Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

الَّذِينَ يُؤْمِنُونَ بِالْغَيْبِ وَيُقِيمُونَ الصَّلَاةَ وَمِمَّا رَزَقْنَاهُمْ يُنفِقُونَ

“Ambao wanaamini ghaibu na husimamisha swalah na hutoa sehemu ya vile tulivyowaruzuku.”[1]

Hapa kunaingia matumizi ambayo ni wajibu. Kwa mfano zakaah, wake, ndugu, watumwa na wengineo, na matumizi yaliyopendekezwa kwa njia zote za kheri. Hakutaja wapokeaji kutokana na wingi wa sababu zake na kusampulika kwa wingi watu wake. Jengine ni kwa matumizi yenyewe kama yenyewe ni kujikurubisha kwa Allaah.

Hiyo من iliyotajwa hapo inafahamisha sehemu tu. Lengo ni kuwazindua kwamba hakuna anachotaka kutoka kwao isipokuwa kiwango kidogo tu kutoka katika mali yao kisichowadhuru wala kuwatia uzito. Bali wao ndio wenye kunufaika kwacho kwa kule kukitoa na pia wananufaika ndugu zao. Maneno Yake:

رَزَقْنَاهُمْ يُنفِقُونَ

“… tulivyowaruzuku.”

kuna ishara kwamba mali hii ilioko mikononi mwenu hamkuipata kwa sababu ya nguvu au uwezo wenu. Bali ni riziki ya Allaah aliyokutunukuni na akakuneemesheni. Kama ambavo amekuneemesheni na akakufadhilisheni juu ya waja Wake wengine wengi, basi mshukuruni kwa kutoa baadhi ya yale aliyokuneemesheni na wapeni ndugu zenu masikini.

Mara nyingi Allaah katika Qur-aan anakusanya kati ya swalah na zakaah. Kwa sababu ndani ya swalah kuna kumtakasia nia Muumba. Upande wa pili ndani ya zakaah na matumizi kuna kuwafanyia wema waja Wake. Anwani ya furaha ya mja ni kule kumtakasia nia Muumba na kujibidisha kuwanufaisha viumbe kama ambavo anwani ya maangamivu na khasara ya mja ni kutokuwa na mambo haya mawili. Kwa msemo mwingine mtu akawa hana kumtakasia Allaah nia wala kuwatendea waja wema.

[1] 02:03

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdur-Rahmaan bin Naaswir as-Sa´diy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Taysiyr-ul-Kariym, uk. 30
  • Imechapishwa: 05/05/2020