Unasema kwenye barua yako:

“Usichapishe kitabu hiki ambacho kitakuja kukupa tetesi mbaya na kukufanya kusema vibaya heshima ya ndugu yako muislamu.”

Mosi nazingatia kuwa unawazuia watu na njia ya Allaah kwa kufanya hivi. Kwa sababu naona kuwa kitabu hiki ni miongoni mwa vitabu vyangu bora kabisa. Humo nimeinusuru haki na kuitetea Tawhiyd na ´Aqiydah ya Kiislamu. Nataraji nimefanya hivo hali ya kuwa ni mwenye kumtakasia nia Allaah na nimetekeleza haki Yake na kuitetea dini Yake. Hata hivyo sisemi kuwa mimi sina mapungufu na makosa.

Pili ninaonelea kuwa kwa kufanya hivi unaikosesha nusura haki na kuwanusuru na kuwasaidia watu wa batili. Inatosheleza kule tu kutangamana vibaya na dini na kuwadhalilisha watu wake. Allaah amesema juu ya watu hawa:

وَمَنْ أَحْسَنُ قَوْلًا مِّمَّن دَعَا إِلَى اللَّهِ وَعَمِلَ صَالِحًا وَقَالَ إِنَّنِي مِنَ الْمُسْلِمِينَ

“Na nani mwenye kauli nzuri zaidi kuliko yule anayelingania watu kwa Allaah na akatenda mema na akasema: “Hakika mimi ni miongoni mwa waislamu?”[1]

Tatu nimesikia kuwa baadhi ya Hizbiyyuun hununua kiwango kikubwa cha vitabu ambavyo vimetahadharisha mfumo wao kisha wanavichoma moto. Kuna tofauti gani kati ya kuchoma kitabu baada ya kuwa kimeshachapishwa na kunasihi kisichapishwe?

Nne ninaonelea kuwa unajiingiza kwenye jambo lisilokuhusu ili kuzuia kheri. Hadiyth tukufu inasema:

“Miongoni mwa uzuri wa Uislamu wa mtu ni kuacha yale yasiyomuhusu.”

Tano kitabu kitachapishwa na kuenezwa ili kuthibitisha Tawhiyd na kukataza shirki, kuthibitisha Sunnah na kukataza Bid´ah, kuthibitisha haki na kukataza batili. Lililo la wajibu kwako badala yake unatakiwa kuharakisha kukichapa ili kuinusuru Tawhiyd, Sunnah na haki. Pamoja na hivyo umefanya kinyume kabisa na kuomba kisichapishwe. Kwa hivyo umewanusuru kidhuluma Ahl-ul-Bid´ah na Hizbiyyah dhidi ya Ahl-ut-Tawhiyd was-Sunnah na wale wenye kuwafuata Salaf. Hivyo basi mtake Allaah msamaha na utubu Kwake kabla haijachelewa. Hatokufaa fulani wala fulani. Kitachokufaa ni kusimama kuisimamia haki na kuinusuru na watu wake.

Kuhusiana na kwamba unachelea kikichapishwa kukaenezwa tetesi mbaya juu yangu, basi utambue kuwa tetesi mbaya inakuwa kwa kuinusuru batili, kuizungumza au kuitendea kazi. Namshukuru Allaah kuona sikufanya makosa wala sikuwanusuru watu wa batili mpaka tetesi mbaya iweze kuenea kwa waumini ambao ndio mashahidi wa Allaah juu ya ardhi. Pamoja na hivyo nimetenda haki na kuinusuru haki na ninataraji thawabu kutoka kwa Allaah kwa hilo. Ama kuhusu watu wa batili, sijali watavyoonelea.

Ninamuomba Allaah mtukufu, Mola wa ´Arshi kubwa, anikinge na shari zao na alinde na vitimbi vyao. Nitachapisha kitabu na kukieneza – Allaah akitaka – na ninamtegemea Allaah ambaye Yeye ndiye aliye na usimamizi kwa walimwengu wote.

Swalah na salamu zimwendee Mtume wetu Muhammad, kizazi zake na Maswahabah zake.

Ahmad bin Yahyaa Muhammad Shubayr an-Najmiy

[1] 41:33

  • Mhusika: ´Allaamah Ahmad bin Yahyaa an-Najmiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Radd-ul-Jawaab, uk. 34-36
  • Imechapishwa: 05/07/2020