Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

وَإِن كُنتُمْ فِي رَيْبٍ مِّمَّا نَزَّلْنَا عَلَىٰ عَبْدِنَا فَأْتُوا بِسُورَةٍ مِّن مِّثْلِهِ وَادْعُوا شُهَدَاءَكُم مِّن دُونِ اللَّـهِ إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ

“Mkiwa mko katika shaka kutokana na Tuliyoyateremsha juu ya mja Wetu, basi leteni Suurah mfano wake na waiteni mashahidi wenu pasipo na Allaah mkiwa ni wakweli.”[1]

Hapa kuna dalili juu ya kwamba yule ambaye kuna matarajio juu yake ya kutoka upotofuni ni yule ambaye ana shaka na amechanganyikiwa kwa njia ya kwamba hajui haki ni ipi na upotevu ni upi. Huyu anapobainishiwa haki basi ni mwepesi sana kuongozwa muda wa kuwa ni mkweli katika kuitafuta ile haki.

Kuhusu mkaidi ambaye anaijua haki lakini hata hivyo akaiacha, huyu ni vigumu kusema ajirudi. Kwani huyu ameiacha baada ya kuwa mambo yamekwishambainikia na si kwamba ameiacha kwa ujinga. Kwa ajili hiyo hakuna namna juu yake.

Vivyo hivyo mwenye shaka ambaye si mkweli katika kuifuta kwake haki, bali ni mpuuzaji na si mwenye kujitahidi kuitafuta, mtu kama huyu mara nyingi haongozwi.

[1] 02:23

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdur-Rahmaan bin Naaswir as-Sa´diy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Taysiyr-ul-Kariym, uk. 35
  • Imechapishwa: 13/05/2020