Umeandika kwenye barua yako:

“Miaka kumi iliyopita nilipata khabari kuhusu mtu huyu kutoka kwa wanachuoni waheshimiwa kama Shaykh ´Abdur-Razzaaq ´Afiyfiy, Shaykh ´Abdur-Rahmaan ad-Dawsaariy, Shaykh ´Abdullaah bin Humayd, Shaykh ´Abdul-´Aziyz bin Baaz na watu mfano wao. Walitaja athari zake nzuri. Wakachunguza khabari zake… “

Mosi ni kuwa uliwauliza Mashaykh hawa kabla ya kujua hali yake.

Pili pengine kipindi hicho ni pale ambapo mtu alikuwa tu na uelewa wa kijumla juu ya ulinganizi wake. Ni kitu ambacho watu wengi wamedanganyika nacho mpaka hii leo. Hawajui mfumo huu vizuri kwa vile walikuwa hawajausoma.

Tatu walikuwa kimya kwa sababu walikuwa hawajui makosa yake. Katika hali hii mtu anatakiwa kunyamaza.

Nne makosa mengi ya mfumo wake yamejitokeza na yule aliyehifadhi ni hoja juu ya yule ambaye hakuhifadhi. Hii ni kanuni inayojulikana kwa Muhaddithuun na ni wajibu kuitendea kazi katika hali kama hii.

Tano Shaykh ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz bado yuko hai. Ni jambo lisilokuwa na shaka anajua waliyomo. Aliulizwa swali lifuatalo:

“al-Ikhwaan al-Muslimuun wameingia Saudi Arabia tangu kipindi fulani. Wamekuwa ni wenye uchangamfu kati ya wanafunzi. Unasemaje juu ya harakati hizi na ni kiasi gani imeafikiana na mfumo wa Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah?”

Akajibu:

“al-Ikhwaan al-Muslimuun wamekosolewa na wanachuoni wakubwa kwa kuwa hawatilii umuhimu kulingania katika Tawhiyd na kukemea shirki na Bid´ah. Wana njia maalum ambazo nafasi zake zinafanya kutolingania kwa Allaah na ´Aqiydah sahihi walionayo Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah. al-Ikhwaan al-Muslimuun wanatakiwa kutilia umuhimu wa kulingania kwa mujibu wa ulinganizi wa Salafiyyah na kulingania kwa Allaah na kukataza kuyaabudia makaburi, kuwategemea wafu, kuwataka msaada wafu kama al-Husayan, al-Badawiy au wengine. Hili ndio linalotakikana kufikisha.”[1]

Ndugu muislamu mpendwa! Umesikia alivojibu Shaykh ´Abdul-´Aziyz bin Baaz? Ni kwa nini husemi aliyosema kuhusu ulinganizi wa al-Ikhwaan al-Muslimuun na yale yanayoenda kinyume na mfumo wa Salaf?

Ama kuhusu Mashaykh wengine uliyowataja mbali na Shaykh ´Abdul-´Aziyz, basi wamedanganyika kama wewe ikiwa kama ni kweli wametaja athari zake nzuri. Lakini yanayodhihiri katika maneno yako ni kwamba wewe ni mwenye kukinaika juu ya kwamba alikuwa na athari nzuri. Ndio maana nina maswali kadhaa ya kukuuliza ambayo nilikuwa nataka unijibu kwa haki na kwa uwazi:

1- Je, ni katika athari zake nzuri kunyamazia kwake shirki ambayo ilikuwa inafanywa na watu kwenye makaburi Misri pasi na kukataza hilo?

2- Je, ni katika athari zake nzuri kuasisi kwake chama ambacho amekiacha baada yake kikatenganisha Ummah?

3- Je, ni katika athari zake nzuri kuita katika ukhaliyfah badala ya Tawhiyd iliyolinganiwa na Mitume?

4- Je, ni katika athari zake nzuri kuwafanya watu wakawachukia watawala na wanachuoni kuzipindua nchi zilizoko sasa ili, kama wanavodai, waanzishe ukhaliyfah?

5- Je, ni katika athari zake nzuri kupekua kasoro za watawala na wanachuoni, jambo ambalo linafanywa na wafuasi wake, na kudai ya kwamba hawastahiki kuwa na uongozi na kwamba wanachuoni ni wenye kuwapaka tu mafuta?

6- Je, ni katika athari zake nzuri kuwadanganya watu na kuwaacha wakalingania katika Uislamu ilihali ni wajinga?

7- Je, ni katika athari zake nzuri kujiwajibishia yeye mwenyewe kiapo cha utiifu na kuwaacha watawala?

8- Je, ni katika athari zake nzuri kuhamasisha Shiy´ah na Ahl-us-Sunnah kuwa na ukaribu? Hii ina maana ya kila kundi liache baadhi ya I´tiqaad zake ili kati yao wawe na ukaribu.

9- Je, ni katika athari zake nzuri kudai kwake ya kwamba Salaf walikuwa hawajui ni nini maana ya sifa zote za Allaah?

10- Je, ni katika athari zake nzuri kusema kuwa hakuna uadui wowote wa kidini kati yetu sisi na mayahudi? Hii ina maana ya kwamba mayahudi ni ndugu zetu.

11- Je, ni katika athari zake nzuri kusema kwamba twashirikiana katika yale tunayoafikiana na kupeana udhuru kati yetu kwa yale tunayotofautiana? Hii ina maana ya kuacha kuamrisha mema na kukataza maovu ambako Allaah amewasifu kwa ajili yake waumini na kuwatapa kwalo:

كُنتُمْ خَيْرَ أُمَّةٍ أُخْرِجَتْ لِلنَّاسِ تَأْمُرُونَ بِالْمَعْرُوفِ وَتَنْهَوْنَ عَنِ الْمُنكَرِ وَتُؤْمِنُونَ بِاللّهِ

“Mmekuwa Ummah bora kabisa uliotolewa kwa watu: mnaamrisha mema na mnakataza maovu na mnamwamini Allaah.”[2]

12- Je, ni katika athari zake nzuri kukusanya I´tiqaad zote kama Ahl-us-Sunnah, Shiy´ah, Suufiyyah, Jahmiyyah, Mu´tazilah na nyengnezo na kudai ya kwamba wote ni ndugu kwa sababu wote wanashuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah ijapo watakuwa na mambo yanayovunja shahaadah hii?

13- Je, ni katika athari zake nzuri kuhuisha Bid´ah kama ya Maulidi na mfano wake?

14- Je, ni katika athari zake nzuri kusema kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anahudhuria sherehe zao na kuwabariki na kuwasamehe madhambi yao?

15- Je, ni katika athari zake nzuri alivokuwa amekolea katika Suufiyyah, kuipenda na kuwaunga kwake mkono?

16- Je, ni katika athari zake nzuri kuufupiza Uislamu katika nukta ishirini na kufanya hayo ni Shari´ah kwa wafuasi wake?

17- Je, ni katika athari zake nzuri kufanya bay´ah kuwa na sharti kumi yanayokosa msingi katika Kitabu cha Allaah na Sunnah za Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)?

18- Je, ni katika athari zake nzuri pindi alipofanya utiifu kuwa ni moja katika sharti na kusema:

“Ninachokusudia kwa utiifu ni kujisalimisha na maamrisho na kuyatekeleza kwa khiyari katika kipindi kizito na chepesi. Hilo ni kwa sababu ngazi za Da´wah hii ni tatu… Ngazi ya pili ni ya malezi. Hapa ndipo kulipo muundo wa Da´wah kutokana na Suufiyyah iliosafi inapokuja katika kiroho na kijeshi inapokuja katika kuitendea kazi.”?[3]

Pamoja na kwamba ni wajibu kumsikiliza na kumtii mtawala pale kunapotimizwa masharti mawili:

  1. Kitendo kiwe kinajuzu. Hakuna utiifu katika kumuasi Allaah.
  2. Mja awe anaweza kitendo hicho.

19- Je, ni katika athari zake nzuri kuhudhuria kaburi la Zaynab katika mnasaba wa mwaka mpya wa Kiislamu bila ya kutaja shirki hata moja iliyopo hapo? Bali uhakika wa mambo ni kwamba alikuwa akiwaamrisha wahudhuriaji kujisafisha wao wenyewe na nafsi zao kutokamana na chuki na nia mbaya.

20- Je, ni katika athari zake nzuri kuwaacha manaswara wa Misri kuingia katika shirika lake na kuinusuru Da´wah yake? Kuna yeyote katika wanaolingania katika dini ya Allaah alofanya kitu kama hicho?

21- Je, ni katika athari zake nzuri kufanya sherehe kwa ajili ya Muhammad ´Uthmaan al-Marghaniy ambaye alikuwa anajulikana kuamini Wahdat-ul-Wujuud? Amemsifu na kusema katika sherehe hiyo:

“Sisi, al-Ikhwaan, tuna mapenzi masafi na heshima kubwa kwa kiongozi Marghaniyyah.”

22- Je, ni katika athari zake nzuri kwenda katika sherehe ya usiku tarehe moja Rabiy´-ul-Awwaal na kubaki huko mpaka tarehe kumi na mbili na kuimba kwa nyimbo zilizo na shirki kubwa:

“Ee Allaah, swalia nuru (yaani Mtume) Ulioifanya kuja kwa walimwengu na inayoangazia kwa jua na mwezi. Mpenzi huyu (yaani Mtume) amehudhuria pamoja na wapenzi wake na amemsamehe kila mmoja kwa yaliyopitika.”?

23- Je, ni katika athari zake nzuri kutembea kwake masaa matatu kwenda na kurudi kutembelea makaburi ya makuhani kutoka Hasswaafiyyah na Shaadhiliyyah? Endapo kuna ambaye atasema kuwa matembezi yake yalikuwa ya ki-Sunnah, hivyo nitasema kuwa haijuzu kuyafungia safari makaburi.

24- Je, ni katika athari zake nzuri kuimba nyimbo zilizo na Wahdat-ul-Wujuud waziwazi:

“Ee Allaah! Sema na uache uwepo na yale yaliyomo. Ikiwa umeelewa, basi utaona kuwa hakuna aliyepo isipokuwa Allaah, si maalum wala jumla.”?

25- Je, ni katika athari zake nzuri kuonelea kuwa kufanya Tawassul kupitia jaha ya watu wema, ambayo ndio moja ya sababu kubwa ya shirki, ni jambo dogo tu ambalo halitakiwi kutiliwa umuhimu kiasi hicho?

Ee Shaykh! Nakuuliza kama mambo haya yanaafikiana na dini au hapana?

Heshima ya Hasan al-Bannaa ina umuhimu mkubwa wa kulindwa kuliko dini?

Mtu mwenye kuwabainishia watu haki na kutetea ´Aqiydah anazingatiwa kuwa ni mkoseaji na aliyefanya tendo na jinai? Anastahiki kukatazwa na kulaumiwa na kutoshauriwa kuchapisha kitabu?

[1] al-Majallah/ash-Shaykh Ibn Baaz: Lastu muta´asswiban…

[2] 03:110

[3] Majmuu´-ur-Rasaa-il/at-Ta´aaliym, uk. 268

  • Mhusika: ´Allaamah Ahmad bin Yahyaa an-Najmiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Radd-ul-Jawaab, uk. 15-22
  • Imechapishwa: 05/07/2020