2570 – Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Unapovaa viatu vyako, basi anza na upande wa kulia, na pindi unapovivua, basi anza na upande wa kushoto. Fanya upande wa kulia ndio wa kwanza unaouvisha na upande wa kushoto ndio wa mwisho unaovua. Usitembee kwa kiatu kimoja. Ima vivue vyote viwili au vivae vyote viwili.”

Ameipokea Abu ´Amr bin Mandah katika ”al-Muntakhab min al-Fawaa-id”[1] kupitia kwa ´Utbaan bin Bashiyr, kutoka kwa Khuswayf, kutoka kwa Muhammad bin ´Ajlaan. ´Utbaan amesema: Baada ya hapo nilikutana na Muhammad bin ´Ajlaan ambaye alinihadithia kutoka kwa Abuz-Zinaad, kutoka kwa al-A´raj, kutoka kwa Abu Hurayrah, kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Cheni ya wapokezi hii ni nzuri kupitia njia zinazoitolea ushahidi.

´Utbaan bin Bashiyr na Muhammad bin ´Ajlaan ni waaminifu. Hifdhi zao zina kitu katika udhaifu, lakini Hadiyth zao angalau ni nzuri – Allaah akitaka.

Hadiyth imepokelewa kupitia njia nyingine. Ahmad amesema: ”Sufyaan ametuhadithia, kutoka kwa Abuz-Zinaad…[2]

Cheni ya wapokezi ni Swahiyh na ni kwa mujibu wa masharti ya al-Bukhaariy na Muslim.

Maalik amepokea mfano wake kupitia kwa Abuz-Zinaad[3].

Tambua kwamba Hadiyth hii imetaja adabu ya viatu na inatofautisha kati ya kile cha kwanza kinachovaliwa na kinachovuliwa. Waislamu wengi hii leo wameghafilika na jambo hili kwa sababu ya ujinga mwingi juu ya Sunnah na uchache wa watu wanaowalea juu yake. Miongoni mwao kunaingia vilevile wale wanaodai kwamba ni walinganizi wanaolingania katika Uislamu. Bali miongoni mwao kuko wale ambao wanasema kuhusu adabu hii kwamba ni katika mambo madogomadogo na yasiyokuwa na maana yoyote. Enyi waislamu! Msidanganyike nao. Ninaapa kwa Allaah kwamba ni wajinga juu ya Uislamu. Ni wenye chuki na uadui dhidi ya Uislamu sawa ikiwa watalijua hilo au hawalijui. Hapo kabla ilizoeleka kusemwa kwamba yule mwenye kulijahili jambo basi hulifanyia uadui.

Miongoni mwa mambo ya ajabu ni kwamba siku zote wanasema katika Khutbah na mihadhara yao kwamba ni lazima kuwa na Uislamu mzimamzima kisha wao ndio wa kwanza wanaokanusha yale wanayolingania kwayo. Mambo hayo yanaonekana katika matendo na mavazi yao. Utawaona wengi wao hawatilii umuhimu mavazi ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Badala yake ni wenye kujifananisha na al-Hasan al-Bannaa na mfano wake: ndevu zao ni fupi na tai. Baadhi yao wako na ndevu kwa mujibu wa ule msemo wa wajinga katika baadhi ya miji:

“Ndevu bora ni zile za kuashiria tu.”

Aidha wanavaa mavazi ya wanachuoni kilemba na juba ambalo pengine likawa refu kama mavazi ya wanawake.

[1] 2/265.

[2] al-Musnad (2/245).

[3] al-Muwattwa’ (3/105).

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Silsilat-ul-Ahaadiyth as-Swahiyhah (6/1/144-145)
  • Imechapishwa: 22/06/2019