98. Dalili zinapobaki roho za waumini baada ya kufa

Imesihi ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema kuhusu mashahidi:

“Roho zao ziko ndani ya matumbo ya kijani ya ndege. Ziko na mataa yaliyotundikwa kwenye ´Arshi. Zinaruka huku na kule Peponi zinapotaka. Halafu zinarudi kwenye kwenye lile taa.”

Katika upokezi wa Qataadah kumetajwa matamshi geni:

“Roho za waumini ziko katika umbile la ndege weupe.”

al-Qaadhwiy ´Iyaadhw amesema:

“Katika Hadiyth hii kumetajwa roho za mashahidi na katika Hadiyth ya Maalik kumetajwa roho ya Nismah na si za mashahidi. Nismah wakati fulani hutumika kwa mwanaadamu, mwili na roho, na wakati mwingine hutumika kwa roho peke yake. Ndicho kilichokusudiwa katika Hadiyth hii na Allaah ndiye anajua zaidi. Katika Hadiyth hii kuna dalili ya kukata ya kwamba kinachokusudiwa ni roho kwa kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mpaka pale Allaah anapomrudishia nayo mwilini mwake siku ya Qiyaamah.”

Hata hivyo wakati fulani inataja Nismah ya muumini na wakati mwingine inataja roho za mashahidi. Imepokelewa katika Hadiyth ya Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ya kwamba roho za waumini, mbali na za mashahidi, zinaona mahala pao asubuhi na jioni, kama ilivyotajwa juu ya watu wa Fir´awn:

النَّارُ يُعْرَضُونَ عَلَيْهَا غُدُوًّا وَعَشِيًّا ۖ وَيَوْمَ تَقُومُ السَّاعَةُ أَدْخِلُوا آلَ فِرْعَوْنَ أَشَدَّ الْعَذَابِ

“Moto unadhihirishwa kwao asubuhi na jioni, na Siku itakayosimama Saa [Malaika watasema]: “Waingizeni watu wa Fir’awn katika adhabu kali kabisa!” 40:46

al-Qaadhwiy ´Iyaadhw amesema sehemu nyingine:

“Imesemekana vilevile kuwa inahusu roho za waumini zote zinazoingia Peponi bila ya adhabu. Zinaingia Peponi kutokana na dalili ya ujumla wa Hadiyth.”

Hivi ndivyo ilivyotajwa na an-Nawawiy katika “Swahiyh Muslim”.

´Allaamah Ibn-ul-Qayyim amesema:

“Huu ni uhai wa roho na riziki yake baada ya kuwa viwiliviwili zimeshasambuka.”

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amefasiri uhai huu na kusema kuwa ni roho zao ziko ndani ya matumbo ya kijani ya ndege na zina mataa yaliyotundikwa kwenye ´Arshi. Zinaruka huku na kule Peponi zinapotaka kisha zinarudi kwenye yale matamaa. Mola wao anaziangalia na kuwaambia: “Kuna kitu mnataka?” Waseme: “Tutake nini ilihali tunaruka vizuri huku na kule Peponi tunapotaka.” Aulize hivo mara tatu. Pindi wanapoona kuwa ni lazima wanatakiwa wajibu waseme: “Tunataka uzirudishe roho zetu kwenye viwiliwili vyetu ili tuweze kuuawa kwa ajili Yako kwa mara nyingine.” Hadiyth hii imepokelewa kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kupitia njia nyingi. Baadhi ya mapokezi yanasema kuwa zinakula kwenye matunda ya Peponi.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Muhammad al-Hanbaliy al-Manbajiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tasliyatu Ahl-il-Maswaa-ib, uk. 213-214
  • Imechapishwa: 10/12/2016