Qadariyyah wamegawanyika sehemu mbili:

1 – Qadariyyah waliyopindukia.

2 – Qadariyyah walio kati kwa kati.

Qadariyyah waliyopindukia wamepinga daraja mbili za mwanzo ambayo ni kule kuyajua kwake mambo na kule kuyaandika.

Qadariyyah walio kati kwa kati wamepinga ujumla wa daraja mbili za mwisho. Wameamini elimu na uandishi wa Allaah, kwa msemo mwingine wamekiri hilo na wakasadikisha daraja mbili za mwanzo. Lakini pamoja na hivyo wamepinga ujumla wa daraja mbili za mwisho kama itakavyokuja huko mbele.

Qadariyyah waliyopindukia waliotangulia, kama mfano wa Ma´abad al-Juhaniy, ambaye Ibn ´Umar aliulizwa juu ya maneno yake, ´Amr bin ´Ubayd, wanapinga elimu ya Allaah iliyotangulia na ilioko huko mbele. Watu hawa wanadai vilevile kuwa Allaah anaamrisha na kukataza mambo lakini wakati huo huo hajui ni nani atakayemtii na atakayemuasi. Badala yake anasema kuwa mambo yako bure tu. Msemo huu ndio wa kwanza uliozushwa katika Uislamu baada ya kuisha karne za Makhaliyfah waongofu. Mtu wa kwanza aliyeleta hilo Basrah ilikuwa ni Ma´abad al-Juhaniy na mtu anayeitwa Ghaylaan ad-Dimashqiy akachukua kutoka kwake madhehebu haya. Maswahabah wengine wakamraddi ikiwa ni pamoja na ´Abdullaah bin ´Umar, ´Abdullaah bin ´Abbaas, Waathilah bin Asqaa´ na wengineo. Qadariyyah wamegawanyika makundi mawili:

Kundi la kwanza: Wanapinga kabisa kuwa Allaah alitangulia kuyajua mambo na wanadai kuwa Allaah hakuyakadiria mambo milele na hakutangulia kuyajua. Anayajua pale yanapotokea. Hawa ndio wale waliyopindukia.

Wanachuoni wamesema kuwa pote hili limetoweka na hawa ndio wale waliofanyiwa Takfiyr na maimamu kama Maalik, ash-Shaafi´iy na Ahmad. Hawa ndio wale ambao Imaam ash-Shaafi´iy (Rahimahu Allaah) alisema juu yao:

“Jadiliana na Qadariyyah kwa elimu. Wakiikubali watakuwa ni wenye kushindwa na wakiipinga basi wamekufuru.”

Kundi la pili: Ni wale walioko kati kwa kati; Qadariyyah wa kawaida. Hawa wamekubali elimu na uandishi. Wameenda kinyume na Salaf pale waliposema kuwa matendo ya waja wameyakadiria wenyewe na ni yenye kujitokeza kutoka kwao kwa njia ya upekee. Kwa msemo mwingine wanachotaka kusema ni kuwa matendo ya waja hakuyataka Allaah na wala hakuyaumba na kwamba matakwa ya Allaah ni yenye kuenea isipokuwa tu matendo ya waja na kwamba aliyoumba Allaah ni yenye kuenea katika kila kitu isipokuwa tu matendo ya mja. Madhehebu haya, pamoja na kwamba ni madhehebu batili, lakini hata hivyo ni mepesi kuliko hayo ya kwanza.

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajhiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Hidaayah ar-Rabbaaniyyah fiy Sharh al-´Aqiydah at-Twahaawiyyah (01/355-357)
  • Imechapishwa: 21/05/2020