98. Du´aa ya kwanza kabla ya Tasliym

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akisoma katika swalah yake[1] du´aa mbalimbali mara akisoma hizi na mara akisoma hizi. Alimwamrisha mtu yule aliyeswali vibaya kusoma kama anataka[2]. Hizi hapa kama ifuatavyo:

1-

اللَّهُمَّ إِنِّي أَعُوذُ بِكَ مِنْ عَذَابِ الْقَبْرِ وَأَعُوذُ بِكَ مِنْ فِتْنَةِ الْمَسِيحِ الدَّجَّالِ وَأَعُوذُ بِكَ مِنْ فِتْنَةِ الْمَحْيَا وَالْمَمَاتِ اللَّهُمَّ إِنِّي أَعُوذُ بِكَ مِنَ الْمَأْثَمِ وَالْمَغْرَمِ

“Ee Allaah! Hakika mimi nakuomba ulinzi kutokamana na adhabu ya kaburi. Nakuomba ulinzi kutokamana na fitina ya al-Masiyh ad-Dajjaal. Nakuomba ulinzi kutokamana na fitina ya uhai na kifo. Ee Allaah! Nakuomba ulinzi kutokamana kutokamana na madhambi na madeni[3].”[4]

[1] Sababu ya mimi kutoandika “katika Tashahhud yake” ni kwa sababu Hadiyth inasema “katika swalah yake”. Kwa hivyo haikufupizika katika Tashahhud au sehemu nyingine. Bali ni katika sehemu zote ambazo inafaa kuomba du´aa kama katika Sujuud na Tashahhud. Maamrisho ya kuomba ndani yake yamekwishatangulia.

[2] al-Bukhaariy na Muslim. al-Athram amesema:

“Nilisema kumwambia Ahmad: “Niombe kwa kusema nini baada ya Tashahhud?” Akajibu: “Kama ilivyopokelewa.” Nikasema: “Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): “… kisha aombe anachotaka?” Akajibu: “Aombe anachotaka kutoka katika yale yaliyopokelewa.” Nikakariri swali langu ambapo akawa anajibu: “Yale yaliyopokelewa.”

Ameyanukuu Ibn Taymiyyah katika ”Majmuu´-ul-Fataawaa” (1/218/69) na akayafanya kuwa mazuri na akasema:

“Du´aa iliyotajwa kwa njia ya uhakika kunamaanishwa du´aa anayoipenda Allaah, na sio du´aa yoyote tu.”

Kisha akasema:

“Lililo bora ni kusoma du´aa zilizowekwa katika Shari´ah na zilizopendekezwa. Zile du´aa zilizopokelewa na zilizo na manufaa.”

Amepatia. Lakini maarifa ya kuzitambua du´aa zilizo na manufaa kunategemea na elimu yenye manufaa, jambo ambalo wako nalo wachache. Kwa hivyo lililo bora ni kutosheka na du´aa zilizopokelewa na khaswakhaswa ikiwa ndani yazo tayari mna yale anayoomba muombaji – na Allaah anajua zaidi.”

[3] ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesema:

“Kuna mtu alisema: “Ee Mtume wa Allaah! Ni wingi ulioje unaomba kinga dhidi ya madeni!” Akasema: “Pindi mtu anapochukua deni huzungumza akasema uongo na akaweka ahadi na asiitimize.”

[4] al-Bukhaariy na Muslim.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Swifatu Swalaat-in-Nabiy, uk. 159
  • Imechapishwa: 09/01/2019