al-Albaaniy kuhusu mtawala anayeweka hukumu zilizotungwa na watu badala ya Shari´ah


Tukirudi katika Jamaa´at-ut-Takfiyr, au wale waliotokana nao, na kuwakufurisha kwao watawala na wale wanaoishi chini yao na kuwafanyia kazi, basi tutaona namna ambavo fikira yao imejengeka juu ya fikira mbovu inayotokana na kwamba yule mwenye kufanya dhambi kubwa ni kafiri.

Mimi nilikutana na kikosi cha watu ambao walikuwa pamoja na Jamaa´at-ut-Takfiyr, kisha baadaye Allaah akawaongoza. Nikawaambia:

“Nyinyi mmewakufurisha baadhi ya watawala, ni kwa nini basi muwakufurishe maimamu, watoe khutbah, waadhini na watunzaji wa misikiti? Ni kwa nini mnawakufurisha waalimu wanaofunza Shari´ah kwenye mashule na maeneo mengine?

Wakasema:

“Kwa sababu watu hawa wameridhia hukumu ya watu hawa ambao wanahukumu kinyume na yale aliyoteremsha Allaah.”

Ikiwa kuridhika huku juu ya kuhukumu kinyume na yale aliyoteremsha Allaah ni ndani ya moyo, basi hapo kufuru haihusiani tena na ya kimatendo na inaenda katika kufuru ya kiimani. Mtawala yeyote anayehukumu kinyume na yale aliyoteremsha Allaah na wakati huohuo anaona kuwa ndio sawa kwa leo kinyume na hukumu ya Shari´ah inayotokana na Qur-aan na Sunnah basi hapana shaka yoyote kwamba hiyo inahusu kufuru ya kiimani na si kufuru ya kimatendo. Hukumu hiyohiyo inamgusa yule mwenye kuridhia ridhaa na mtazamo wake.

Isitoshe mosi ni kwamba hamuwezi kusema kwamba mtawala yeyote anayehukumu kwa hukumu za kimagharibi na za kikafiri – au nyingi katika hizo – anasema kuwa ni haki na ni sawa kutohukumu kinyume na hukumu ya Kiislamu. Wangelisema hivo kweli wangelikuwa ni makafiri.

Tukirudi kwa wananchi na ndani yao wamo wanazuoni, wema na wengineo, nawaulizeni ni vipi mnaweza kuwakufurisha kwa sababu tu wanaishi chini ya uongozi unaowakusanya wao kama ambavo unawakusanyeni nyinyi pia? Nyinyi mnasema kwa marefu na mapana kwamba ni makafiri wenye kuritadi na kwamba ni lazima kuhukumu kwa yale aliyoteremsha Allaah. Kisha mnasema hali ya kuzipa nyudhuru nafsi zenu kwamba kwa sababu tu mtu ameenda kinyume na hukumu ya ki-Shari´ah kimatendo peke yake hakupelekei kwamba mtendaji huyo yeye kama yeye anaritadi kutoka nje ya dini! Hayahaya ndio yanasemwa na wenzenu. Kikubwa mnachotofautiana nao, kwa dhuluma kabisa, ni kule tu kuwakufurisha kwenu.

Miongoni mwa jumla ya mambo yanayoweka wazi makosa na upotofu wao ni kuwauliza ni lini muislamu anahukumiwa kuwa ameritadi kutoka nje ya dini yake. Je, inatosha mara moja? Au ni lazima atangaze wazi kwamba ameritadi kutoka nje ya dini yake? Hawajui jawabu na wala hawatopatia. Kwa ajili hiyo tunalazimika kuwapigia mfano.

Hebu tuseme kwamba kuna hakimu ambaye mazowea yake anahukumu kwa Shari´ah. Lakini siku miongoni mwa siku akateleza na akahukumu kinyume na Shari´ah ambapo akampa haki dhalimu na akamnyima yule mdhulumiwaji. Huyu hapana shaka kwamba amehukumu kinyume na yale aliyoteremsha Allaah. Je, mnaweza kusema kwamba huyu amekufuru ukafiri wa kuritadi? Watasema hapana, kwa sababu huyu imetokea mara moja peke yake. Je, anakufuru iwapo atafanya hivo kwa mara ya pili na mara ya tatu na pia akaenda kinyume na hukumu ya ki-Shari´ah? Nikakariri swali hilo mara tatu au mara nne? Ni lini anakuwa kafiri? Hawawezi kuweka kikomo ni mara ngapi hukumu ya Shari´ah  inatakiwa kukhalifiwa ili mtu huyo asikufurishwe.

Ingawa wanaweza kufanya hivo kinyume na hivo kikamilifu. Wakijua kuwa mtu huyo katika hukumu yake ya kwanza ameona hukumu kinyume na yale aliyoteremsha Allaah kuwa ni nzuri, akaihalalisha na akadharau hukumu ya Shari´ah, hapo ni sahihi kabisa kusema kwamba mtu huyo amekufuru na kuritadi.

Kinyume chake. Endapo tutamuona mtu anahukumu hukumu kumi tofauti zinazokwenda kinyume na Shari´ah na tukamuuliza ni kwa nini amehukumu kinyume na yale aliyoteremsha Allaah, akasema kwamba ni kwa sababu amechelea juu ya nafsi yake au amepokea rushwa. Hili ni baya zaidi kuliko hilo la kwanza. Hata hivyo hatuwezi kusema kwamba ni kafiri mpaka yeye mwenyewe aseme kuwa hapendi kuhukumu kwa yale aliyoteremsha Allaah. Katika hali hiyo tunaweza kusema kwamba amekufuru ukafiri wa kuritadi nje ya dini.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fitnat-ut-Takfiyr, uk. 44-48
  • Imechapishwa: 28/06/2021