al-Khaliyliy amekubali mwenyewe ya kwamba kizazi cha kwanza katika as-Salaf as-Swaalih kilipita pasi na masikio yao kusikia kabisa kabisa neno hata moja kuhusu mada hii[1]. Hivi ndivyo alivyosema. Lakini anajifanya kukosea na kutaka kuwapaka wasomaji mchanga wa machoni. Anasema kuwa as-Salaf as-Swaalih hawakusema na anadai kitu asichokuwa nacho dalili. Haya hapa maelezo yake ya sentesi aliyosema ya kwamba as-Salaf as-Swaalih kiliisha kizazi chao pasi na masikio yao kusikia neno hata moja juu ya mada hii. Amesema:

“Walikuwa ni wenye kuafikiana juu ya kwamba Allaah ndiye muumbaji wa kila kitu na kila kisichokuwa Yeye kimeumbwa na kwamba Qur-aan ni kama vitabu Vyake vingine vilivyoteremshwa, maneno ya Allaah[2], Wahy Wake na uteremsho Wake. Haya ndio waliyoafikiana nayo waislamu wote wakati wa Imaam al-Muhannaa bin Ja´far.”[3]

Hivi ndvyo anavyosema. Haya ni maneno yaliyozugwazugwa ambayo hakuna ayajuaye isipokuwa yule anayejua ´Aqiydah ya Mu´tazilah na wale wanaofuata maoni yao na wanaonelea kuwa ´Aqiydah yao juu ya maneno ya Allaah (´Azza wa Jall) na maoni yao yaliyo wazi kabisa ya kwamba Qur-aan tukufu imeumbwa. Hayo ndiyo yanayowekwa wazi na mwandishi al-Khaliyliy katika kitabu chake hichi. Hili hapa jawabu ili kufichua kosa hili la kukusudia. Tunamraddi ifuatavyo:

“Maneno yake ya kwamba kizazi cha kwanza katika as-Salaf as-Swaalih kilipita pasi na masikio kabisa kabisa kusikia neno hata moja kuhusu mada hii.”

Hilo ni kweli. Hilo si kwa sababu nyingine isipokuwa ni kwa kuwa as-Salaf as-Swaalih katika Maswahabah na wale waliowafuata kwa wema hawakuzua katika mada hii. Bali walikuwa wakiamini na wakisadisha ya kwamba Qur-aan ni maneno ya Allaah (´Azza wa Jall) ambayo amezungumza kwayo kikweli vile alivyotaka ambapo Jibriyl (´alayhis-Salaam) akayasikia kutoka Kwake, akateremka nayo kwa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Allaah akaamrisha kuwalingania watu kwayo. Hakika yeye mwenyewe (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akijionyesha kwa makabila mbalimbali na akiwaomba wamsaidie juu ya kuwafikishia watu maneno ya Mola Wake. Imaam na al-Haafidhw Ibn Mandah amepokea katika “Kitaab-ut-Tawhiyd” kwa mlolongo wa wapokezi wake kupitia kwa Jaabir bin ´Abdillaah (Radhiya Allaahu ´anh) aliyeeleza:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akijionyesha kwa watu katika kisimamo na kusema: “Hakika Quraysh wamenizuia nisiyafikishe maneno ya Mola Wangu.””

Kizazi cha kwanza kimepita juu ya ´Aqiydah hii. Kuhusu maneno yake:

“Walikuwa ni wenye kuafikiana juu ya kwamba Allaah ndiye muumbaji wa kila kitu.”

Huku ni kutaka kumpaka mpenzi msomaji na wengineo vievile wasiojua ´Aqiydah ya Mu´tazilah mchanga wa machoni. Hakika al-Khaliyliy anawakilisha ´Aqiydah ya Mu´tazilah inapokuja katika maneno ya Allaah na inapokuja katika Qur-aan tukufu ambayo Allaah amezungumza kwayo na Jibriyl (´alayhis-Salaam) akayasikia kutoka Kwake ambapo akawa ameteremka nayo kwa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambaye ni Mtume mwaminifu.

al-Khaliyliy ambaye anaitakidi kuwa Qur-aan imeumbwa na kulingania katika hilo anataka kuyaingiza maneno ya Allaah (´Azza wa Jall) katika jumla ya maneno Yake (Ta´ala):

الله خالق كل شيء

“Allaah ndiye muumba wa kila kitu.”

na kunaamisha ya kwamba Qur-aan tukufu ni kitu na hivyo basi nayo itakuwa imeumbwa.

Hizi ni mbwembwe zinazotambulika tokea wakati wa Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) na wanachuoni wa Salaf ambapo waliwaraddi wenye nazo kwa dalili za wazi kabisa na hoja za kukata na wakazisambaratisha kwa dalili za Qur-aan na Sunnah Swahiyh. Maneno ya al-Khaliyliy ni kuwazulia uongo Salaf. as-Salaf as-Swaalih anaowaashiria yeye kwa lengo la kutaka kujificha nyuma ya ´Aqiydah yake ambayo ni batili juu ya Qur-aan hawakuyaingiza maneno ya Allaah (Jalla wa ´Alaa) katika vitu vilivyoumbwa. Kwa kuwa Allaah (´Azza wa Jall) Yeye ndiye amewaumba viumbe wote kwa maneno Yake. Amesema (Ta´ala):

إِنَّمَا قَوْلُنَا لِشَيْءٍ إِذَا أَرَدْنَاهُ أَن نَّقُولَ لَهُ كُن فَيَكُونُ

“Hakika Kauli Yetu juu ya kitu tunapokitaka hukiambia: “Kuwa!” – basi kinakuwa.”[4]

Neno lake Allaah “Kuwa!” katika Aayah ndilo analoumba kwalo vile viumbe vyote anavyovitaka.

Salaf wameafikiana wote ya kwamba viumbe vyote kuanzia mbingu, ardhi, bahari, milima na miti na mbingu na ardhi na vilivyomo ndani yake vyote hivyo ni katika viumbe vya Allaah. Allaah hakushirikiana na yeyote katika kuviumba. Uumbaji na amri vyote viwili ni Vyake.

[1] Ya kuumbwa au kutokuumbwa kwa Qur-aan.

[2] Tazama http://www.wanachuoni.com/content/ulazima-wa-kuongeza-sentesi-haikuumbwa

[3] Uk. 106

[4] 16:40

  • Mhusika: ´Allaamah ´Aliy bin Naaswir al-Faqiyhiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ar-Radd al-Qawiym, uk. 192-194
  • Imechapishwa: 14/01/2017