Swali: Tuna Shaykh ambaye ana elimu lakini wanawatukana Mashaykh ambao hawakubaliani naye na khaswa Shaykh Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy. Anamtahadharisha takriban kila siku usiku wa Ramadhaan. Anasema kuwa hayo ndio maoni ya kila muheshimiwa juu ya al-Albaaniy na kwamba hana kazi nyingine zaidi ya kufanya biashara ya vitabu. Unasemaje na unaonelea nini juu ya al-Albaaniy ili tupate kumjuza?

Jibu: Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy ni miongoni mwa ndugu zetu waaminifu msitari wa mbele wanaotambulika kwa elimu, ubora na kuzitilia umuhimu Hadiyth Swahiyh hali ya kuzisahihisha na kuzidhoofisha. Hakulindwa na makosa. Wakati mwingine anaweza kukosea wakati anaposahihisha na kudhoofisha. Lakini haijuzu kumtukana, kumsema vibaya wala kumsengenya. Bali kilichowekwa katika Shari´ah ni kumwombea du´aa azidi kuafikishwa na kuwa na nia njema na matendo. Ambaye atapata kosa la wazi kwa mujibu wa dalili basi analazimika kumnasihi na kumwandikia. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Dini ni kupeana nasaha.”

“Muislamu ni ndugu yake muislamu; hamkoseshi nusura… “

Jariyr bin ´Abdillaah al-Balkhiy amesema:

“Nilikula kiapo kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) juu ya kusimamisha swalah, kutoa zakaah na kumnasihi kila muislamu.”

Ni jambo linalotambulika kwamba waumini wa kiume na wa kike, na khaswa wanazuoni, ni marafiki wandani wao kwa wao. Allaah (Subhaanah) amesema:

وَالْمُؤْمِنُونَ وَالْمُؤْمِنَاتُ بَعْضُهُمْ أَوْلِيَاءُ بَعْضٍ ۚ يَأْمُرُونَ بِالْمَعْرُوفِ وَيَنْهَوْنَ عَنِ الْمُنكَرِ وَيُقِيمُونَ الصَّلَاةَ وَيُؤْتُونَ الزَّكَاةَ وَيُطِيعُونَ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ ۚ أُولَـٰئِكَ سَيَرْحَمُهُمُ اللَّـهُ ۗ إِنَّ اللَّـهَ عَزِيزٌ حَكِيمٌ

“Waumini wanaume na waumini wanawake ni marafiki wao kwa wao; wanaamrisha mema na wanakataza maovu na wanasimamisha swalah na wanatoa zakaah na wanamtii Allaah na Mtume Wake – hao Allaah atawarehemu. Kwani hakika Allaah ni Mwenye nguvu kabisa, Mwenye hekima.”[1]

Kwa hivyo ni lazima kwa wote kushauriani na kuusiana kwa yaliyo ya haki na kumzindua aliyekosea juu ya kosa lake na kumwelekeza katika yaliyo ya sawa kwa mujibu wa dalili za Shari´ah.

[1] 09:71

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: http://www.binbaz.org.sa/mat/3330
  • Imechapishwa: 29/06/2021