96. Nguzo sita za imani na ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah juu ya mtenda dhambi kubwa

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Nguzo zake ni sita: Kumuamini Allaah, Malaika Wake, Vitabu Vyake, Mitume Yake, kuamini siku ya Mwisho na uamini Qadar; kheri na shari yake.

MAELEZO

Imani imejengeka juu ya nguzo na tanzu. Ni ipi tofauti kati ya mawili hayo? Tofauti ni kwamba nguzo ni kitu ambacho ni cha lazima. Kukiondoka kitu katika hizo basi imani inaondoka. Kwa sababu kitu hakisimami isipokuwa juu ya imani. Kukikosekana nguzo katika nguzo za kitu basi hakisimami. Kuhusu tanzu ni zenye kukamilisha. Imani haiondoki kwa kukosekana kitu katika hayo. Lakini ni yenye kukamilisha ima kwa njia ya ulazima au kwa njia ya kupendekeza. Mambo ya wajibu kwa sababu ya kuikamilisha imani yanakuwa ni wajibu na mambo ya kupendekeza kwa ajili ya kuikamilisha imani yanakuwa ni yenye kupendekeza. Muislamu akiacha kitu katika mambo ya wajibu au akifanya kitu katika mambo ya haramu imani yake haiondoki kikamilifu kwa mujibu wa Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah. Lakini kinachoondoka ni ukamilifu wake wa wajibu na hivyo ima anakuwa ni mwenye imani pungufu au fasiki. Ni kama ambavo akinywa pombe, akiiba, akizini au akifanya kitu katika dhambi kubwa basi mtu huyu anakuwa amefanya jambo la haramu na dhambi kubwa. Lakini hata hivyo hakufuru kwa jambo hilo na wala hatoki nje ya imani. Bali anakuwa ni mtenda dhambi na anasimamishiwa adhabu ikiwa maasi hayo ni yenye kupelekea kusimamishiwa adhabu. Vivyo hivyo inahusiana na yule mwenye kuacha jambo la lazima kama mfano wa mwenye kuacha kuwatendea wema wazazi wawili au kuwaunga ndugu, mambo ambayo ni lazima. Yule mwenye kuyaacha imani yake inapungua na anakuwa ni mtenda dhambi kwa kuacha jambo la lazima. Hivyo anakuwa ni mtenda dhambi ima kwa sababu ya kuacha jambo la lazima au kwa sababu ya kufanya jambo la haramu. Kwa hali zote hizo hatoki nje ya imani. Anakuwa ni muumini mwenye imani pungufu.

Haya ndio madhehebu ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah. Hayo ni tofauti na Khawaarij na Mu´tazilah ambao wanamkufurisha mtenda dhambi kubwa. Khawaarij wanamkufurisha na wanamtoa nje ya dini. Mu´tazilah pia wanamtoa nje ya dini. Lakini hata hivyo hawamwingizi ndani ya ukafiri. Wanasema kuwa yuko katika daraja kati ya daraja mbili; sio muumini na wala sio kafiri. Haya ndio madhehebu yao. Ni madhehebu yaliyozuliwa yanayopingana na dalili na yanayopingana na ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah. Sababu ya hilo ni kufupika kwao katika dalili ambapo wametendea kazi dalili za matishio na wakaacha dalili za ahadi kama mfano wa maneno Yake (Ta´ala):

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ

“Hakika Allaah hasamehi kushirikishwa na anasamehe yaliyo chini ya hayo kwa amtakae.”[1]

Hii ni miongoni mwa dalili za ahadi zilizofahamisha kwamba mtenda dhambi ambaye hakufikia kiwango cha kufuru na shirki ni mwenye kutarajiwa kwake msamaha na kwamba yuko katika khatari ya kuadhibiwa. Inatakiwa kuoanishwa na maneno Yake (Ta´ala):

وَمَن يَعْصِ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ فَإِنَّ لَهُ نَارَ جَهَنَّمَ خَالِدِينَ فِيهَا أَبَدًا

“Na yeyote yule atakayemwasi Allaah na Mtume Wake, basi hakika atapata Moto wa Jahannam hali ya kuwa wenye kudumu humo milele.”[2]

Mwenye kuchukua udhahiri wake atakafirisha moja kwa moja kwa madhambi. Lakini ikirejeshwa katika maneno Yake (Ta´ala):

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ

“Hakika Allaah hasamehi kushirikishwa lakini anasamehe yaliyo chini ya hayo kwa amtakaye.”[3]

basi haki itabainika na kwamba hatoki nje ya dini. Lakini hata hivyo ni mwenye kutishiwa Moto. Allaah akitaka, atamsamehe, na akitaka atamuadhibu. Anaweza kupitikiwa na vitu vyenye kufuta dhambi zake duniani au akaadhibiwa ndani ya kaburi na ikawa ni sababu ya kusamehewa madhambi yake hayo. Vitu vyenye kufuta dhambi za mtu ni nyingi. Anaweza kujaribiwa kwa majanga mbalimbali, akajaribiwa kwa adhabu mbalimbali duniani, akaadhibiwa ndani ya kaburi au akacheleweshwa mpaka siku ya Qiyaamah na hivyo akawa chini ya matakwa ya Allaah. Haya ndio madhehebu ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah.

[1] 04:48

[2] 72:23

[3] 04:48

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 201-205
  • Imechapishwa: 20/01/2021