al-Fawzaan akielezea rai tatu tofauti za Ahl-us-Sunnah kuhusu darsa na mawaidha ya video na kwenye TV

Swali: Inajuzu kurekodi kanda za mihadhara kwa njia ya video na kuuza kanda hizi katika baadhi ya maduka ya rekodi? Pamoja na kuzingatia ya kwamba kunakuwepo vilvile kanda za maonyesho na tamthiliya/filamu zinazoitwa “tamthiliya/filamu za Kiislamu”. Ni yepi maoni yako juu ya hilo?

Jibu: Masuala ya kurekodi mihadhara kwa njia ya video au kwa njia ya TV ni jambo limefanyiwa utafiti. Upande mmoja ndani yake kuna manufaa; kuwafikishia watu kheri na kuwafundisha. Lakini upande mwingine kuna madhara vilevile; picha. Kwa hivyo masuala haya ni yenye mashaka. Iwapo tutatazama zile kheri zinazopatikana ndani yake tunaweza kusema kwamba kheri inatakiwa kuenezwa. Lakini tukitazama picha zinazopatikana ndani yake tunaweza kusema kuwa haya ni madhara na wala haijuzu kuchukulia wepesi suala la picha ambalo limeharamishwa na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwa hiyo jambo hili mimi nimenyamaza. Kutokana na ninavyojua wanachuoni wana maoni tatu:

1- Wapo ambao wanaonelea kuwa ni haramu. Wameupa nguvu upande wa uharamu kutokana na jambo la picha. Hawa wanaonelea kuwa kuna uwezekano wa kuwafunza watu na kueneza elimu pasi na kutumia njia hii.

2- Wapo wengine ambao wameupa nguvu upande wa manufaa na wakajuzisha kurekodi mihadhara ya kidini ya video na kwenye TV kwa kutazama zaidi upande wa manufaa. Wanachuoni hao wao wenyewe wameshiriki na kuhudhuria kwenye TV. Wapo wanachuoni waliofanya hivi. Wana mtazamo wao unaoangaliwa.

3- Kuna wengine ambao wamenyamaza.

Kwa hivyo masuala kuna utafiti ndani yake. Kila mwanafunzi ayape nguvu yale maoni ambayo anaonelea yeye kuwa yana nguvu. Kuhusu mimi nanyamaza kuhusu masuala haya.

Kuhusu filamu hakuna tamthiliya/filamu za Kiislamu. Tamthiliya/filamu hizi ni za maonyesho. Kwa hiyo zinatakiwa kuitwa “tamthiliya/filamu za maonyesho”. Vilevile zinatakiwa kuitwa “sanaa za kiaina”. Kusema kwamba ni tamthiliya/filamu za Kiislamu si kweli. Katika Uislamu hakuna tamthiliya/filamu kwa sampuli hii ambazo zimetuingilia kutoka huko Ulaya na Marekani. Uislamu umejitosheleza kutokamana na tamthiliya/filamu hizi.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://soundcloud.com/user-621373875/al-fawzaan-kuhusu-mawaidha-ya-video-camera-na-kwenye-tv
  • Imechapishwa: 27/04/2018