98. Dalili katika Qur-aan na Sunnah kwamba imani inazidi na inapungua

Ni ipi dalili ya kuzidi na kupungua kwa imani? Kuhusu dalili ya kuzidi ni maneno Yake (Ta´ala):

إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ الَّذِينَ إِذَا ذُكِرَ اللّهُ وَجِلَتْ قُلُوبُهُمْ وَإِذَا تُلِيَتْ عَلَيْهِمْ آيَاتُهُ زَادَتْهُمْ إِيمَانًا

“Hakika si vyenginevyo waumini ni wale ambao anapotajwa Allaah nyoyo zao zinajaa khofu na wanaposomewa Aayah Zake basi huwazidishia imani.”[1]

Ni dalili ambayo imeonyesha kuwa Qur-aan inazidi kwa kusikiliza Qur-aan. Vilevile maneno Yake (Ta´ala):

وَإِذَا مَا أُنزِلَتْ سُورَةٌ فَمِنْهُم مَّن يَقُولُ أَيُّكُمْ زَادَتْهُ هَـٰذِهِ إِيمَانًا ۚ فَأَمَّا الَّذِينَ آمَنُوا فَزَادَتْهُمْ إِيمَانًا وَهُمْ يَسْتَبْشِرُونَ

“Na inapoteremshwa Suurah, basi miongoni mwao wako wanaosema: “Nani kati yenu [Suurah] hii imemzidishia imani?” Ama wale walioamini huwazidishia imani nao wanafurahia.”[2]

Ni dalili yenye kuonyesha kuwa imani inazidi kwa kuteremka kwa Qur-aan, kuisikiliza na kuizingatia. Amesema (Ta´ala):

وَمَا جَعَلْنَا أَصْحَابَ النَّارِ إِلَّا مَلَائِكَةً ۙ وَمَا جَعَلْنَا عِدَّتَهُمْ إِلَّا فِتْنَةً لِّلَّذِينَ كَفَرُوا لِيَسْتَيْقِنَ الَّذِينَ أُوتُوا الْكِتَابَ وَيَزْدَادَ الَّذِينَ آمَنُوا إِيمَانًا

“Hatukufanya walinzi wa Moto isipokuwa ni Malaika na hatukufanya idadi yao isipokuwa iwe ni jaribio kwa wale waliokufuru; ili wayakinishe wale waliopewa Kitabu na iwazidishie imani wale walioamini.”[3]

Ni dalili yenye kuonyesha kuwa imani inazidi kwa utiifu na kwa kusadikisha.

Kuhusu upunguaji kila kitu chenye kuongezeka hupungua. Kila kitu chenye kukubali kuongezeka basi hukubali vilevile kupungua. Hili ni mosi. Pili ni dalili ya maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika Hadiyth Swahiyh:

“Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) siku ya Qiyaamah atasema: “Mtoeni nje ya Moto yule ambaye moyoni mwake alikuwa na imani sawa na mbegu ya hardali.”[4]

Ni dalili inayoonyesha kuwa imani inashuka mpaka inakuwa na uzito sawa na mbegu ya hardali ndani ya moyo.

Vivyo hivyo maneno Yake (Ta´ala):

هُمْ لِلْكُفْرِ يَوْمَئِذٍ أَقْرَبُ مِنْهُمْ لِلْإِيمَانِ

“Wao siku ile walikuwa karibu na ukafiri kuliko imani.”[5]

Ni dalili inayofahamisha kuwa imani inashuka mpaka inakuwa karibu na ukafiri. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Yule katika nyinyi anayeona maovu basi ayazuie kwa mkono wake, asipoweza, basi afanye hivo kwa kuzungumza, asipoweza basi afanye hivo kwa moyo wake. Hiyo ni imani dhaifu kabisa.”[6]

Ni dalili inayoonyesha kuwa imani hudhoofika na inapungua. Kwa hiyo imani inazidi kwa matendo mema na inashuka kwa maasi.

[1] 08:02

[2] 09:124

[3] 74:31

[4] al-Bukhaariy (22) na Muslim (184).

[5] 04:167

[6] Muslim (49).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 205-206
  • Imechapishwa: 21/01/2021