Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimsikia mtu akiomba ndani ya swalah yake pasi na kumtukuza Allaah (Ta´ala) na wala hakumsifu yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambapo akasema: “Amefanya haraka.” Kisha akamwita na akamwambia yeye na wengine:

“Pindi mmoja wenu anaposwali basi aanze kwanza kumhimidi na kumsifu Mola wake (Jalla wa ´Azz). Halafu amsifu Mtume na kisha baada ya hapo aombe anachotaka.”[1]

Alimsikia (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) mtu mmoja anaswali akamtukuza na kumshukuru na kumsifu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambapo akasema:

“Omba utaitikiwa. Uliza utapewa.”[2]

[1] Ahmad, Abu Daawuud, Ibn Khuzaymah (2/83/1) na al-Haakim ameisahihisha na adh-Dhahabiy akaafikiana naye.

Tambua kwamba Hadiyth hii ni dalili inayoonyesha kuwa ni wajibu kumsifu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika Tashahhud hii. Haya ndio maoni ya ash-Shaafi´iy na Ahmad katika maoni yake ya mwisho yaliyopokelewa kwake. Kabla yao walikuwa na maoni tofauti kutoka kwa kundi la Maswahabah. Bali al-Ajurriy amesema:

“Yule asiyemsifu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika Tashahhud yake ya mwisho basi ni wajibu kwake kuirudi swalah yake.” (ash-Shariy´ah, uk. 415).

Kwa ajili hiyo ni dhuluma kumtuhumu ash-Shaafi´iy kwamba amepondoka katika suala hili kwa vile anaonelea kuwa kitendo hicho ni wajibu, kama alivyobainisha Faqiyh al-Haytamiy katika ”ad-Durr al-Mandhuud fiys-Swalaati was-Salaami ´alaa Swaahib-il-Maqaam al-Mahmuud” (13-16).

[2] an-Nasaa’iy kwa cheni ya wapokezi Swahiyh.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Swifatu Swalaat-in-Nabiy, uk. 158-159
  • Imechapishwa: 08/01/2019