Swali: Ahl-ul-Kitaab ni wepi?

Jibu: Ahl-ul-Kitaab, ni kama ambavo Allaah amebainisha ndani ya Qur-aan, ni mayahudi na wakristo. Wameitwa “Ahl-ul-Kitaab” kwa sababu Allaah amewateremshia Vitabu viwili juu ya wana wa israaiyl. Kitabu cha kwanza juu ya Muusa, ambacho ni Tawraat. Kitabu cha pili juu ya ´Iysaa, ambayo ni Injiyl. Ndio maana wakaitwa Ahl-ul-Kitaab, wanaitwa pia “Ahl-ul-Kitaabayn”. Wana hukumu ambazo ni maalum kwao ambazo zinatofautiana na washirikina wengine. Wanashirikiana na makafiri wengine katika jina “makafiri” na “washirkina.” Wao ni makafiri na washirikina kama waabudia makaburi, waabudia nyota na makafiri wengineo. Lakini wana hukumu maalum kwa sababu walipokea Vitabu viwili kupitia Mitume wao waliotangulia ambao ni Muusa na Haarun na ´Iysaa (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam). Ndipo Allaah akawafanyia hukumu maalum. Miongoni mwa hukumu hizo ni kuhalalika vichinjwa vyao ambavyo havikuchinjwa kwa ajili ya mwengine asiyekuwa Allaah, havikutajiwa jina la mwengine asiyekuwa Allaah na hakukupatikana ndani yake kitu kinachovifanya kuwa haramu. Vichinjwa hivi ni halali kwetu. Allaah (Subhaanah) amesema:

وَطَعَامُ الَّذِينَ أُوتُوا الْكِتَابَ حِلٌّ لَّكُمْ وَطَعَامُكُمْ حِلٌّ لَّهُمْ

“… na chakula cha wale Ahl-ul-Kitaab ni halali kwenu.”[1]

Vivyo hivyo wanawake wao ni halali wetu. Inahusiana na wale wanawake wenye kujiheshimu wenye kujichunga na machafu ambao ni waungwana. Amesema (Subhaanah):

وَالْمُحْصَنَاتُ مِنَ الْمُؤْمِنَاتِ وَالْمُحْصَنَاتُ مِنَ الَّذِينَ أُوتُوا الْكِتَابَ مِن قَبْلِكُمْ

“… na wanawake wenye kujichunga na machafu [wasiozini] miongoni mwa Ahl-ul-Kitaab kabla yenu.”[2]

Hukumu hizi mbili ni maalum kwa Ahl-ul-Kitaab: wale wanawake wao wenye kujiheshimu ni halali na vile vichinjwa ambavyo havikuchinjwa kwa ajili ya mwingine asiyekuwa Allaah na kadhalika havikuchinjwa kinyume na Shari´ah ya Allaah. Washirkina wengine wanawake wao si halali wala vichinjwa vyao.

[1] 05:05

[2] 05:05

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/7598/%D8%A7%D9%87%D9%84-%D8%A7%D9%84%D9%83%D8%AA%D8%A7%D8%A8-%D9%88%D8%AD%D9%83%D9%85%D9%87%D9%85
  • Imechapishwa: 16/01/2020