99. Nguzo ya kumwamini Allaah na Malaika


Nguzo zake ni sita – Bi maana nguzo zake ambazo Uislamu umesimama juu yake na unaharibika kwa kukosekana moja katika nguzo hizo. Nguzo zenyewe ni zifuatazo:

1- Kumwamini Allaah: Nguzo ya kwanza ni kumwamini Allaah. Ndani yake kunaingia vigawanyo vitatu vya Tawhiyd. Kuamini kwamba Allaah ni Mmoja wa pekee na Mwenye kuhitajiwa juu ya kila jambo. Hana mshirika katika uola Wake, katika uungu Wake, katika majina na sifa Zake.

2- Kuamini Malaika: Malaika ni viumbe wa Allaah katika ulimwengu wa ghaibu. Allaah amewaumba ili wamwabudu Yeye na ili watekeleze maamrisho Yake juu ya ufalme Wake. Wamegawanyika sampuli mbalimbali. Kila sampuli ina kazi yake waliyopewa na wanayosimama nayo. Hawamwasi Allaah kwa yale aliyowaamrisha na wanatekeleza yale waliyoamrishwa. Miongoni mwao wako waliopewa kazi ya Wahy ambaye ni Jibriyl (´alayhis-Salaam). Naye ndiye Malaika mtukufu zaidi. Naye ndiye roho mwaminifu na mwenye nguvu madhubuti kwelikweli. Miongoni mwao wako ambao wamepewa kazi ya kubeba ´Arshi:

الَّذِينَ يَحْمِلُونَ الْعَرْشَ وَمَنْ حَوْلَهُ

“Ambao wanabeba ‘Arshi na walio pembezoni mwake.”[1]

وَالْمَلَكُ عَلَىٰ أَرْجَائِهَا ۚ وَيَحْمِلُ عَرْشَ رَبِّكَ فَوْقَهُمْ يَوْمَئِذٍ ثَمَانِيَةٌ

”Malaika watakuwa kandoni mwake na watabeba ‘Arshi ya Mola wako juu yao siku hiyo [Malaika] wanane.”[2]

´Arshi ndio kiumbe kikubwa zaidi. Hakuna anayejua ukubwa wake isipokuwa Allaah (´Azza wa Jall). Inabebwa na Malaika. Hii ni dalili inayoonyesha ukubwa wa Malaika na ukubwa wa nguvu zao na umbile lao. Amesema (Ta´ala):

الْحَمْدُ لِلَّـهِ فَاطِرِ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ جَاعِلِ الْمَلَائِكَةِ رُسُلًا أُولِي أَجْنِحَةٍ مَّثْنَىٰ وَثُلَاثَ وَرُبَاعَ ۚ يَزِيدُ فِي الْخَلْقِ مَا يَشَاءُ

“Himdi zote njema anastahiki Allaah, mwanzilishi wa mbingu na ardhi, Mwenye kuwafanya Malaika kuwa wajumbe wenye mbawa mbilimbili na tatutatu na nnenne – huzidisha katika uumbaji atakavyo.”[3]

Miongoni mwao wako wenye mbawa miasita kama mfano wa Jibriyl (´alayhis-Salaam). Hakuna anayejua ukubwa wa umbile lake isipokuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala):

بَلْ عِبَادٌ مُّكْرَمُونَ لَا يَسْبِقُونَهُ بِالْقَوْلِ وَهُم بِأَمْرِهِ يَعْمَلُونَ

“Bali ni waja waliokirimiwa. Hawamtangulii kwa kauli nao kwa amri Yake wanafanya.”[4]

Miongoni mwao wako ambao wamepewa kazi ya mazao na mimea ambaye ni Mikaaiyl.

Miongoni mwao wako ambao wamepewa kazi ya kupuliza kwenye baragumu ambaye ni Israafiyl. Atapuliza kwenye baragumu na kitakufa kila kitu. Amesema (Ta´ala):

وَنُفِخَ فِي الصُّورِ فَصَعِقَ مَن فِي السَّمَاوَاتِ وَمَن فِي الْأَرْضِ إِلَّا مَن شَاءَ اللَّـهُ

“Itapulizwa katika baragumu, basi watazimia wale walioko mbinguni na ardhini isipokuwa amtakaye Allaah.”

Kisha atapuliza mara ya pili na roho zitaruka kuingia kwenye viwiliwili vyake:

ثُمَّ نُفِخَ فِيهِ أُخْرَىٰ فَإِذَا هُمْ قِيَامٌ يَنظُرُونَ

“Kisha litapulizwa humo jengine, tahamaki hao wanasimama wakitazama.”[5]

Roho zitaruka kutoka kwenye bagarumu na ziingie ndani ya viwiliwili ambapo wapate uhai kwa idhini ya Allaah. Baada ya hapo waandamane kwenda katika uwanja.

Miongoni mwao wako ambao wamepewa kazi ya kuzitoa roho pindi unapoisha muda wa mtu kuishi. Naye ni Malaika wa mauti. Amesema (Ta´ala):

قُلْ يَتَوَفَّاكُم مَّلَكُ الْمَوْتِ الَّذِي وُكِّلَ بِكُمْ ثُمَّ إِلَىٰ رَبِّكُمْ تُرْجَعُونَ

“Sema: “Atakufisheni Malaika wa mauti ambaye amewakilishwa kwenu, kisha kwa Mola wenu mtarejeshwa.”[6]

Anakuwa na wasaidizi wake katika Malaika:

تَوَفَّتْهُ رُسُلُنَا وَهُمْ لَا يُفَرِّطُونَ

“Wajumbe Wetu humfisha, nao hawazembei.”[7]

Bi maana wasaidizi wake katika Malaika.

Miongoni mwao wako ambao wamepewa kazi ya watoto ndani ya matumbo ya mama zao. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakika kila mmoja wenu linakusanywa umbile lake tumboni mwa mama yake kwa masiku arubaini. Kisha inakuwa kipande cha damu kwa muda kama huo. Halafu inakuwa kinofu cha nyama kwa muda kama huo. Halafu anatumiwa Malaika kumpulizia roho… “[8]

Miongoni mwao wako ambao kazi yao ni kuhifadhi matendo ya mwanadamu. Amesema (Ta´ala):

وَإِنَّ عَلَيْكُمْ لَحَافِظِينَ كِرَامًا كَاتِبِينَ

“Na hakika juu yenu bila shaka kuna wenye kuhifadhi; watukufu wenye kuandika.”[9]

 Wanalazimiana nanyi mchana na usiku. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Wanapishana kwenu Malaika wa usiku na Malaika wa mchana.”[10]

Wanakusanyika katika swalah ya Fajr na swalah ya ´Aswr. Wanawatolea ushahidi mbele Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala):

إِنَّ قُرْآنَ الْفَجْرِ كَانَ مَشْهُودًا

“Kwani hakika swalah ya alfajiri ni yenye kushuhudiwa.”[11]

Bi maana inahudhuriwa na Malaika. Ni wale Malaika wa usiku na mchana.

Miongoni mwao wako ambao wamepewa kazi ya kumuhifadhi mwanadamu kutokamana na yale yenye kuchukiza, majanga, maadui, wanyama wakali na nyoka. Muda wa kuwa bado anao muda wa kuishi basi anakuwa na Malaika wanaomuhifadhi kutokamana na khatari. Analala katikati ya wanyama wakali na nyoka nchikavu. Ni nani anayemlinda kutokamana na nyoka na wanyama wakali? Yuko pamoja naye Malaika ambao amewepesishiwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Allaah (Ta´ala) amesema juu yao:

لَهُ مُعَقِّبَاتٌ مِّن بَيْنِ يَدَيْهِ وَمِنْ خَلْفِهِ يَحْفَظُونَهُ مِنْ أَمْرِ اللَّـهِ

“Ana Malaika wanaopishana kwa zamu mbele yake na nyuma yake [ambao] wanamuhifadhi kwa amri ya Allaah.”[12]

Viumbe hawa kutokana na amri ya Allaah wanamlinda mwanadamu kutokamana na mambo yenye kuchukiza na khatari mbalimbali mpaka pale utapofika muda wake. Unapofika muda wake basi wanajitenga naye mbali. Matokeo yake mtu anafikwa na yale ambayo Allaah amemkadiria kutokamana na kifo au mtihani ambao unapelekea yeye kufa.

Miongoni mwao wako Malaika ambao wamepewa kazi ya kuhakikisha zinatekelezwa amri za kwenye zoni ya mbingu na ardhini. Hakuna awajuaye isipokuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Wako Malaika ambao wanatafuta vikao anavotajwa Allaah na wanahudhuria katika vikao hivyo. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hawakusanyiki watu katika nyumba miongoni mwa nyumba za Allaah, wakikisoma Kitabu cha Allaah na wakadarasishana baina yao, isipokuwa huteremka juu yao utulivu, rehema huwafunika, Malaika huwazunguka na Allaah huwataja kwa wale walioko pamoja Naye.”[13]

Ni Malaika wanaozunguka ardhini ambao wanatafuta vikao anavyotajwa Allaah na kuvihudhuria.

Hakuna anayewajua Malaika, aina zao na sifa zao isipokuwa Allaah pekee. Lakini yaliyopokelewa katika maandiko ya Qur-aan na Hadiyth za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) tunayathibitisha na kuyaamini. Ambayo hatukutajiwa tunayanyamazia na hatuyatafiti. Kwa sababu mambo haya ni katika elimu iliyojificha ambayo hatuingii ndani yake isipokuwa kwa dalili.

[1] 40:07

[2] 69:17

[3] 35:01

[4] 21:26-27

[5] 39:68

[6] 32:11

[7] 06:61

[8] al-Bukhaariy (3208) na Muslim (2643).

[9] 82:10-11

[10] al-Bukhaariy (555) na Muslim (632).

[11] 17:78

[12] 13:11

[13] Muslim (2699).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 206-211
  • Imechapishwa: 21/01/2021