakidi haki pasina kuwa na mashaka. Afuatishe jema kwa dhambi pengine ikafutwa.

  • Mhusika: Shaykh Swaalih bin ´Abdil-´Aziyz Aalush-Shaykh
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-Arba´iyn an-Nawawiyyah, uk. 281-282
  • Imechapishwa: 14/05/2020