Swali: Ni yapi maoni yako kuhusiana na vitabu vifuatavyo ”Fiy Dhwilaal-il-Qur-aan” cha Sayyid Qutwub, vitabu vya ash-Shawkaaniy na vitabu vya Hasan al-Bannaa?

Jibu: Ninamuomba Allaah (Ta´ala) aniwafikishe kujibu sawa maswali haya. Ni maswali magumu. Sio mepesi. Kwa kuwa baadhi ya vitabu hivi vimekuwa na athari kati ya vijana wetu. Kuna madai ya kipotofu katika nisba ya baadhi ya vitabu hivi.

Kitabu cha kwanza ”adh-Dhwilaal” cha Sayyid Qutwub. Ni tafsiyr ya Qur-aan ambayo haikujengeka juu ya Athar wala lugha. Ni muundo na mchanganyiko wa maoni ya Ashaa´irah, Wahdat-ul-Wujuud na Suufiyyah. Ninawaambilisha ukweli wa wazi kabisa. Ninawaomba kwa kuwaelekeza kwenda kusoma miongoni mwa Suurah fupi katika Qur-aan. Someni aliyoandika Sayyid Qutwub juu ya tafsiyr ya Suurah al-Ikhlaasw. Ama wanafunzi wadogo hawatotoka na natija yoyote kabisa, kwa kuwa ameandika kwa usulubu wa Ibn ´Arabiy at-Twaa´iy ambaye ndio raisi wa Wahdat-ul-Wujuud. Ameongea kuhusu upekee. Hata hivyo hakuongelea kuhusu upekee wa Kiislamu. Ameongelea upekee wa Wahdat-ul-Wujuud. Kwa ajili hiyo amesema Sayyid Qutwub, hakika ya uwepo wa kikweli ni uwepo wa Allaah Mmoja na kwamba matendo ya kiukweli ni matendo ya Allaah Mmoja.

Lau utamuuliza mwanafunzi mmdogo mwenye kusoma tafsiyr hii katika baadhi ya masomo leo na inayogawiwa katika Maktabah na katika baadhi ya Misikiti ni nini amestafidi wakati ataposoma ya kwamba uwepo wa kiukweli ni uwepo wa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala), na kwamba kutenda kwa kiukweli ni kutenda kwa Allaah. Nini maana ya maneno haya? Ikiwa tutayafasiri kwa lugha ya kiarabu, na si kwa lugha ya Ibn ´Arabiy at-Twaa-iy, basi inaweza kuleta maana mbili:

Ya kwanza: Kila kitu kisichokuwa Allaah kina uwepo wa majazi. Uwepo wa viumbe vyote sio uwepo wa kiukweli. Ni uwepo tu wa majazi. Maneno batili.

Ya pili: Upekee wa kiukweli, ambao ni upekee wa Allaah, maana yake Allaah Amekuwa kitu kimoja na Viumbe Vyake. Kwa njia hiyo hakuna upekee isipokuwa upekee Wake na uwepo wake tu. Haya ndio madhehebu ya Ibn ´Arabiy at-Twaa-iy. Ni yeye ndiye aliyesema:

Mola ni mja na mja ndiye Mola

Sijui ni nani aliyekafilishwa kwa matendo yake.

Ni Ibn ´Arabiy ndiye aliyesema:

”Hakuna kilichomo ndani ya juba isipokuwa ni Allaah tu.”

Ikiwa anakusudia haya, basi hii ni kufuru ya wazi. Kwa kuwa amedai Allaah kuwa kitu kimoja na Viumbe na kusema ya kwamba kuna uwepo mmoja tu. Ulimwengu wote huu kuna uwepo mmoja na si zaidi. Maana yake ni kwamba Mola na mja ni kitu kimoja.

Kutokana na dini ya Ibn ´Arabiy kuna mtu anasema:

“Mbwa na nguruwe si lolote isipokuwa ni Mola Wetu.

Allaah si kitu isipokuwa mtawa kwenye kanisa.”

Mshairi wao Ibn-ul-Faaridh anaabiri kwa maneno haya na kusema:

“Ninaswali Swalah zangu katika mahala.

Ambapo nashuhudia ya kwamba pameniswalia mimi.”

Anasema hivi kwa kuwa anaonelea kuwa Allaah ni kitu kimoja na yeye.

Namna ya Sayyid Qutwub katika kufasiri Suurah al-Ikhlaasw inafasiriwa kwa maana hii.

Tukizidi kwenda chini na kusema ya kwamba maneno yake yanaweza kufasiriwa kwa njia nyingine, nayo ni kuwa uwepo mwingine wote usiokuwa wa Allaah ni uwepo wa majazi na kwamba matendo yasiyokuwa ya Allaah ni matendo ya majazi na kwamba mtendaji wa kiukweli ni Allaah Mmoja, basi itakuwa ni ´Aqiydah ya Jabriyyah. Kwa kuwa wanaonelea ya kwamba mja sio mtendaji wa kiukweli na kwamba mwenye kutenda hayo ni Allaah. Hii ndio ´Aqiydah ya Ashaa´irah. Kuwa Sayyid Qutwub ni Ash´ariy hili halina mashaka yoyote. Lau angelikuwa hai na akasikia anayosema Ash´ariy basi angelifurahi na asingelihuzunika. Ashaa´irah ni wenye fakhari kwa Ash´ariyyah. Sio usengenyaji. Mwenye kusema kuwa Sayyid Qutwub na mfano wake ya kwamba ni Ashaa´irah hakuwasengenya na wala hakusema isipokuwa yaliyo ya kweli. Atakuwa hakusema isipokuwa wayapendayo na wanayojifakharisha nayo.

Ni kama tulivyosema ni tafsiyr ya ki-Ashaa´iyrah. Huko kuna mchanganyiko wa Ashaa´irah, Suufiyyah na Wahdat-ul-Wujuud. Soma tafsiyr ya Suurah al-Ikhlaasw na Suurah al-Hadiyd. Yanatosheleza.

Kutokana na haya tunawanasihi wanafunzi wadogo wasisome tafsiyr ya hii Qur-aan. Kama jinsi tunavyowanasihi wanafunzi wakubwa kuisoma na kujua shari iliyomo ili waweze kuwanasihi wanafunzi wadogo. Dini ni kupeana nasaha.

Ama kuhusiana na vitabu vya ash-Shawkaaniy, haviko katika mkumbo huu. Ni aina nyingine. Imaam ash-Shawkaaniy alikuwa Imaam na mwanachuoni katika misingi, kiarabu, Hadiyth na Fiqh. Isipokuwa Imaam huyu mwanzoni mwa uhai wake alikuwa katika ´Aqiydah ya Mu´tazilah kwa kuwa alikuwa Zaydiy. Zaydiyyah na mapote mengine yote ya Shiy´ah yana ´Aqiydah ya Mu´tazilah. Hata hivyo Allaah Akamuokoa Imaam huyu. Akaacha maeneo ya Zaydiyyah bila ya kubaki maeneo ya Shaafi´iyyah. Akajaribu kujiunga na madhehebu ya Salaf. Akajitahidi kwa hilo jitihada iliyokuwa kubwa kabisa. Hata hivyo ´Aqiydah yake kwa nisba ya Sifa za Allaah haikuwa safi kama inavyotakikana. Kwa ajili hiyo akaweza kuanguka katika kuyafanyia taawili baadhi ya maandiko [katika Qur-aan na Sunnah]. Jitihada yake ilimpelekea mwishoni kufahamu ya kwamba Salaf walikuwa wanatumia Tafwiydhw. Pamoja na hadhi yake tukufu na ubobeaji wake wa elimu hakuweza kutofautisha baina ya Tafwiydhw ya Salaf na Tafwiydhw ya Mufawwidhwah. Tafwiydhw ya Salaf inahusiana na kwamba mtu hawezi kujua uhakika wa namna ya Sifa na namna yake zilivyo wakati huo huo wanajua maana ya maandiko. Manhaj na madhehebu ya Salaf kwa nisba ya maana ya Sifa, wanajua maana ya Kauli Yake Allaah (Ta´ala):

الرَّحْمَـٰنُ عَلَى الْعَرْشِ اسْتَوَىٰ

“Mwingi wa rehema amelingana juu ya ´Arshi.” (20:05)

Wanajua maana ya “kuja” katika Aayah:

وَجَاءَ رَبُّكَ وَالْمَلَكُ صَفًّا صَفًّا

”Atakapokuja Mola wako, na Malaika safusafu.” (89:22)

Wanajua maana ya “Kushuka”:

“Mola Wetu (Tabaaraka wa Ta´ala) anashuka… “

Wanajua maana ya Uso, Mkono, Kusikia na Kuona maana yake. Hivyo basi, ni kipi wasichojua na kumuachia Allaah? Namna ya Sifa za Allaah (Ta´ala) zilivyo. Wana kanuni inayosema ya kuwa maneno kuhusu Sifa ni tawi la maneno kuhusu Dhati na kwamba vinaenda mkono kwa mkono. Kama jinsi tunavyoamini Dhati ya Allaah kwa Imani, kuthibitisha na kujisalimisha bila ya kuulizia namna gani – hatuulizii namna ya Dhati ya Allaah (Subhaanahu) – vivyo hivyo hatuulizii vilevile Sifa Zake. Hatuulizii Yuko juu namna gani, Anakuja namna gani, Anashuka namna gani, namna gani ulivo Uso Wake na Mkono Wake. Hatusemi hivi na wala hatuulizii swali kama hili.

Badala yake tunasema ya kwamba Kustawaa (kuwa Kwake juu), Kushuka, Kuja, Kusikia, Uso vinajulikana tofauti na namna yake. Kuamini Sifa hizo ni wajibu. Kuulizia namna yake ni Bid´ah. Haya ndio madhehebu ya Salaf.

Ibara hii mara ya kwanza kuisikia ilikuwa ni kwa Imaam Maalik (Rahimahu Allaah). Alikuwa ni katika wakubwa wa waliokuja baada ya Taabi´iyn. Kwa sababu kabla ya kuja zama za waliokuja baada ya Taabi´iyn, hakuna yeyote angeliweza kuja na kuuliza Allaah Yuko juu namna gani, Anashuka namna gani na namna gani Anavyokuja. Hakuna yeyote angeliweza kuthubutu kuuliza kitu kama hicho. Lakini Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisema kweli pale aliposema:

“Hakuna mwaka isipokuwa ulio baada yake unakuwa ni wa shari zaidi.”

Maswali kama haya yalianza katika zama za waliokuja baada ya Taabi´iyn na yakaendelea. Na leo ni mabaya zaidi. Leo watu wanathubutu zaidi kwa Allaah.

Ninachotaka kusema ni kwamba Imaam ash-Shawkaaniy hakukutakana na ufafanuzi huu. Sababu ilikuwa hana mtu wa kumrudilia ambaye alikuwa na madhehebu ya Salaf na Mashaykh Salafiyyuun. Hata hivyo alifanya kila aliwezalo. Kwa ajili hiyo tunataraji taawili zilizopitika kwake zinafunikwa na bahari ya elimu aliyokuwa nayo na kazi yake kubwa juu ya Qur-aan, Sunnah na Uislamu. Si sawa kuwa na dhana mbaya kwake. Si sawa kumtuhumu kuwa alikuwa ni Ash´ariy au mzushi, kama wanavyosema baadhi ya vijana wakali na wenye papara. Usilichukulie, baadhi ya vijana wetu wana aina ya papara.

Hivyo ninasema haya kuwaambia ili wasiwe na papara. Ninawatahadharisha kuwa na papara na khaswa kwa wanachuoni wakubwa ambao wameitumikia Sunnah na Uislamu kama Imaam ash-Shawkaaniy, Imaam as-Swan´aaniy, Imaam Ibn Hajar, an-Nawawiy na mfano wao. Makosa yao juu ya baadhi ya Sifa zisiwazuie kutofaidika kutokana na elimu iliobobea na elimu yenye manufaa. Inatakiwa kufaidika navyo. Yanayosemwa juu ya baadhi ya vijitabu vya Imaam ash-Shawkaaniy – ar-Rasaail as-Salafiyyah – ibara hii iko kati ya vidole. Vinginevyo sio Salafiyyah safi. Ndani yake kuna utata.

Kisha akasema – yaani muulizaji – vitabu vya Hasan al-Bannaa. Mimi sijui kuwa Hasan al-Bannaa ana vitabu. Ninajua tu kuwa ana baadhi ya vijitabu ambapo ndani yake amehadithia kuhusu siasa yake na harakati zake za kisiasa. Sijui kuwa ana baadhi ya vitabu vya kielimu. Vijitabu hivi vimehadithia harakati zake, siasa yake, kuwakusanya kwake watu na kupinzana kwake na vyama vingine. Kwa kuwa chama hichi cha kisiasa – yaani cha al-Ikhwaan al-Muslimuun – kimeundwa ili kipinzane na vyama vingine vya siasa vilivyokuwa wakati huo. Kwa ajili hiyo kutokana na akili yake akajaribu Hasan al-Bannaa kuwa pamoja nae Suufiyyah, Ash´ariyyah na Salafiyyah ili wapinzane na vyama vingine kama al-Qawmiyyuun, ´Ilmaaniyyuun na mfano wao. Kwa ajili hiyo akajaribu akusanye katika chama chake mgongano, Suufiyyah na Ash´ariyyah. Kama jinsi mnavyojua katika baadhi ya vijitabu vyake aliweka kichwa cha khabari.

Kwa kifupi, hivi sio vitabu vya kielimu. Ni vijitabu vilivyo na maelekeo kwa wafuasi wa siasa yake na mfumo wake anaotaka. Kwa ajili hii kutaja hizi vijitabu pamoja na vitabu vya ash-Shawkaaniy sio jambo la sawa.

  • Mhusika: ´Allaamah Muhammad Amaan al-Jaamiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: http://www.eljame.com/
  • Imechapishwa: 22/05/2022