Swali: Mimi ni mjane wa Kiislamu Alhamduli Allaah ambaye ninafunga na kuswali. Nilisibiwa na maradhi makubwa siku miongoni mwa siku katika Ramadhaan ambayo yalikuwa yanataka kuniua. Nikawa nimekula kutokana na ukubwa wa maradhi kisha nikalipa siku hii. Anauliza kama kula kwake (siku hii ya Ramadhaan) ana madhambi?

Jibu: Hana madhambi, bali ni mwenye kupewa ujira. Mtu akisibiwa na maradhi, na Swawm ikamkuwia kwake nzito inajuzu kwake kula na ni mwenye ujira kwa kuchukua rukhusa (ya Allaah). Anasema Allaah (Subhaanah):

فَمَن كَانَ مِنكُم مَّرِيضًا أَوْ عَلَىٰ سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِّنْ أَيَّامٍ أُخَرَ

“Basi atakayekuwa mgonjwa miongoni mwenu, au yuko safarini (akafunga baadhi ya siku); basi (akamilishe) idadi (ya siku anazotakiwa kufunga) katika siku nyinginezo.” (02:184)

Na anasema Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hakika ya Allaah Anapenda kuchukuliewa (mambo ya) rukhusa Zake kama Anavyochukia kufuatwa maasi Yake (Aliyokataza).”

Mtu akichukua rukhusa kwa kumtii Allaah na kufanyia kazi Aliyoyaweka katika Shari´ah (Ta´ala), ni mwenye ujira na hana madhambi. Wewe dada muulizaji huna dhambi juu yako kwa kula kwako kutokana na hali ya maradhi. Na ni juu yako kulipa na umekwishafanya hivyo Alhamdulillaah.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Nuur ´alaad-Darb
  • Imechapishwa: 03/04/2018