95. Dalili katika Sunnah kwamba imani ni kuzungumza, kuamini na matendo

Tanzu za imani ni nyingi kama mnavojua. Ni sehemu sabini na kitu. Imaam al-Bayhaqiy ametunga kitabu kikubwa ambacho amebainisha tanzu za imani. Ana kitabu vilevile kilichoeleza kwa ufupi ambacho kimechapishwa.

Miongoni mwa dalili za wanachuoni kwamba imani ni kuzungumza kwa mdomo, kuamini ndani ya moyo na matendo ya viungo ni maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Ya juu yake ni neno “hapana mungu wa kweli isipokuwa Allaah.”

Ni dalili ya kuzungumza.

Maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Ya chini yake ni kuondosha kitu chenye kudhuru katika njia.”

Kitendo hichi kimefahamisha kuwa matendo yanaingia katika imani.

Maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hayaa ni sehemu katika imani.”

Kitu hichi kinakuwa ndani ya moyo. Hayaa inakuwa moyoni. Hii ni dalili inayoonyesha kuwa imani ni kuzungumza kwa mdomo, kuamini moyoni na matendo ya viungo.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 201
  • Imechapishwa: 20/01/2021