Kuna aina mbili za kuvumbua katika dini:

Ya kwanza: Uzushi wa kimaneno na wa kiimani. Ni kama mfano wa maneno ya Jahmiyyah, Mu´tazilah, Raafidhwah na mapote mengine potofu na imani zao.

Ya pili: Uzushi katika ´ibaadah. Kama kumwabudu Allaah kwa ´ibaadah ambazo hakuweka. Umegawanyika aina mbalimbali:

1- Jambo ambalo limejengeka juu ya msingi wa ´ibaadah. Kama mtu kuzusha ´ibaadah ambayo ina msingi katika dini. Mtu akazusha swalah ambayo haikuwekwa katika Shari´ah, swawm ambayo haikuwekwa katika Shari´ah au sherehe ambayo haikuwekwa katika Shari´ah kama mfano wa maulidi na nyenginezo.

2- Kitu ambacho kimezidishwa katika ´ibaadah zilizowekwa katika Shari´ah. Kwa mfano mtu akaongeza Rak´ah ya tano katika swalah ya Dhuhr au swalah ya ´Aswr.

3- Yanayokuwa katika namna ya kutekeleza ´ibaadah zilizowekwa katika Shari´ah. Mtu akazitekeleza kwa namna ambayo haikuwekwa katika Shari´ah. Kwa mfano watu wakasoma Adhkaar zilizowekwa katika Shari´ah kwa sauti ya pamoja za kuimba na mfano mwingine kuifanyia nafsi ugumu katika ´ibaadah mpaka katika kiwango kitachomtoa mtu nye ya Sunnah za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

4- Yanayokuwa kwa kutenga wakati maalum kwa ajili ya ´ibaadah zilizowekwa katika Shari´ah muda ambao haukutengwa maalum na Shari´ah. Kwa mfano watu wanatenga muda maalum kwa ajili ya nusu Sha´baan na nyusiku zake wanafunga na kusimama usiku kuswali. Msingi wa swawm na kusimama usiku ni mambo yamewekwa katika Shari´ah. Lakini hata hivyo kutenga muda maalum ni jambo linahitajia dalili.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ´Aqiydat-ut-Tawhiyd, uk. 180-181
  • Imechapishwa: 20/11/2019