Abu ´Ubaydah bin al-Jarraah


´Aamir bin ´Abdillaah bin al-Jarraah bin Hilaal bin Uhayb bin Dhayyah bin al-Haarith bin Fihr bin Maalik bin an-Nadhwr bin Kinaanah bin Khuzaymah bin Mudrikah bin Ilyaas bin Mudhwr bin Nizaar bin Ma´d bin ´Adnaan al-Qurashiy al-Fihriy al-Makkiy.

Ni mmoja katika wale waislamu waliotangulia wa mwanzo. Abu Bakr alikuwa anataka achukue ukhaliyfah baada ya kufa kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na akamteua siku ya Saqiyfah. Yeye na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wanakutana katika ukoo kwa Fihr. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimshuhudilia Pepo na akamwita kuwa “mwaminifu wa Ummah”. Fadhilah zake zinatambulika na ni nyingi.

Amepokea Hadiyth zenye kuhesabika na ameshiriki vita vingi.

Baadhi ya waliohadithia kutoka kwake ni pamoja na al-´Irbaadhw bin Saariyah, Jaabir bin ´Abdillaah, Abu Umaamah al-Baahiliy, Samurah bin Jundab, Aslam, huria wa ´Umar, ´Abdur-Rahmaan bin Ghanm na wengineo.

Anayo katika Hadiyth moja katika “as-Swahiyh” ya Muslim, moja katika “al-Jaamiy´” ya at-Tirmidhiy na kumi na tano katika “al-Musnad” ya Baqiyy bin Makhlad.

Maalik bin Yakhaamir alimweleza Abu ´Ubaydah akasema:

“Alikuwa ni mwanamme mwembamba na uso wenye bashasha. Alikuwa na ndevu khafifu. Alikuwa ni mwenye kuinama kwa mbele na yamevunjwa meno yake ya mbele.”

Zayd bin Ruumaan amesema:

“Ibn Madh´uun, ´Ubaydah bin al-Haarith, ´Abdur-Rahmân bin ´Awf, Abu Salamah bin ´Abdil-Asad na Abu ´Ubaydah bin al-Jarraah waliondoka wakaenda kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Akawadhihirishia Uislamu na wakasilimu papohapo.”

Abu ´Ubaydah alishiriki vita vya Badr na akamuua baba yake. Katika vita vya Badr alifikia nafasi nzuri. Siku hiyo aliondosha vipande viwili vya chumba vilivyokuwa vimeingia kwenye kofia ya kinga ya Mtume wa Allaah wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa meno yake ya mbele. Hivyo yakatoka meno yake. Pamoja na hivyo mapengu yake yakawa mazuri. Mpaka ikasemwa kwamba hajawahi mtu kuwa na pengu kati ya meno yake ya mbele zuri kama pengu la Abu ´Ubaydah.

Abu Bakr as-Swiddiyq alisema wakati wa kufariki kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Nimeridhia kukuteulieni wanamme hawa wawili kama wagombea wenu: ´Umar na Abu ´Ubaydah.”

az-Zubayr bin Bakkaar amesema:

“Kimekwisha kizazi cha Abu ´Ubaydah na watoto  wote wa ndugu zake.”

Ibn Ishaaq na al-Waaqidiy wamesema kwamba alikuwa miongoni mwa wale waliohajiri kwenda Uhabeshi.

Kama kweli alihajiri kwenda huko, basi hakukaa kwa muda mrefu.

Abu ´Ubaydah alikuwa miongoni mwa wale waliokusanya Qur-aan Tukufu.

Imethibiti kutoka njia nyingi kwamba Anas amemsikia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema:

“Hakika kila Ummah una mtu mwaminifu na mwaminifu wa Ummah huu ni Abu ´Ubaydah.”[1]

´Abdullaah amesema:

“Nilimuuliza ´Aaishah: “Ni mtu gani Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akimpenda zaidi?” Akasema: “Abu Bakr, kisha ´Umar halafu Abu ´Ubaydah bin al-Jarraah.”[2]

Khaliyfah bin Khayyaat amesema:

“Abu Bakr alimfanya Abu ´Ubaydah kusimamia hazina ya mali.”

Bi maana mali ya waislamu, kwa sababu kipindi hicho hakukuwepo hazina ya mali. Mtu wa kwanza aliyefanya hazina ya mali alikuwa ´Umar.

Ibn-ul-Mubaarak amepokea katika “Kitaab-ul-Jihaad” kutoka kwa Hishaam bin Sa´d, kutoka kwa Zayd bin Aslam, kutoka kwa baba yake ambaye amesema:

“´Umar alipata khabari kwamba Abu ´Ubaydah amezingirwa Shaam na adui. Akamwandikia:

“Amma ba´d: Kamwe muumini hafikwi na shida yoyote, isipokuwa Allaah hujaalia baada yake faraja. Katu ugumu haushindi wepesi mbili:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اصْبِرُوا وَصَابِرُوا وَرَابِطُوا

“Enyi mlioamini! Subirini na zidini kuvuta subira na bakieni imara.”[3]

Ndipo Abu ´Ubaydah akamwandikia akimjibu:

“Amma ba´d: Hakika Allaah anasema:

أَنَّمَا الْحَيَاةُ الدُّنْيَا لَعِبٌ وَلَهْوٌ وَزِينَةٌ وَتَفَاخُرٌ بَيْنَكُمْ وَتَكَاثُرٌ فِي الْأَمْوَالِ وَالْأَوْلَادِ ۖ كَمَثَلِ غَيْثٍ أَعْجَبَ الْكُفَّارَ نَبَاتُهُ ثُمَّ يَهِيجُ فَتَرَاهُ مُصْفَرًّا ثُمَّ يَكُونُ حُطَامًا ۖ وَفِي الْآخِرَةِ عَذَابٌ شَدِيدٌ وَمَغْفِرَةٌ مِّنَ اللَّـهِ وَرِضْوَانٌ ۚ وَمَا الْحَيَاةُ الدُّنْيَا إِلَّا مَتَاعُ الْغُرُورِ

“Maisha ya dunia ni mchezo na pumbao na mapambo na kufakharishana kati yenu na kushindana kukithiri katika mali na watoto; ni kama mfano wa mvua inayowafurahisha wakulima mimea yake, kisha yananyweya, basi utayaona yamepiga manjano, halafu yanakuwa mabua yaliyonyauka na kupondekapondeka.  Na Aakhirah kuna adhabu kali na msamaha kutoka kwa Allaah na radhi. Na maisha ya dunia si chochote isipokuwa ni sterehe fupi za kughuri.”[4]

´Umar akatoka na barua yake, akaisoma juu ya mimbari na akasema:

“Enyi watu wa al-Madiynah! Pateni kiu juu ya Jihaad.”

Maalik amesema:

“´Umar alimwagizia Abu ´Ubaydah dinari 4000 au 400 na akamwambia mjumbe wake: “Tazama atazifanyisha nini.” Akasema: “Akazigawanya.” Kisha akamwagizia Mu´aadh bin Jabal. Mjumbe anasema: “Yeye pia akazigawanya isipokuwa kitu kidogo tu ambacho mke wake alimwambia kuwa wanakihitaji.” Wakati mjumbe alimletea khabari ´Umar akasema: “Himdi zote ni stahiki ya Allaah ambaye amefanya kuwepo waislamu wenye kufanya mambo kama haya.”

Abu ´Ubaydah amesema:

“Natamani laiti ningekuwa kondoo ambapo nikachinjwa, ikaliwa nyama yangu na ukanywewa mchuzi wangu.”

´Imraan bin Huswayn amesema:

“Natamani ningekuwa majivu yanayopelekwa na upepo.”

Twaariq amesema:

“Wakati tauni ilipoenea, ´Umar alimwandikia Abu ´Ubaydah: “Nahitaji kitu ambacho siwezi kukipata isipokuwa kutoka kwako. Haraka sana kuja kwangu.” Ndipo Abu ´Ubaydah akasema: “Najua anachohitajia kiongozi wa waumini. Anataka abaki yule ambaye si mwenye kubaki.” Akamwandikia akijimbu: “Nimekwishaijua haja yako. Naomba nibaki. Mimi niko pamoja na wanajeshi wa waislamu na sipendi kuwaacha.” Wakati ´Umar aliposoma ile barua akalia. Akaambiwa: “Abu ´Ubaydah amekufa?” Akasema: “Hapana, lakini ni kama yeye ndiye amefanya hivo.”[5]

Baadaye Abu ´Ubaydah akafariki na tauni ikapotea.

Muhammad bin ´Umar al-Marwaziy amesema:

“Wamesema kuwa Abu ´Ubaydah alikuwa kati ya wanajeshi 30000. Hakukubaki isipokuwa 6000.”

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimfanya Abu ´Ubaydah kuwa kiongozi wa vita mara nyingi. Miongoni mwazo ni ile mara ambayo maaskari wake walishikwa na njaa. Bahari ikamtema nyangumi nchikavu ambaye tayari kishakufa. Abu ´Ubaydah akasema: “Mzoga. Kisha akasema: “Hapana. Sisi ni wajumbe wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na tunapambana katika njia ya Allaah. Mleni!”

Hadiyth hii imetajwa katika al-Bukhaariy na Muslim[6].

Abu Hafsw al-Fallaas amesema:

“Abu ´Ubaydah alifariki mwaka wa 18. Aliishi miaka 58.”

[1] Ahmad (3/133), al-Bukhaariy (3744), Muslim (2419) na wengineo.

[2] at-Tirmidhiy (3657), Ibn Maajah (102), al-Haakim (3/73) na wengineo. al-Haakim ameisahihisha na adh-Dhahabiy akaafikiana naye.

[3] 03:200

[4] 57:20

[5] al-Haakim (3/263) na al-Humaydiy. adh-Dhahabiy amesema:

”Ni yenye kuafikiana na sharti za al-Bukhaariy na Muslim.”

[6] al-Bukhaariy (2483) och Muslim (1935).

  • Mhusika: Imaam Shams-ud-Diyn Muhammad bin Ahmad adh-Dhahabiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Siyar A´laam-in-Nubalaa' (1/5-23)
  • Imechapishwa: 13/01/2021